Mar 21, 2024 07:50 UTC
  • Ukosoaji wa Afrika Kusini dhidi ya Israel kwa kukaidi uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema kuwa kutotekelezwa maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya Israel kunaidhoofisha mahakama hiyo.

Kufuatia malalamiko ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, mahakama hiyo imetoa uamuzi mwingine unaoutaka utawala huo wa kibaguzi kuchukua hatua za lazima kwa ajili ya kuzuia mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Kuhusiana na hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Naldi Pandour, katika hotuba yake katika taasisi ya Carnegie mjini Washington, amesema Israel imepuuza kabisa uamuzi huo, akiashiria mgogoro na hali ya njaa katika Ukanda wa Gaza, na kusema serikali ya Afrika Kusini imeiomba Mahakama ya Kimataifa ya Haki ichunguze haraka uamuzi wa Israel wa kupanua operesheni zake za kijeshi mjini Rafah na kuzuia jambo hilo mara moja.

Wakati huo huo, Volker Turk, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema, vikwazo na vizuizi vinavyowekwa na utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya kuzuia kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza ni jinai ya kivita.

Cindy McCain, mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), pia ameashiria ongezeko la vifo vinavyotokana na njaa katika Ukanda wa Gaza na kusema: "Kasi ya kuenea mgogoro wa njaa na utapiamlo katika Ukanda wa Gaza inatisha."

Umoja wa Mataifa umekuwa ukionya kwa wiki kadhaa sasa kwamba njaa inakarinia kuwaangamiza watu wa Gaza, ambapo mashirika ya misaada yameripoti kuwa ufikiaji eneo hilo, haswa kaskazini, ni mgumu.

Hata hivyo jinai za utawala wa Kizayuni bado zinaendelea ambapo unaendelea kuonyesha wazi ukatili wake katika kushambulia vituo vya afya na miundombinu ya afya. Katika jinai yake ya karibuni siku ya Jumatatu asubuhi, ulishambulia Hospitali ya Shafa huko Gaza, ambapo mbali na kuua shahidi Wapalestina wasio na hatia ulizingira mamia ya wakimbizi, wagonjwa, waandishi wa habari na wahudumu wa afya katika hospitali hiyo.

Mahakama ya ICJ

Kuhusiana na hilo, ofisi ya vyombo vya habari ya serikali ya Gaza imetangaza katika taarifa  kuwa: 'Jeshi la utawala ghasibu wa Israel limekiri kufanya jinai ya umwagaji damu kwa kuwanyonga raia zaidi ya 50 wa Kipalestina na kuwatia mbaroni wengine karibu 200 katika jengo la hospitali ya Shifa na maeneo ya pembeni. Kitendo hiki ni uhalifu wa wazi wa kivita na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.'

Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, alisema Jumanne usiku kwamba Israel inapinga kurejea maisha katika hali ya kawaida huko Gaza na wakati huo huo kuzuia mazungumzo ya Doha.

Pamoja na hayo, kuendelea mashambulizi ya kikatili ya Israel dhidi ya raia huko Gaza kumeibua ukosoaji kutoka kwa baadhi ya nchi za Magharibi. Giorgia Meloni Waziri Mkuu wa Italia akizungumza siku ya Jumanne katika Baraza la Seneti la nchi hiyo, alikosa mipango ya Israel ya kutaka kulishambulia eneo la Rafah huko Gaza na kusema: "Kufunguliwa njia mpya za ardhini na pia baharini kutoka Cyprus hadi Ukanda wa Gaza ni kipaumbele ili kuhakikisha uwasilishaji salama wa misaada ya kibinadamu katika ukanda huo."

Katika mahojiano na gazeti la Toronto Star, toleo la Jumanne usiku, Melanie Joly, Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada alitangaza uamuzi wa nchi hiyo wa kusimamisha uuzaji wa silaha kwa utawala wa Kizayuni.

Uamuzi huo umekuja baada ya wabunge wa Canada kupiga kura Jumatatu kwa ajili ya kuunga mkono mswada wa kupiga marufuku uuzaji silaha kwa Israel.

Tags