Jun 23, 2023 02:27 UTC
  • Chokochoko mpya zilizoanzishwa na Biden kuhusiana na China

Rais Joe Biden wa Marekani siku ya Jumanne wiki hii alimfananisha mwenzake wa China, Xi Jinping na madikteta.

Akizungumza katika harambee ya kuchangisha pesa kwa ajili ya kampeni zake za uchaguzi Kaskazini mwa California, Biden alisema hasira ya Xi Jinping ilichochewa na tukio la Februari; Tukio ambalo puto la China, ambalo Washington inadai lilitumika kwa ajili ya ujasusi, liliruka juu ya anga ya Marekani, lakini lilitunguliwa na ndege za kijeshi za nchi hiyo.

Joe Biden amesema: "Jambo lililomkasirisha sana Xi Jinping nilipolitungua puto hilo lililokuwa na vyumba viwili vilivyojaa vifaa vya kijasusi ni kwamba hakujua kuwa lilikuwa hapa. Ninamaanisha ninachosema. Ilikuwa aibu kubwa kwa madikteta wakati ambapo hawakujua kilichotokea."

China imejibu kwa hasira matamshi hayo yaliyotolewa na Rais wa Marekani, Joe Biden, ya kumfananisha Xi Jinping na madikteta. Wizara ya Mambo ya Nje ya China imeyataja matamshi ya Joe Biden kuwa ni ya kijinga na ya kutowajibika ya kisiasa, na kwamba yanakiuka hadhi ya kisiasa ya China.

Ni vyema kutambua kwamba, Russia, ikiwa ni mshirika wa karibu wa China, ambayo ina mtazamo na maslahi ya pamoja na Beijing katika kukabiliana na tawala za kibeberu za Magharibi zikiongozwa na Marekani, imechukua msimamo dhidi ya matamshi hayo ya kudhalilisha ya Biden kwa mwenzake wa China. Msemaji wa ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, amesema: "Hili ni dhihirisho jingine la kupingana kwa sera ya kigeni ya Marekani, ambayo kwa upande mmoja inaonyesha kutotabirika kwa Washington, na kwa upande mwingine, inaonyesha sera ya kigeni ya kiimla na mahubiri ambayo hayakubaliwi na nchi nyingi, na idadi ya nchi hizi inaongezeka."

Dmitry Peskov

Licha ya madai ya Marekani ya eti kujaribu kuboresha uhusiano na China na kupunguza mivutano katika uhusiano wake na Beijing, jambo ambalo lilidhihirishwa na ziara ya hivi majuzi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken, mjini Beijing na kukutana kwake na maafisa wakuu wa China, lakini matamshi mapya ya Biden yanaonyesha kuwa, Washington sio tu kwamba haijabadilisha msimamo wake wa chuki dhidi ya China, lakini pia imemkashifu na kumvunjia heshima Rais wa China kwa kutumia maneno ambayo yanakinzana na desturi za kisiasa na kaida za kidiplomasia. Matamshi hayo ya Joe Biden yametolewa huku wachambuzi wengi wakisisitiza kuwa, safari ya Blinken nchini China iliyolenga kupunguza mivutano kati ya Beijing na Washington haikuwa na mafanikio. Katika mazungumzo yake na Blinken, Rais Xi Jinping wa China alisisitiza kuwa Washington inapaswa kuiheshimu China, maslahi na haki zake za kisheria. Blinken pia alisema baada safari yake ya siku mbili mjini Beijing na mazungumzo yake maafisa wa China, akiwemo rais wa nchi hiyo, kwamba hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana katika kurejesha mawasiliano ya moja kwa moja ya kijeshi na serikali ya China.

Ziara ya Blinken mjini Beijing ilikuwa ya kwanza ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani nchini China katika kipindi cha miaka mitano iliyopita; na tangu hapo awali maafisa wa Marekani na wachambuzi wa mambo walitabiri kuwa haitafanikiwa katika kutatua hitilafu zilizopo kati ya nchi hizo mbili, na wala haitakuwa na matokeo chanya katika kuboresha uhusiano wao uliodorora. Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Qin Gang alisema katika mkutano wake na mwenzake wa Marekani, Anthony Blinken, kwamba uhusiano kati ya China na Marekani uko katika kiwango cha chini kabisa, jambo ambalo ni kinyume na maslahi ya nchi zote mbili. Pia amesisitiza kuwa "Taiwan ndio suala kuu katika uhusiano kati ya China na Marekani, na ni hatari kubwa zaidi katika uhusiano huo."

Kabla kidogo ya safari ya Blinken huko Beijing, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilitoa taarifa ikiionya Washington kuhusu kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Beijing ilitilia mkazo ulazima wa kukomesha njama za kudhoofisha mamlaka ya China, usalama na maendeleo yake zinazofanywa na Marekani kwa kisingizio cha ushindani, na kuongeza kuwa: Washington inaitambua Beijing kuwa mpinzani wake mkuu na changamoto muhimu zaidi ya jiografia ya kisiasa, na hilo ni kosa kubwa katika tathmini yake.

China na Marekani zinahitilafiana katika masuala mbalimbali, kuanzia biashara kati ya nchi hizo mbili hadi masuala ya utawala bora na hali ya haki za binadamu. Himaya na misaada ya kijeshi ya Marekani kwa Taiwan, ambayo China inaitambua kuwa ni sehemu ya ardhi yake, imeibua wasiwasi wa kuzuka makabiliano ya kijeshi kati ya Beijing na Washington juu ya kisiwa hicho. China inapinga vikali kuwepo kwa majeshi ya Marekani katika eneo hilo. Beijing pia inataka kuondolewa vikwazo na kukomeshwa vizuizi katika njia ya maendeleo ya kisayansi ya China. Sambamba na hayo Marekani imezidisha udhibiti wa mauzo ya bidhaa na teknolojia kwa China kutokana na kile ilichokiita ushirikiano wa taasisi na makampuni ya China na jeshi la nchi hiyo au ukiukaji wa haki za binadamu. 

Licha ya madai ya maafisa wa serikali ya Biden kuhusu kuwepo ushindani sawa na China na kukomesha mivutano katika uhusiano wa nchi mbili, pamoja na safari ya hivi majuzi ya Blinken huko Beijing, lakini kinachoonekana zaidi kupitia misimamo na hatua za Marekani dhidi ya China tangu Biden achukue madaraka ni juhudi za Washington za kukabiliana na Beijing katika nyanja zote za kiuchumi, kibiashara, kijeshi, kisiasa na kadhalika.

Tags