Maandamano dhidi ya vita katika nchi za Ulaya
(last modified Mon, 27 Feb 2023 11:44:54 GMT )
Feb 27, 2023 11:44 UTC
  • Maandamano dhidi ya vita katika nchi za Ulaya

Sambamba na kuendelea vita nchini Ukraine na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii katika nchi mbalimbali za Ulaya, wananchi barani humo wamefanya maandamano katika nchi kadhaa wakipinga sera za nchi za Magharibi na kuingilia kati vita vya Ukraine.

Kuhusiana na hili, maelfu ya watu kutoka makundi tofauti ya kisiasa walikusanyika jana mjini Berlin wakitaka kuanza mazungumzo ya amani na kumalizika vita nchini Ukraine. Maandamano hayo yalifanyika kuunga mkono wito wa "Manifesto ya Amani" iliotolewa na mwandishi na mbunge wa chama cha kushoto, Sahra Wagenknecht. Pia, mamia ya raia wa Uhispania, Italia na Uingereza wamefanya maandamano wakipinga sera za kuchochea vita za Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) wakizitaja kuwa ndiyo sababu kuu ya kuzuka na kurefuka muda wa vita nchini Ukraine.

Kurefusha vita vya Ukraine na matokeo yake hasi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa katika maisha ya raia wa nchi za Ulaya kumezidisha maandamano yanayokosoa utendaji wa serikali za nchi za Ulaya kuhusiana na vita vya Ukraine. Ni takriban mwaka mmoja sasa ambapo nchi za Ulaya zimekuwa zikiisaidia Ukraine kwa kutuma silaha na kupasisha vikwazo mtawalia dhidi ya Russia. Sera hizi zimesababisha matatizo ya kiuchumi na kijamii kwa raia wa nchi za Ulaya. Ongezeko la bei ya mafuta, uhaba wa chakula na mfumuko wa bei wa kila uchao katika nchi hizo vimezusha malalamiko na hali ya kutoridhishwa wananchi na utendaji wa serikali na sera zao za kuchochea moto wa vita huko Ukraine.

Kwa sababu hiyo, katika siku ya kumbukumbu ya kuanza vita huko Ukraine, makundi ya kiraia, mashirika ya kupinga vita, jumuiya za kutetea haki za binadamu na wanaharakati wa masuala ya kijamii katika nchi tofauti za Ulaya wamefanya maandamano na mikusanyiko mingi kupinga sera za vita za nchi za Magharibi. Washiriki wa maandamano hayo, waliokuwa wamebeba mabango yanayopinga vita vya Ukraine na sera za Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), wametoa wito wa kukomeshwa vita hivyo na kusitishwa misaada ya silaha ya Magharibi kwa Ukraine.

Mwanaharakati wa kupinga vita, Dalia Sanchez anasema: "Watu wengi wamepoteza maisha katika vita vya Ukraine, bila kujali wapo upande gani. Sikubaliani na kupeleka silaha Ukraine, hatua hii itarefusha vita na mapigano."

Licha ya malalamiko hayo, lakini viongozi wa nchi za Ulaya wanasisitiza kuendelezwa sera za vita vya Ukraine na kwa hakika wanachochea vita hivi kwa kutoa silaha za kisasa kwa serikali ya Kiev. Ripoti zinaonyesha kuwa, Umoja wa Ulaya umetoa msaada wa kijeshi wa takriban dola bilioni 12 kwa Ukraine. Hii ni licha ya kwamba, mbali na athari za kiuchumi na kijamii zilizosababishwa na vita hivyo, raia wengi wa nchi za Ulaya wana wasiwasi kwamba misaada ya silaha za kisasa kwa vikosi vya jeshi la Ukraine vitavifanya vita hivyo kuwa vya kimataifa au hata vita vya nyuklia kati ya madola makubwa ya dunia.

Mwanasiasa wa Ufaransa, Marine Le Pen anasema kuhusiana na suala hili: "Vita hivi hadi sasa vimesababisha kukatika uhusiano kati ya Ulaya na Russia na vimeifanya Moscow kuwa mshirika bora zaidi wa Beijing na New Delhi. Umewadia wakati wa kuelekeza juhudi zetu upande wa kurejesha amani nchini Ukraine."

Marine Le Pen

Alaa kulli hal, wasiwasi kuhusu kuendelea vita nchini Ukraine na hatari ya kupanuka wigo wake na kuchukua muda mrefu zaidi inaongezeka siku baada ya nyingine. Hata hivyo na licha ya hatua za wanasiasa wa Ulaya za kuendelea kuingilia kati vita vya Ukraine; raia wa nchi za bara hilo wamechoshwa na sera hizo za kuchochea moto wa vita.

Inaonekana kuwa iwapo hitilafu na mwendo huu utaendelea, nchi za Ulaya zitakabiliwa na matatizo mapya ya kisiasa na kijamii.