Feb 21, 2023 10:54 UTC
  • Jeshi la Marekani mchafuzi mkubwa zaidi wa hewa Mashariki ya Kati

Ripoti iliyotolewa na tovuti ya habari ya Middle East Eye inaonyesha kuwa jeshi la Marekani ni moja ya wasababishaji wakubwa zaidi wa uchafuzi unaoleta mabadiliko ya hali ya hewa katika Mashariki ya Kati.

Katika miongo mitatu iliyopita, uzalishaji wa gesi chafuzi umeongezeka mara tatu katika maeneo mbalimbali duniani yakiwemo ya Mashariki ya Kati na Afrika na kupelekea joto la sayari ya dunia kufikia mara mbili ya wastani wa kimataifa.
Tovuti ya habari ya Middle East Eye imetangaza ikinukuu ripoti ya jarida la Forbes, kwamba Marekani ndiyo nchi inayozalisha silaha kwa wingi zaidi duniani na kuwa nchi hiyo inapasa itambulike kama moja ya wasababishaji wakuu wa uzalishaji wa gesi chafuzi, huku Washington ikiwa pia miongoni mwa watumiaji wakubwa zaidi wa mafuta katika sayari hii ya dunia.
Nita Crawford, mkurugenzi wa sasa wa mradi wa makadirio ya gharama za vita katika Chuo Kikuu cha Brown nchini Marekani amesema: gesi zinazozalishwa na silaha za kijeshi za Marekani kila mwaka ni zaidi ya gesi zote zinazozalishwa na nchi kubwa za viwanda.

Kulingana na mradi wa makadirio ya gharama za vita, kuanzia mwaka 2001 hadi 2017, jeshi la Marekani lilizalisha takriban tani bilioni 1.2 za gesi ya kaboni dioksidi, ambapo tani milioni 400 kati ya hizo zilizalishwa baada ya Septemba 11 katika vita na mapigano katika nchi za Afghanistan, Iraq, Pakistan na Syria.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, madhara makubwa zaidi yanayosababishwa na gesi chafuzi za sekta ya kijeshi na silaha za Marekani ni katika matumizi ya mafuta ya ndege, ambayo ni mengi zaidi mara mbili hadi nne kulinganisha na fueli nyinginezo.
Kwa mujibu wa Bi. Crawford, kama Marekani ina nia ya dhati ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, katika hatua ya kwanza inapaswa ipunguze uzalishaji wa gesi hizo katika viwanda vyake vya silaha.
Ripoti hiyo imemalizia kwa kueleza kwamba, moja ya tabia ya Marekani ni kuchoma moto taka inazozalisha katika maeneo yalipo majeshi yake, hatua ambayo husababisha kusambaa pia gesi mbalimbali na uchafuzi wa sumu katika hewa.../

 

Tags