Sanders aitaka Marekani iondoe askari wake Saudia, iache kuiuzia silaha
Oct 08, 2022 06:50 UTC
Seneta wa kujitegemea aliyekuwa pia mgombea uteuzi wa kuwania urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic ametoa wito wa kuondolewa wanajeshi wa Marekani nchini Saudi Arabia na kukomeshwa kwa misaada ya kijeshi kwa Ufalme wa kihafidhina wa nchi hiyo kwa sababu ya kupunguza uzalishaji wa mafuta.
Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa Twitter, Bernie Sanders amesema:"ikiwa Saudi Arabia, moja ya wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu duniani, inataka kushirikiana na Russia kupora bei za gesi ya Marekani, inaweza pia kumwezesha Putin kulinda ufalme wake".
Seneta huyo wa jimbo Vermont aliandika ujumbe huo jana siku moja baada ya Umoja wa OPEC+ kutangaza kupunguza uzalishaji wake wa mafuta kwa siku.
Sanders amesisitiza kwa kusema: "lazima tuwaondoe wanajeshi wote wa Marekani kutoka Saudi Arabia, tuache kuwauzia silaha na tukomeshe udalali wake wa kupanga bei za mafuta".
Seneta huyo alielezea hisia kama hizo siku ya Jumatano aliposema, Marekani lazima ikomeshe udalali haramu wa upangaji bei unaofanywa na OPEC, uondoe usaidizi wa kijeshi kwa Saudi Arabia, na kuchukua hatua za haraka kwa ajili ya kutumia nishati jadidika.../