Jumatatu, 11 Agosti, 2025
Leo ni Jumatatu tarehe 17 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria mwafaka na 11 Agosti 2025.
Siku kama ya leo miaka 551 iliyopita, alizaliwa Muhammad Mustafa Imad, maarufu kwa jina la Abus-Su’ud, faqihi na mfasiri wa Kiislamu katika kijiji cha Mudares karibu na mji wa Istanbul huko Uturuki.
Baada ya kuhitimu masomo yake, Abus-Su’ud alijishughulisha na ufundishaji na kufanya kazi ya ukadhi mjini Istanbul, kazi aliyoendelea nayo hadi mwisho wa uhai wake. Abus-Su’ud alikuwa hodari katika masuala mbalimbali ya kijamii na aliweza kuandaa sheria za kiidara kwa mujibu wa dini ya Kiislamu katika utawala wa Othmania.
Mbali na kuzungumza lugha ya Kituruki, alizungumza pia lugha za Kifarsi na Kiarabu. Msomi huyo wa Kiislamu ametunga mashairi kadhaa kwa lugha hizo. Miongoni mwa vitabu vya Abus-Su’ud ni pamoja na ‘Irshadul-Aqlis-Saliim’ ‘Dua Nameh’ ‘Qanun Nameh’ na ‘Mafrudhaat'.

Tarehe 11 Agosti miaka 496 iliyopita Martin Luther alitangaza rasmi madhehebu ya Protestant.
Uprotestanti ulianzishwa na Martin Luther kama harakati ya kidini katika karne ya 16 kwenye ulimwengu wa Kikristo kwa lengo la kufanya mageuzi ya kidini. Harakati hiyo ilianza dhidi ya kanisa Katoliki na udikteta wa viongozi wa madhehebu hiyo kuhusu suala la msamaha wa dhambi unaotolewa na makasisi na Papa.
Martin Luther aliyekuwa Mjerumani alianza harakati hiyo ya uasi ndani ya kanisa Katoliki baada ya kufasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani tofauti kabisa na amri ya Papa kwa lengo la kuvunjilia mbali taasubu za kimadhehebu za Kikatoliki.

Katika siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, alizaliwa Sheikh Abdul Rahim Sultanul-Qurrai Tabrizi, qaari mkubwa wa Qur’ani Tukufu na mmoja wa walimu mashuhuri wa taaluma ya qiraa, huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran.
Baada ya kujifunza taaluma hiyo kutoka kwa baba yake, Sultanul-Qurrai Tabrizi alifahamiana na Sheikh Shamil Daghestani na kushirikiana naye. Wakati Sheikh Shamil Daghestani alipoandaa jeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi, Sultanul-Qurrai alifanya safari kuelekea Daghestani ili kushiriki katika harakati hiyo. Baadaye alirejea Tabriz na kuanzisha chuo cha kisomo cha Qur’ani na ni wakati huo ndipo alipopewa lakabu ya Sultanul-Qurrai.
Miongoni mwa athari zake ni pamoja na ‘Risala katika Elimu ya Tajwidi’. Sultanul-Qurrai alifariki dunia mwaka 1336 Hijiria mjini Tabriz.

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita Haile Selassie, aliyekuwa mfalme wa Ethiopia alitia saini azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililokuwa na lengo la kuiunganisha Eritrea na Ethiopia.
Ardhi ya Waislamu ya Eritrea ambayo hapo kabla ilikuwa ikikoloniwa na Italia, katika Vita vya Pili vya Dunia ilikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Mwezi Disemba 1950 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha Eritrea kuongozwa kwa mfumo wa shirikisho sambamba na kuunganishwa na Ethiopia.
Hata hivyo kutokana na kwamba wananchi wengi wa Eritrea hawakuridhishwa na hatua hiyo pamoja na kupuuzwa haki zao na utawala wa Ethiopia, walizidisha upinzani dhidi ya utawala wa Addis Ababa na hatimaye kuanzisha harakati ya kupigania uhuru wa nchi yao mnamo mwaka 1960.
Mwaka 1993 mapambano ya wananchi wa Eritrea yalizaa matunda ambapo walishiriki katika kura ya maoni na kupiga kura ya kujitenga na Ethiopia.

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita nchi ya Chad ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa na siku hii hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo.
Mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 wakoloni wa Ufaransa waliishambulia Chad na katika kipindi cha miaka mitatu wakaidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mwaka 1958 Ufaransa iliipa Chad hiari ya kujiongoza na miaka miwili baadaye na katika siku kama ya leo nchi hiyo ikapata uhuru kamili na kuchagua mfumo wa uongozi wa jamhuri.
Nchi ya Chad inapakana na nchi za Libya, Cameroon, Sudan, Afrika ya Kati, Nigeria na Niger.
