Apr 12, 2023 02:12 UTC
  • Kiongozi wa Waislamu Canada: Waislamu kote nchini wana sababu ya kuwa na wasiwasi baada ya hujuma ya msikiti wa Ontario

Kiongozi wa Jumuiya ya Waislamu nchini Canada ameeleza wasiwasi wake kuhusu kushamiri vetendo vya chuki dhidi ya Uislamu nchini humo baada ya mwanamume mmoja kuvamia msikiti wa jimbo la Ontario Alhamisi iliyopita, kutoa vitisho sambamba na kujaribu kuwavamia waumini nje ya msikiti huo.

Qasir Nasir Khan, mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Markham, amewaambia waandishi wa habari kwamba mtu mmoja alifanya "vitendo kadhaa vya chuki dhidi ya Uislamu" nje ya msikiti huo, yapata kilomita 30 kaskazini mwa jiji la Toronto.

“Alitishia kuuchoma moto msikiti wetu na kutoa matusi dhidi ya Mtume Muhammad,” Khan alisema mbele ya mkutano na wanahabari. Qasir Nasir Khan amesema: "Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, mtu huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu alijaribu kuwagonga waumini kwa gari lake."

Aliongeza kuwa, kwa kuzingatia tukio hili na matukio mengine ya hivi karibuni ya chuki na hujuma dhidi ya Uislamu nchini Canada, "Waislamu kote nchini wana sababu ya kuwa na wasiwasi".

Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu nchini Canada amesema: "Ikiwa tunatazama mauaji ya Msikiti wa Quebec, au shambulio la London ambapo mtu mmoja aliangamiza familia nzima ya Waislamu kwa kuwagonga makusudi kwa lori lake, jamii zetu zina sababu za kuwa na hofu." Khan amesisitiza kuwa wangeweza kuwa kwenye mazishi baada ya hujuma ya juzi dhidi ya msikiti wa Ontario.

Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Kiislamu ya Markham (ISM), ambayo ni moja ya taasisi kongwe na kubwa zaidi za Kiislamu nchini Canada, ilisema kuwa Alhamisi iliyopita mtu mmoja alifika eneo hilo akiwa na gari ambapo aliingia msikitini na kurarua nakala ya Qur'ani Tukufu. Ilisema mbaguzi huyo aliyekuwa akitoa nara za ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu, alijaribu pia kuwagonga Waislamu waliokuwepo eneo hilo kwa gari lake.

Hujuma ya hivi majuzi ambayo imefanyika wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni ya karibuni zaidi katika kile viongozi wa Kiislamu nchini Canada wanakitaja kuwa ni ongezeko la unyanyasaji na wakati mwingine vitendo vya mauaji vinavyolenga jamii yao.

Mnamo mwaka wa 2017, mtu aliyekuwa na bunduki aliwaua wanaume sita wa Kiislamu waliokuwa wakisali katika msikiti mmoja katika Jiji la Quebec, na kusababisha mshtuko mkubwa kote nchini Canada na maeneo mengine ya dunia.

Mlinzi wa msikiti pia aliuawa katika eneo la Toronto mnamo 2020, wakati Juni 2021, watu wanne wa familia ya Kiislamu waliuawa, na mwanafamilia wa tano, mvulana mdogo, alijeruhiwa vibaya - wakati mbaguzi mmoja alipowagonga kwa lori lake huko London, Ontario.

Tags