May 25, 2023 06:15 UTC
  • New York Times: Ukraine ilihusika la shambulio dhidi ya Ikulu ya Kremlin

Gazeti la The New York Times limewanukuu maafisa wa Marekani wakisema kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba Waukraine ndio waliotekeleza shambulio lililofanywa na ndege zisizo na rubani (drone) kwenye Ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin) tarehe 3 mwezi huu wa Mei.

Maafisa hao wamesema kuwa vyombo vya ujasusi vya Marekani vilifikia tathmini ya awali kupitia mawasiliano yaliyonaswa, na kwamba huenda shambulio hilo lilipangwa na kitengo maalumu cha jeshi au cha ujasusi cha Ukraine.

Maafisa hao wa Marekani pia wameeleza kuwa haikubainika wazi iwapo Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky au maafisa wake wakuu walikuwa na habari kuhusu shambulizi hilo kabla ya kufanyika kwake.

Ni vyema kueleza kwamba Russia iliishutumu Marekani kwamba ilihusika kwa njia moja au nyingine na shambulizi hilo lililolenga Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, na kusisitiza kuwa inayo machaguo kadhaa kwa ajili ya kujibu hujuma hiyo.

Msemaji wa Ofisi ya Rais wa Russia aliituhumu Marekani kuwa ndiyo iliyopanga shambulio la ndege isiyo na rubani dhidi ya Kremlin.

Dmitry Peskov amesema kwamba, Marekani ambayo inaiainishia Ukraine maeneo ya kulenga shabaha, ndiyo iliyohusika na shambulio la ndege isiyo na rubani dhidi ya Kremlin na kuongeza kuwa: Juhudi za Washington na Kiev za kukana kuhusika na shambulio hilo ni za kipuuzi.

Rais Putin hakuwa katika Ikulu ya Kremlin wakati wa hujuma hiyo na iliripotiwa kwamba siku hiiyo alikuwa akifanya kazi katika makazi yake ya Novo Ogaryovo nje ya Moscow.

Baada ya hujuma hiyo, Dmitry Medvedev, Naibu wa Mkuu wa Baraza la Usalama la Russia ametoa wito wa kuuawa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

Dmitry Medvedev

Dmiry Medvedev aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba: Shambulio hilo ni la kigaidi na halikuibaikishia Moscow chaguo jingine isipokuwa kumuondoa katika uso wa dunia Zelensky na wenzake.