Jul 06, 2023 02:18 UTC
  • Rais wa Azerbaijan: Ufaransa inaendeleza ukoloni mamboleo

Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan amesema Ufaransa ni moja ya nchi ambazo zinaendelea kung'angania na kutekeleza sera ya ukoloni mamboleo.

Rais wa Azerbaijan amesema hayo leo katika hotuba yake mbele ya mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) mjini Baku na kusisitiza kuwa, Rais Emmanuel Macron anapaswa kuziomba radhi nchi ambazo ziliathiriwa na ukoloni wa Ufaransa.

Amemhutubu Rais wa Ufaransa kwa kusema, "Waombe radhi mamilioni ya watu ambao watangulizi wako waliwakoloni, kuwafanya watumwa, kuwaua, kuwatesa na kuwadhalilisha."

Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan ameuambia mkutano wa NAM mjini Baku kuwa, endapo Macron ataomba radhi kwa niaba ya viongozi waliomtangulia, itaonyesha kuwa Ufaransa imekiri makosa yake ya kihistoria ya enzi za ukoloni.

Aliyev amesema yumkini hatua hiyo ya Macron kuyaomba radhi mataifa yaliyoathirika na ukoloni wa Ufaransa ikaisaidia nchi hiyo ya Ulaya kuondokana na mgogoro wa kisiasa na kijamii unaoikabili, hasa baada ya mauaji ya kikatili ya kijana aliyekuwa na asili ya Algeria.

Rais Aliyev amekutana na kufanya mazungumzo na Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Maandamano makubwa ya ghasia yanashuhudiwa nchini Ufaransa tokea Juni 27, baada ya kijana huyo aliyekuwa na miaka 17 kwa jina Nahel M kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika wilaya ya Au du Seine kusini mwa Paris. Maandamano hayo yameripotiwa kuenea hadi katika miji ya nchi mbili za Ubelgiji na Uswisi.

Rais Abdelmajid Tebboune wa Algeria amekuwa akisisitiza kuwa, wananchi wa Algeria hawatasahau jinai na uhalifu uliofanywa na Ufaransa nchini humo enzi za ukoloni. Zaidi ya Waalgeria milioni moja waliuliwa na wanajeshi wa Ufaransa katika kipindi cha vita vya kupigania ukombozi wa Algeria kuanzia mwaka 1954 hadi 1962.  

Tags