Feb 09, 2023 11:59 UTC
  • Korea Kaskazini yaonyesha makombora mapya ya kuvuka mabara ya ICBM

Korea Kaskazini imeonyesha makombora yake mapya ya kisasa kabisa ya balestiki, yenye uwezo wa kuvuka mabara ya ICBM.

Pyongyanga ilizindua makombora hayo yenye uwezo kamili wa kufanya shambulio la nyuklia, katika gwaride kubwa la kiijeshi lililofanyika usiku wa kuamkia leo.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA, Pyongyang imefanya gwaride hilo kubwa la kijeshi kwa mnasaba wa kuadhimisha miaka 75 tangu kuasisiwa vikosi vya kijeshi vya nchi hiyo.

Gwaride hilo limehudhuriwa na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, mke wake, binti yake, na makamanda wa ngazi za juu wa vikosi vya jeshi la nchi hiyo.

Picha na video zilizosambazwa na KCNA zinaonesha jeshi la Korea Kaskazini likionyesha kwa akali makombora 11 ya Hwasong-17, ambayo ndiyo makombora makubwa zaidi ya ICBM ya nchi hiyo. Kombora hilo lilifanyiwa majaribio ncini humo kwa mara ya kwanza mwaka uliopita 2022.

Kombora la ICBM la Korea Kaskazini

Mbali na ICBM, silaha nyingine za kimkakati zilizooneshwa kwenye gwaride hilo ni makombora ya cruise ya masafa marefu, na mfumo wa makombora ya balestiki ya masafa mafupi ya SRBM.

Korea Kaskazini imekuwa ikiendelea kustawisha uwezo wake wa silaha za makombora tangu yalipokwama mazungumzo ya kuishinikiza itokomeze silaha zake za nyuklia na makombora ya balestiki, mkabala wa kupunguziwa vikwazo vilivyolemaza uchumi wa nchi hiyo.

Tags