Jun 24, 2023 10:43 UTC
  • Russia yapinga kushiriki Macron katika mkutano wa BRICS

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov alitangaza Alhamisi iliyopita kwamba Moscow haidhani kuwa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ataruhusiwa kuhudhuria mkutano ujao wa kundi la BRICS nchini Afrika Kusini, kwa sababu Paris inatekeleza sera ya chuki dhidi ya Moscow.

Ryabkov amesema: Hapana shaka kuwa ni kazi ya mwenyeji wa mkutano wa BRICS kuainisha wageni watakaohudhuria mkutano huo na huu ni utaratibu uliowekwa, hata hivyo, ni bora kujadili suala hili na wanachama wengine.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa: Nchi ambazo zina sera ya uhasama na isiyokubalika dhidi ya Russia zinataka kuitenga Moscow katika medani ya kimataifa na ni sehemu ya shirika la kijeshi la nchi za Magharibi (NATO); na baya zaidi ni kwamba nchi hizo zinataka kushinda stratijia ya Russia na kuiondoa nchi hii katika kundi la mataifa makubwa, hivyo hazistahili kuhudhuria mkutano wa BRICS.

Sergei Ryabkov 

Msimamo huo wa Russia umetangazwa baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Catherine Colonna, kutangaza katika ziara yake mjini Pretoria, mji mkuu wa Afrika Kusini wiki hii, kwamba Macron angependa kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya Magharibi kuwa mgeni katika mkutano wa BRICS.

Mambo kadhaa yanaweza kutajwa kama sababu ya msisitizo wa Ufaransa wa kushiriki Macron katika mkutano wa kilele wa BRICS nchini Afrika Kusini. Kwanza ni kwamba, nchi za Magharibi ikiwemo Ufaransa, licha ya kupuuza, kudogesha na kuzibeza taasisi zinazoinukia kama vile BRICS, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), au Muungano wa Kiuchumi wa Eurasia, zinafahamu vyema umuhimu na hadhi ya jumuiya hizo katika medani ya kimataifa na vilevile mchango wa makundi na mashirika ya kikanda na kimataifa. BRICS inajumuisha nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, na hadi sasa imepokea maombi mengi kutoka nchi tofauti zinazotaka kujiunga na jumuiya hiyo. Miongoni mwa malengo ya BRICS ni kukomesha utawala wa sarafu ya dola ya Marekani na kutumia sarafu za nchi wanachama, suala ambalo limezua taharuki na wahka miongoni mwa nchi za Magharibi. 

Kwa msingi huo, wanasiasa kama Macron, ambaye siku zote amekuwa akichukua hatua za kiubunifu, tofauti na viongozi wengi wa Ulaya na Magharibi, badala ya kuangalia tu kwa macho shughuli zinazopanuka za taasisi kama BRICS, anapanga kushiriki kikamilifu katika mkutano wa BRICS ili pamoja na kufafanua maoni ya nchi za Magharibi haswa dhidi ya Russia, afanye juhudi za kuwa na taathira katika sera na maamuzi yake.

Emmanuel Macron

Sababu nyingine inayoweza kutajwa ya nia ya Macron kuhudhuria mkutano wa BRICS ni kwamba wanachama wengi wa kundi hili la kimataifa ni nchi zinazoinukia kiuchumi; hivyo amenuia kuzishawishi nchi hizo ziwe na sera zinazoipinga Russia. Katika muktadha huo, lengo la Paris ni kuibua mgawanyiko na tofauti kati ya wanachama wa BRICS; na kushiriki Macron katika mkutano wa kilele na kushauriana na wakuu wa nchi wanachama wake kunalenga kuzusha tofauti ili kuzidisha mashinikizo dhidi ya Russia. Kisingizio kinachotumiwa na Wamagharibi akiwemo, Rais wa Ufaransa, kwa ajili ya kuhalalisha sera hizo ni madai kuwa Russia ni mchokozi kutokana na mashambulizi yake dhidi ya Ukraine, na ulazima wa kuiadhibu Moscow. Hii ni licha ya kwamba, Macron akiwa mmoja wa viongozi wa nchi za Magharibi, anaelewa vyema sababu za operesheni maalumu ya kijeshi ya Russia dhidi ya Ukraine. Kabla ya kuanza operesheni hiyo Moscow ilionya mara kadhaa kuhusu jaribio la nchi za Magharibi kuiunganisha Ukraine na NATO na ililitangaza suala hilo kuwa ni mstari mwekundu wa usalama wa taifa lake. Hata hivyo Wamagharibi, sambamba na kuendeleza sera ya kupanua NATO upande wa Mashariki na kujaribu kuidhibiti na kuizingira Russia, wameendelea na sera hiyo hata kwa gharama ya kuanzisha vita vikubwa kati ya Russia na Ukraine, na wanatuma silaha na zana za kijeshi huko Ukraine na kudumisha vita hivyo vya umwagaji damu.

Rais wa Russia, Vladimir Putin hivi majuzi alitangaza kwamba washirika wa Magharibi wa Ukraine wameamua kupigana vita dhidi ya Russia hadi mwanajeshi wa mwisho wa Ukraine na hawajali lolote kuhusu majanga yanayoendelea kupawata Waukraine.

Vladimir Putin

Suala jingine ambalo linapaswa kuzingatiwa katika muktadha huu ni kwamba Wamagharibi hawaruhusu kushiriki maafisa wa ngazi za juu au Rais wa Russia katika majukwaa ya kimataifa au ya Magharibi katika fremu ya vikwazo vya pande zote dhidi ya Russia; lakini hivi sasa inaonekana kuwa Macron na kwa kutumia mtazamo ule ule wa nchi za Magharibi wa kujiona juu na bora kuliko nchi nyingine, anajipa haki ya kushiriki katika mkutano wa viongozi wa kundi BRICS nchini Afrika Kusini bila ya ridhaa ya Moscow, ambayo ni mmoja wa wanachama wakuu wa kundi hilo, ili kufikia malengo yake dhidi ya Russia.

Tags