Rais wa FIFA: Hakuna pombe viwanjani wakati wa Kombe la Dunia
(last modified Sun, 20 Nov 2022 02:44:47 GMT )
Nov 20, 2022 02:44 UTC
  • Rais wa FIFA: Hakuna pombe viwanjani wakati wa Kombe la Dunia

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) amepuulizia mbali mashinikizo ya kutaka kuruhusiwa pombe viwanjani wakati wa fainali za Kombe la Dunia zinazoanza leo nchini Qatar.

Baada ya serikali ya Qatar kutangaza kuwa haitaruhusu vileo uwanjani wakati wa mechi za Kombe la Dunia nchini humo, nchi za Magharibi zililalamika na kukosoa vikali msimamo huo.

Bosi wa FIFA ameunga mkono msimamo huo wa serikali ya Doha na kusisitiza kuwa, hakuna dharura yotoye ya kulewa wakati wa mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani.

Katika kikao na waandishi wa habari kabla ya kuanza fainali hizo jana Jumamosi, Gianni Infantino, Rais wa FIFA alisema, "Binafsi naamini kuwa, ukikosa kunywa bia kwa masaa matatu kwa siku hautakufa."

Infantino ameeleza bayana kuwa, kutouzwa pombe ndani na nje ya uwanja wa soka si jambo geni, kwani linafanyika pia katika nchi za Ufaransa, Uhispania na Scotland.

Shirikisho la Kimataifa la Kandanda limesema halitaruhusu mashabiki wa soka wauziwe pombe ndani na nje ya viwanja vyote vinane vikavyoshuhudia mechi hizo za Kombe la Dunia nchini Qatar. Tayari kampuni ya pombe ya Budweiser ya Marekani ilikuwa imeweka vibanda vya kuuzia vileo nje ya viwanja hivyo.

Kabla ya hapo,  Gianni Infantino, Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) aliyaandikia barua mashirikisho ya soka ya timu 32 zinazoshiriki Kombe la Dunia, akiyataka yajiepushe na masuala ya siasa katika fainali hizo.

Baadhi ya nchi za Magharibi zilikuwa zinataka kutumia majukwaa ya mashindano hayo kupigia debe masuala ya ushoga na ubaradhuli, huku zingine zikishinikiza kuondolewa timu ya taifa ya soka ya Iran kwenye fainali hizo, na nafasi yake ichukuliwe na Ukraine.