Ofisi ya UN: Mapatano ya Iran, Saudia yataharakisha usitishaji vita Yemen
(last modified Sun, 12 Mar 2023 07:38:22 GMT )
Mar 12, 2023 07:38 UTC
  • Ofisi ya UN: Mapatano ya Iran, Saudia yataharakisha usitishaji vita Yemen

Ofisi ya ubalozi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imepongeza mapatano ya kurejesha tena uhusiano wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Saudi Arabia na kueleza kuwa, muafaka huo utaharakisha mchakato wa kusitishwa vita na mapigano nchini Yemen.

Ofisi hiyo ya kudumu ya Iran yenye makao yake mjini New York ilisema hayo jana Jumamosi, siku moja baada ya Iran na Saudi Arabia kukubaliana kuanzisha tena uhusiano kati ya pande mbili kwa upatanishi wa China baada ya mkwamo wa miaka saba.

Taarifa ya ofisi hiyo ya kidiplomasia ya Iran mjini New York imeeleza kuwa, kuhuishwa uhusiano wa Tehran na Riyadh kutakuwa na taathira chanya kwa pande tatu; uhusiano wa pande mbili (iran na Saudia), wa kieneo na kimataifa.

Kadhalika taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, kufufuliwa uhusiano wa kisiasa wa Iran na Saudia kutaharakisha mchakato wa kuhitimishwa mgogoro wa nchini Yemen, sanjari na kuimarisha uhusiano katika umma wa Kiislamu.

Aidha hapo jana, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitoa taarifa ya kupongeza mapatano hayo ya kurejesha tena uhusiano wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imesema muafaka baina ya Iran na Saudia ni kwa maslahi ya Wairani, mataifa ya Kiislamu, na nchi rafiki katika eneo la Asia Magharibi.

Riyadh ilikata uhusiano wake na Iran tokea mwaka 2016, kwa kisingizio cha kushambuliwa ubalozi na ubalozi wake mdogo mjini Tehran na katika mji wa Mash'had; kitendo ambacho kililaaniwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Tags