Russia: Jinai za kivita za Marekani na Nato Afghanistan zimepuuzwa
Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo kuwa jinai za kivita za Marekani na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) huko Afghanistan zimepuuzwa.
Marekani na waitifaki wake Oktoba 7, 2001 ziliivamia na kuanza kuikalia kwa mabavu Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kulinda usalama wa nchi hiyo.
Wanajeshi wa Marekani baada ya kuikalia kwa mabavu Aghanistan kwa miaka 20 na kutenda jinai chungu nzima ikiwa ni pamoja na kuharibu miundombinu ya kiuchumi na huduma za afya; hatimaye mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka jana waliondoka nchini humo kwa fedheha baada ya kugonga mwamba juhudi zao. Kundi la Taliban pia katikati ya mwezi huo wa Agosti liliingia madarakani na kushika hatamu za kuiongoza nchi hiyo.
Vasily Nebenzya Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Russia Umoja wa Mataifa aliashiria jana katika kikao cha Baraza la Usalama kuhusu kupuuzwa jinai za kivita zilizotekelezwa na Marekani na Nato dhidi ya wananchi wa Afghanistan na kuzituhumu nchi za Magharibi kwa kutokuwa na azma na kuonyesha hamu ya kutekeleza miradi ya kweli ya kuiletea maendeleo Afghanistan.
Nebenzya pia ametaka kuachiwa fedha za Afghanistan zinazoshikiliwa katika benki za nchi za Magharibi. Marekani imezuia dola bilioni kumi za Benki Kuu ya Afghanistan kwa kisingizio cha kuingilia madarakani kundi la Taliban. Muda mfupi baada ya kuzuiwa fedha hizo tajwa, Washington ilitangaza kuwa itataifisha dola bilioni tatu miongoni mwa fedha hizo kwa maslahi ya wahanga wa tukio la Septemba 11, na baadaye kidogo, iliamua kuhamishia Uswisi dola bilioni 3.5 mali ya Afghanistan.