Mar 23, 2023 12:21 UTC
  • Mama: Askari wa Marekani waliomuua mwanangu ni wanyama

Mama mzazi wa Ivor Otieno, kijana Mkenya aliyeuawa hivi karibuni na polisi ya Marekani akiwa korokoroni amewataja askari polisi waliofanya ukatili huo kuwa wanyama.

Otieno aliaga dunia Machi 6 mikononi polisi katika mji wa Petersberg jimboni Virginia, katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa vitendo vya polisi ya Marekani vya kuwapiga, kuwanyanyasa na hata kuwaua Wamarekani weusi.

Caroline Ouko, mamake Otieno amesema alisikitishwa na mauaji hayo ya kinyama ya mwanawe, ambaye alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya kisaikolojia ya Bipolar (hisia zinazobadilika).

Amesema licha ya kujaribu kuwaeleza maafisa wa polisi kwamba kijana wake huyo aliyekuwa na umri wa miaka 28 alikuwa na maradhi ya kiakili, lakini hawakumsikiliza na waliamiliana naye kinyama wakati wa kumkamata na hata alipokuwa korokoroni.

Aidha Caroline Ouko amesema Mahakama Kuu ya Wilaya ya Henrico ilikataa kumuachia huru kwa dhamana mwanawe huyo wa kiume aliyekuwa anakabiliwa na shitaka la wizi.

Kanda ya video iliyosambaa mtandaoni inaonesha kijana huyo akikandamizwa ardhini na askari polisi 10 wa Marekani kwa zaidi ya dakika 10, licha ya kuwa na pingu mikononi na nyororo miguuni.

Wakili wa familia ya Otieno, Ben Crump amesema kijana huyo wa Kenya mbali na kufungiwa kwenye seli ndogo iliyojaa kinyesi huku akiwa uchi, lakini siku ya kuaga kwake dunia alikandamizwa ardhini na maafisa wa polisi pamoja na kuwa alikuwa mtulivu.

Amesema, "Kwa mara nyingine, ukatili na nyama usio na mpaka wa polisi wa Marekani umemulikwa baada ya mauaji hayo (ya Otieno) yanayofanana na ya George Floyd miaka mitatu iliyopita. Otieno alikandamizwa ardhini na polisi kwa dakika 12 hadi akakata roho."

Mauaji ya Floyd 2020

Matokeo ya uchunguzi uliofanywa karibuni na taasisi ya Gallup yanaonesha kuwa, asilimia 64 ya Wamarekani waamini kuwa, ubaguzi wa rangi dhidi ya watu weusi umekithiri na kukita mizizi nchini Marekani. Vilevile asilimia 55 ya walioshiriki katika uchunguzi huo wa maoni wanaamini kuwa, mienendo ya polisi wa Marekani mkabala wa watu weusi si ya kiadilifu ikilinganishwa na mienendo yao kuhusiana na wazungu. 

Ikumbukwe kuwa, mauaji yaliyofanywa na afisa mmoja wa polisi ya Marekani kwa jina Derek Chauvin dhidi ya Mmarekani mweusi George Floyd tarehe 25 Mei mwaka 2020 yalizusha maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi ndani na nje ya Marekani chini ya vuguvugu la 'Black Lives Matter'.

Tags