Dec 13, 2023 11:15 UTC
  • Wacanada waandamana wakimtaka Trudeau aache kuiuzia Israel silaha

Waungaji mkono wa Palestina wanaoishi nchini Canada wamefanya maandamano makubwa kulaani jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambapo mbali na kuonyesha mshikamano wao na wakazi wa Gaza, lakini pia wamemtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Justin Trudeau kuacha kuuuzia silaha utawala wa Kizayuni.

Waandamanaji hao waliokusanyika mbele ya Kituo cha Shaw mjini Ottawa, wametangaza mshikamano na uungaji mkono kwa wananchi wa Palestina hususan wa Ukanda wa Gaza, na pia wamelaani jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi hao madhulumu.

Huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina, waandamanaji hao wamesisitiza kuwa, Israel ni utawala wa kigaidi na watenda jinai za kivita wa utawala huo dhalimu wanapaswa kushtakiwa na kuadhibiwa katika vyombo vya sheria vya kimataifa.

Wamesema hatua ya Canada ya kulipiga kura azimio linataka kusitishwa mapigano mara moja huko Gaza kwa sababu za kibinadamu 'haitoshi' na kwamba Waziri Mkuu wa nchi hiyo anapaswa kuchukua hatua za maana za kusimamisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza. 

Canada ni katika nchi 153 zilizopiga kura jana Jumanne katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuunga mkono azimio la kusimamisha mapigano mara moja huko Gaza.

Utawala wa kigaidi unavyoua hata watoto wadogo Gaza

Trudeau, kama viongozi wengine wengi wa nchi za Magharibi, hivi karibuni aliwakasirisha Waislamu wa Canada na maeneo mengine ya dunia kwa kusema kuwa, Ottawa inaunga mkono haki ya Israeli ya kujilinda, wakati huu ambapo utawala huo ghasibu unaendelea kuua raia wasio na hatia wa Gaza.

Waziri Mkuu huyo wa Canada alitoa matamshi hayo huko Israel ikiwa tayari imeshaua makumi ya maelfu ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Baadhi ya duru zinasema, waliouawa shahidi Gaza katika hujuma hizo za Israel tokea Oktoba 7 ni watu 20,000.

Maandamano yanaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya dunia kupinga mauaji na mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya raia wa Palestina hususan katika Ukanda wa Gaza, na vilevile kulaani uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa jinai na uhalifu unaofanwa na utawala wa kibaguzi wa Israel.

Tags