Jun 30, 2023 03:26 UTC
  • Mataifa ya Kiislamu yalaani kuchomwa moto Qurani Tukufu Sweden

Ulimwengu wa Kiislamu umelaani vikali kitendo cha kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu (kitabu kitakatifu cha Waislamu) huko nchini Sweden.

Jumuiya ya Umma wa Kiislamu (Muslim World League) imetoa taarifa kali kulaani kudhalilishwa kwa maandishi matakatifu ya Kiislamu nchini Sweden na kusema kuwa, taswira na picha za kuchomwa moto Qurani Tukufu zinakusudia kuchochea na kuumiza hisia za Waislamu kote duniani, hasa kwa kuzingatia kuwa kitendo hicho kimefanyika katika sikukuu ya Iddul Adh'ha.

Sheikh Dakta Mohammed Abdulkarim Al-Issa, Katibu Mkuu wa jukwaa hilo lenye makao yake mjini Makka nchini Saudi Arabia amesema, kitendo hicho kimefanyika chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi wa Sweden, kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, katika hali ambayo kitendo hicho kiuhalisia kimekanyaga wazi uhuru huo.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amelaani jinai hiyo ya kuchoma moto nakala ya Qurani Tukufu nje ya Msikiti wa Jamia mjini Stockholm nchini Sweden na kuitaka serikali ya Sweden kuwachukulia hatua stahiki wahusika wa hujuma hiyo. 

Aidha Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri kimelaani kitendo hicho dhidi ya Qurani Tukufu, na kusema kitendo hicho kimefanywa na watu wenye mfungamano na mrengo wa kulia wa Sweden na kwamba serikali ya Uswidi ni mshirika katika uhalifu huo.

Nembo ya OIC

Al-Azhar imeitaka jumuiya ya kimataifa, mashirika ya kimataifa na viongozi wa dunia kusimama kukabiliana na matukio hayo ya kudhalilisha matakatifu ya kidini na kulaani vitendo hivyo vya uhalifu vinavyofanywa kwa jina la uhuru wa kujieleza.

Kadhalika mataifa mengi ya Waislamu kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq, Saudi Arabia, Kuwait, Pakistan, Jordan na Uturuki yametoa taarifa za kulaani kitendo hicho cha kishenzi cha kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden.

Wakati huohuo, Morocco imemuita nyumbani Balozi wake kutoka Sweden, kulalamikia jinai hiyo ya kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden. Aidha imemuita mwanadiplomasia mkuu wa Sweden mjini Rabat, na kumkabidhi malalamiko rasmi ya serikali ya Morocco juu ya upumbavu huo wa kudhalilishwa kitabu kitakatifu cha Waislamu.

Serikali ya Sweden ilitoa kibali kwa raia mmoja wa nchi hiyo kuchoma moto nakala ya Qurani Tukufu wakati wa sikukuu ya Idul Adh'ha na imetetea kitendo chake hicho cha kijinai.

Tags