Watoto karibu 50 kutoka familia za magaidi wa Daesh kuhamishiwa Moscow
Watoto karibu 50 wa familia za masalia ya magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh (ISIS) wamehamishwa katika mji mkuu wa Russia, Moscow.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, ujumbe wa Russia chini ya uongozi wa Maria Lova Bilova, Mwakilishi wa Rais Vladimir Putin katika Masuala ya Haki za Watoto ameeleza kuwa watoto 40 wenye asili ya Russia kutoka familia za masalia ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh wamerejeshwa Moscow wakitokea katika kambi zilizopo kaskazini mashariki mwa Syria.
Kwa mujibu wa uamuzi uliochukuliwa na Moscow mwaka 2017, watu wasiopungua 341 wenye asilia ya Russia kutoka familia za magaidi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh wakiwemo watoto kadhaa yatima walirejeshwa Russia kati ya mwaka 2018 hadi 2021.
Nchi chache ikiwa ni pamoja na Uzbekistan, Kazakhstan na Kosovo zimekubali kuwapokea watu wa familia za masalia ya magaidi wa Daesh kutoka katika kambi za wakimbizi huko kaskazini mashariki mwa Syria, na baadhi ya wengine khususan nchi za Ulaya zimekubali kupokea idadi maalumu ya watu hao hasa watoto wa masalia ya magaidi hao wa Daesh.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, karibu watu elfu 56 wanaishi katika kambi ya al Hol yapata umbali wa kilomita 15 kutoka katika mpaka wa pamoja wa Syria na Iraq. Al Hol ni kambi kubwa zaidi yenye wanamgambo masalia wa kundi Daesh huko Iraq na Syria.