Jumatatu tarehe 9 Disemba 2024
https://parstoday.ir/sw/radio/event-i119930
Jumatatu tarehe 7 Jamadithani 1446 Hijria sawa na Disemba 9 mwaka 2024.
(last modified 2024-12-09T13:22:58+00:00 )
Dec 09, 2024 13:22 UTC
  • Jumatatu tarehe 9 Disemba 2024

Jumatatu tarehe 7 Jamadithani 1446 Hijria sawa na Disemba 9 mwaka 2024.

Miaka 921 iliyopita katika siku kama ya leo, arifu mkubwa wa Kiislamu Ainul Qudhaat Hamedani mwenye lakabu ya Abul Fadhl, aliuawa shahidi kwa kunyongwa huko Hamedam. Alikuwa fakihi, mwanafasihi, msomi na malenga mahiri.

Ainul Qudhaat alizaliwa mwaka 492 Hijria. Msomi huyo katu hakuwa akiogopa kubainisha itikadi yake. Ni kutokana na misimamo yake hiyo thabiti ambapo mwaka 525 Hijria alitiwa mbaroni na kufungwa huko Baghdad.

Baada ya muda alihamishiwa Hamedan na kunyongwa kando na shule yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Tamhiidat na Haqaiqul Qur’an.

Ainul Qudhaat Hamedani

Siku kama ya leo miaka 282 iliyopita Carl Wilhelm Scheele mwanakemia mashuhuri wa Sweden na mmoja kati ya waasisi wa elimu ya kemia ya leo alizaliwa huko Stockholm mji mkuu wa nchi hiyo.

Mwanakemia huyo aliendelea na masomo yake kutokana na jitihada na hamu yake kubwa aliyokuwanayo licha ya familia yake kuwa duni. Carl Wilhelm ambae aliishi katika zama za kuchanua kwa elimu ya kemikali, mwezi Oktoba mwaka 1772 alifanikiwa kugundua gesi ya chlorine baada ya juhudi za miaka mitano. Gesi hiyo ni moja kati ya mada muhimu za kemikali na inatumika sana viwandani. Mbali na hayo mwanakemia huyo aligundua pia manganese na Glicerine.   

Carl Wilhelm Scheele

Miaka 266 iliyopita katika siku kama hii ya leo vilianza vita vya miezi 13 vya Madras. Vita hivyo vinahesabiwa kuwa mojawapo ya vita vikali zaidi vya kikoloni kati ya Uingereza na Ufaransa huko India.

Vita hivyo vilianza baada ya Ufaransa kuishambulia bandari ya Madras huko kusini mwa India, ambayo ilikuwa ikidhibitiwa na Waingereza. Ufaransa ilipigana ikiwa na wanajeshi elfu tatu dhidi ya Uingereza iliyokuwa na wapiganaji elfu 22.

Mwezi Januari mwaka 1761, Ufaransa ilisalimu amri mbele ya Uingereza baada ya kikosi cha dhiba kushindwa kufika vitani.   

Miaka 63 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 9 Disemba mwaka 1961 ardhi ya Tanganyika ambayo hii leo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijikomboa na kupata uhuru.

Tanganyika ilianza kukoloniwa na Ujerumani mwaka 1880 hadi mwaka 1919 wakati ilipoanza kukoloniwa na Uingereza na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa mkoloni huyo hadi ilipopata uhuru na kujitawala katika siku kama ya leo. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na baadaye akachaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika.

Mwaka 1964 Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Siku kama hii ya leo miaka 38 iliyopita, yalianza mapambano yasiyo na kikomo ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza. Mapambano hayo ya ukombozi ambayo ni mashuhuri kwa jina la "Intifadha ya Kwanza" yalianzishwa baada ya kushadidi mauaji na ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina na pia kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na utawala huo ghasibu. Hayo yalijiri baada ya wananchi Waislamu wa Palestina kukatishwa tamaa na hatua zilizokuwa zikichukuliwa na nchi za Kiarabu na taasisi nyingi za Palestina kwa ajili ya kurejeshewa haki zao.