Umoja wa Mataifa watoa wito wa kukomeshwa vitendo vya ukatili dhidi ya asili
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kukomeshwa kwa vita vya kikatili na visivyo na maana dhidi ya asili, akisisitiza kwamba afya ya mwanadamu inategemea afya ya dunia, hewa tunayovuta, maji tunayokunywa na udongo ambao chakula chetu kinakua.
Antonio Gutterres ameyasema hayo katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia iliyoadhimishwa jana tarehe 22 Aprili na kuhimiza kufikiria kuhusu uhusiano wa mwanadamu na ulimwengu wa asili.
Ametoa wito wa kuimarishwa kwa hatua za kuzuia ongezeko la kasi la joto duniani na, katika suala hili, akahimiza ongezeko la uwekezaji katika miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ustahimilivu, hasa kwa nchi zilizo hatarini zaidi na jamii ambazo zimechangia kidogo katika kusababisha janga la tabianchi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, "mifumo ya ikolojia yenye afya, kuanzia bahari na mito hadi misitu na nyanda, pia ni muhimu kwa mapambano yetu dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa. Hebu turudi kwenye mstari na makubaliano ya kihistoria ya Umoja wa Mataifa kuhusu viumbe hai kulinda asilimia 30 ya ardhi na maji ya Dunia ifikapo mwaka 2030”.

Serikali lazima ziwe na jukumu kubwa katika kulinda maumbile, lakini muhimu vile vile ni jukumu la mashirika, taasisi na asasi za kiraia, pamoja na sifa za uongozi za watu wa asili ambao wametunza mazingira kwa maelfu ya miaka na wanaweza kutoa misaada mbalimbali ya suluhisho za majanga ya dunia, yanayohusiana na hali ya hewa na upotevu wa viumbe hai.
Siku ya Kimataifa ya Mama Duniani iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1970 ambapo takriban watu milioni 20, waliokasirishwa na umwagikaji wa mafuta, uchafuzi wa hewa na mito, waliingia mitaani kupinga janga la mazingira.