IRC: Mabadiliko ya tabianchi yanazidisha migogoro ya binaadamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i91702-irc_mabadiliko_ya_tabianchi_yanazidisha_migogoro_ya_binaadamu
Kulingana na matokeo ya utafiti wa "Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji", mabadiliko ya hali ya hewa yatazidisha kasi ya migogoro ya wanaadamu katika mwaka ujao wa 2023 na kuongeza migogoro mengine ya kiuchumi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 14, 2022 23:10 UTC
  • IRC: Mabadiliko ya tabianchi yanazidisha migogoro ya binaadamu

Kulingana na matokeo ya utafiti wa "Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji", mabadiliko ya hali ya hewa yatazidisha kasi ya migogoro ya wanaadamu katika mwaka ujao wa 2023 na kuongeza migogoro mengine ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Reuters, matokeo ya utafiti wa shirika lisilo la kiserikali la "International Rescue Committee" (IRC) yanaonesha kuwa, mabadiliko ya hali ya hewa mwaka 2023 yataongeza kasi ya migogoro ya wanaadamu duniani kote na kuzidisha matatizo yanayosababishwa na mapigano ya silaha na mdorora wa kiuchumi.

Shirika hilo la misaada ya kibinadamu lenye makao yake makuu mjini New York, limetangaza kwamba, idadi ya watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu imeongezeka sana katika muongo mmoja uliopita na kufikia milioni 339 na laki mbili, ikilinganishwa na milioni 81 mwaka 2014.

Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji imeeleza kuwa, mabadiliko ya hali ya hewa ni miongoni mwa mambo muhimu yanayoharakisha dharura za kibinadamu, ilhali nchi 20 zilizoko kwenye orodha ya nchi zinazohitaji misaada ya dharura ya IRC, kama vile Haiti na Afghanistan, zinachangia sehemu ndogo sana ya asilimia mbili tu duniani ya uzalishaji wa kaboni dioksidi.

IRC:  Mabadiliko ya hali ya hewa yanazidisha  migogoro ya wanaadamu 

Katika utafiti wake, shirika hilo la kimataifa limesisitiza kuwa, sambamba na kuongezeka kwa changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hali imekuwa mbaya zaidi hasa baada ya janga la virusi vya corona na vita nchini Ukraine.

Hapo awali, katika mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa uliofanyika nchini Misri, Umoja wa Mataifa ulitangaza kwamba athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa wakimbizi ni "suala kubwa" ambalo lazima lishughulikiwe kupitia hatua za kimataifa.

Umoja wa Mataifa umezitaka nchi zilizoendelea kuchukua hatua zaidi za kulinda mazingira, kuharakisha mwenendo wa kuelekea kwenye nishati jadidika na kuhakikisha usalama wa binadamu.