Apr 24, 2023 13:17 UTC
  • Ugunduzi wa makaburi 40 zaidi yasiyo na alama; ishara ya unyama dhidi ya wenyeji wa Canada.

Watafiti wametangaza kwamba wamegundua makaburi 40 yasiyo na alama katika shule ya zamani ya Wamishonari wa Kikatoliki huko British Columbia, nchini Canada.

Makaburi haya yapo katika Shule ya Bweni ya St. Augustine au maeneo ya karibu. Maeneo haya yamekaguliwa kwa ombi la jamaa wa Wacanada asilia waliozikwa katika makaburi hayo. 

Utafiti wa kwanza katika suala hili ulifanyika miaka michache iliyopita na ulitumia nyaraka zilizotolewa na watu walionusurika ukatili huo. Rada zinazopenya ndani ya ardhi zimetumika katika utafiti huu. Utafiti huo ulifanyika kwenye kampasi ya Shule ya Bweni ya St. Augustino. Shule hiyo ilifanya kazi kuanzia mwaka 1904 hadi 1975. Kulingana na utafiti huu, makaburi hayo yana kina kifupi sana, na miili ya watoto tu ndiyo inayoweza kuwekwa humo. Kwa kuzingatia suala hili, watoto waliokuwa wakisoma katika shule hiyo hawakuwa wa kaumu ya “shíshálh” tu, bali kutoka kaumu nyingine 51 ambazo watoto wao wameripotiwa kutoweka nchini Canada.

Mojawapo ya mifano ya wazi ya ukatili na mienendo ya kinyama iliyofanywa dhidi ya wenyeji wa Canada ni ugunduzi wa makumi ya makaburi ya watu hao. Mnamo mwaka 2021, makaburi kadhaa ya halaiki yaliyokuwa na miili ya mamia ya watoto wadogo waliozikwa humo yaligunduliwa katika maeneo ya shule za bweni za Wamisonari wa Kikristo katika maeneo mbalimbali ya Canada. Shule hizo za bweni zinamilikiwa na makanisa, ambayo yaliwatenganisha watoto wa wenyeji asilia wa Canada na wazazi wao  kwa lazima, katika jitihada za serikali za kutaka kubadilisha utambulisho na kuharibu mila na utamaduni wao. Madhumuni ya kuanzishwa shule hizo, ambazo ziliendeshwa na taasisi kadhaa za Kanisa Katoliki kati ya 1831 na 1996, yalikuwa kuwaingiza watoto hao katika utamaduni wa wazungu. Karibu watoto 150,000 walihamishwa kutoka makwao na kuwekwa kwenye shule hizo za Wamishonari ambako walikabiliwa na unyanyasaji, ubakaji na utapiamlo. Tume ya Ukweli na Maridhiano iliyoundwa kuchunguza suala hilo mwaka 2015 ililitaja suala hilo kuwa ni mauaji ya kimbari ya kitamaduni.

Mjadala wa muda mrefu na wa mara kwa mara juu ya maafa na masaibu yaliyotokea katika shule hizo uliibuka na kupewa mazingatio tena mwaka 2021 wakati mabaki ya watoto 215 yalipogunduliwa katika eneo la shule ya bweni ya Wacanada asilia katika mkoa wa magharibi wa British Columbia ambayo ilifungwa mnamo 1978. Inaaminika kuwa bado kuna mamia ya maeneo ambayo hayajagunduliwa ambapo miili ya waathiriwa wa ukatili wa shule hizo za Wamishonari wa Kikristo ilizikwa.

kugunduliwa makaburi haya ya umati kwa kweli ni ukumbusho wa ukweli mchungu kwamba tangu wazungu walipohamia Amerika Kaskazini, wenyeji wa Canada wamekuwa wakibaguliwa kimfumo na mchakato huo bado umeendelea hadi sasa. Ingawa Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, amejaribu kuzipa mamlaka madogo ya kujitawala baadhi ya kaumu za watu wa asili ili angalau kufidia na kufunika kashfa ya kufichuliwa makaburi ya maelfu ya wanafunzi wa wenyeji wa nchi hiyo, hata hivyo, ukubwa na kina cha ukandamizaji, ukatili wa wazaungu na ubaguzi dhidi ya watu wa asili wa Canada vimekita mizizi katika historia ya nchi hiyo na haiwezekani kufidia unyama huo kwa hatua hizo za kipropaganda.

Perry Belgerd, mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wenyeji wa Canada, anasema kwamba kupatikana makaburi ya watoto katika shule za zamani za bweni za Wamishonari sio jambo jipya, lakini ni jeraha la zamani ambalo kila wakati linapoonekana linaibua uchungu na maumivu.

Haya yote ni pamoja na kwamba, Canada inachukuliwa kuwa miongoni mwa nchi zinazodai kuwa vinara wa kutetea haki za binadamu na daima imekuwa ikifungua kinywa katika majukwaa ya kimataifa kama vile Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa na kuzikosoa vikali baadhi ya nchi ambazo zinapinga ukiritimba na sera za kibeberu za nchi za Magharibi.

Maelfu ya watoto wa Wcanada asilia waliuawa

Alaa kulli hal, rekodi ya haki za binadamu ya nchi hii ina madoa mengi yenye giza; mojawapo na muhimu zaidi ikiwa unyanyasaji na ukatili unaofanywa dhidi ya wenyeji wa Canada, vikwazo vya aina mbalimbali, ubaguzi na mashinikizo yamayofanywa kwa jamii hiyo. 

Tags