Jul 13, 2023 02:58 UTC
  • Marekani na Ulaya zapinga azimio la UN linalohusiana na kuchomwa moto Qur'ani

Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) limepitisha azimio kuhusu chuki na ubaguzi wa kidini kufuatia tukio la uchomaji moto wa Qur'ani nchini Sweden lililolaaniwa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Azimio hilo lilipitishwa jana Jumatano, lakini lilipingwa na Marekani na Umoja wa Ulaya, zilizodai kuwa linakinzana na misimamo yao kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.

Nchi 28 ziliunga mkono azimio hilo la UNHRC, 12 zilipinga na saba ziliamua kutopiga kura.

Pakistan na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, ambazo zilichukizwa na kitendo cha kishenzi kilichofanywa mwezi uliopita wa Juni na mhamiaji mmoja Muiraqi siku ya Idul-Adhha nje ya msikiti mkuu wa Stockholm, Sweden cha kuivunjia heshima Qur'ani kwa kuuchoma moto Msahafu sikukuu ya Eid al-Adha, zilifanikiwa kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Bilawal Bhutto Zardari aliuambia mkutano huo: "inatupasa tulione hili kwa wazi kama lilivyo: ni uchochezi wa chuki za kidini, ubaguzi na majaribio ya kuchochea machafuko".

Bilawal Bhutto Zardari 

 

Bhutto Zardari amebainisha kuwa vitendo kama hivyo vimefanywa kwa idhini rasmi ya serikali na kwa wahusika kuwa na uhakika kuwa hawatachukuliwa hatua.

Msimamo huo wa waziri wa mambo ya nje wa Pakistan ulitiliwa mkazo na kuungwa na mkono na mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Saudi Arabia na Indonesia.

Azimio la Baraza la Haki za Binadamu la UN limezitolea wito nchi wanachama zichukue hatua ya kuzuia kutokea na kuwachukulia hatua za kisheria wanaotetea uenezaji chuki za kidini.

Aidha, azimio hilo limetaka kadhia hiyo ije ijadiliwe tena katika vikao vya Baraza la Haki za Binadamu vitakavyofanyika mwezi Machi na Juni 2024…/

 

Tags