Mwangwi wa mauaji ya mbunge wa Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i9418-mwangwi_wa_mauaji_ya_mbunge_wa_uingereza
Mauaji ya Jo Cox, mbunge wa Chama cha Labour katika Bunge la Uingereza yamezusha malalamiko makubwa ndani na nje ya nchi hiyo na kulitia wahka na hofu kubwa bunge hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 18, 2016 02:00 UTC
  • Mwangwi wa mauaji ya mbunge wa Uingereza

Mauaji ya Jo Cox, mbunge wa Chama cha Labour katika Bunge la Uingereza yamezusha malalamiko makubwa ndani na nje ya nchi hiyo na kulitia wahka na hofu kubwa bunge hilo.

Mbunge Jo Cox alipigwa risasi Akhamisi iliyopita kisha akadungwa kisu na alifariki dunia baadaye kidogo akiwa hospitalini kutokana na majeraha makali. Polisi ya Uingereza imemtia nguvuni mtu aliyemshambulia mbunge huyo kwa jina la Thomas Mair mwenye umri wa miaka 52. Polisi ya Uingereza imetangaza kuwa, Mair ana fikra na mielekeo ya kundi lenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na kwamba wakati anamfyatulia risasi mbunge huyo alikuwa akinadi kwa sauti kubwa akisema: "Britain First" (Uingereza Kwanza). Britain First ni kundi lenye mielekeo ya utaifa na misimamo mikali ya mengo wa kulia lililoanzishwa mwaka 2011 na mwanachama wa zamani wa chama cha kitaifa cha Uingereza, Paul Golding. Chama hicho kinapinga vikali suala la kuingia wahajiri nchini Uingereza na hakikubali kuwepo tamaduni mbalimbali hususan ustawi na kuenea kwa Uislamu nchini humo.

Kundi hilo la Britain First ambalo kwa sasa halina hata mwakilishi mmoja katika mabunge ya kieneo na kitaifa ya Uingereza au katika Bunge la Ulaya, lilitangaza alasiri ya Alkhamisi iliyopita kwamba halikuhusika katika mauaji ya Jo Cox.

Kiongozi wa Chama cha Labour, Jeremy Corbyn, ametoa taarifa akisema chama hicho na Uingereza nzima imeshtushwa sana na mauaji ya kutisha ya Jo Cox. Corbyn amesema, Jo Cox alifanya jitihada kubwa katika uwanja wa huduma za umma na haki za binadamu kupitia ushirikiano wake ya jumuiya ya Oxfam, Mfuko wa Kupiga Vita Utumwa na Mfuko wa Uhuru. Amesisitiza kuwa, Cox ameuawa akitekeleza majukumu yake ya kibunge na kwamba suala hilo lina umuhimu mkubwa kwa Bunge la Uingereza.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema mauaji ya mbunge huyo ni tukio la kusikitisha mno. Viongozi na shakhsia mbalimbali wa kisiasa wa Uingereza pia wamelaani mauaji ya mbunge Cox na kuyataja kuwa ni ya kutisha.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza pia amekaribisha hatua ya kusitishwa kampeni zote za kuunga mkono au kupinga suala la Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya (Brexit) kufuatia muaji ya mbunge huyo.

Mume wa mbunge Jo, Brendan Cox amesema mke wake daima amekuwa akifanya jitihada za kung'oa mizizi ya hisia na fikra za chuki zilizosababisha mauaji yake. Bi Cox ambaye alikuwa na watoto wawili alikuwa mwanachama wa chama cha Labour na alishinda kiti cha Bunge la Uingereza katika uchaguzi wa mwaka 2015. Kabla ya kuingia bungeni Jo Cox alikuwa miongoni mwa wakurugenzi wa taasisi ya hisani ya Oxfam. Mbunge huyo alikuwa mkuu wa Kundi la Marafiki wa Syria katika Bunge la Uingereza na alikuwa mpinzani mkubwa wa aina yoyote ya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo. Cox pia alikuwa miongoni mwa wabunge wa Uingereza wanaotoa wito wa kukubaliwa wakimbizi wa Syria nchini humo kwa sababu za kibinadamu. Vilevile alikuwa mpinzani wa suala la Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya na ameuawa wiki moja tu kabla ya kura muhimu ya maoni ya kuamua iwapo wananchi wanataka nchi hiyo ijiondoe katika umoja huo au la.

.