Jumamosi, 29 Julai, 2023
Leo ni Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Nne Muharram 1445 Hijria mwafaka na 29 Julai 2023 Miiladia.
Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita, yaani tarehe 11 Muharram mwaka 61 Hijiria, msafara wa mateka wa familia ya Bwana Mtume Muhammad (saw), baada ya tukio chungu la mauaji ya siku ya Ashura, ulianza safari ya kuelekea Sham, yalikokuwa makao makuu ya utawala wa dhalimu wa Yazidi bin Muawiya. Baada ya majeshi ya Yazidi yaliyokuwa yakiongozwa na Omar bin Sa’ad kumuua shahidi Imam Hussein (as) na masahaba wake, majeshi hayo ambayo hayakuwa na chembe ya ubinadamu moyoni, yalianza kupora vitu vya thamani vya msafara wa watu wa familia ya Mtume (saw). Askari hao sanjari na kuchoma moto mahema ya Imam Hussein (as) na watu wake, waliwanyang’anya pia wanawake mapambo yao na kila walichokuwa nacho. Jioni ya siku kama ya leo msafara wa familia ya Imam Hussein uliokuwa ukiongozwa na Imam Sajjad (as) na Bibi Zainab (as), ulielekea Kufa na baadaye Sham. ***

Katika siku kama ya leo miaka 140 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 29 Julai 1883, alizaliwa Benito Mussolini mwanasiasa, dikteta na mwasisi wa chama cha Kifashisti nchini Italia. Ufashisti ni utawala wa kidikteta uliojikita katika kuleta aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani na kupotosha itikadi na fikra za wananchi. Mwaka 1922 Mussolini alinyakua wadhifa wa uwaziri mkuu wa Italia, na hivyo udikteta kuendelea kutawala nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler na kuandaa mazingira ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia. ***

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 29 Julai 1957, Umoja wa Mataifa ulianzisha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA. Lengo la kuanzishwa taasisi hiyo ya kimataifa, ni kusimamia shughuli zote za mitambo ya nyuklia na kuhakikisha kwamba miradi ya nyuklia duniani inatekelezwa kwa njia za amani na kutotumika kwa malengo ya kijeshi na utengenezaji wa silaha za mauaji ya halaiki. ***

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita Abul Hassan Bani Sadr, rais aliyeuzuliwa wa Iran alikimbia nchi akiwa pamoja na kiongozi wa kundi la Munafiqin la MKO, Mas'ud Rajavi. Siku 37 kabla yake Bani Sadr alikuwa ameuzuliwa cheo cha rais kutokana na kukosa ustahiki, kuzusha machafuko nchini na kushindwa kulinda nchi mbele ya hujuma za utawala wa Saddam Hussein. Bani Sadr alikuwa na matumaini kwamba, mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na kundi la MKO yangeweza kumrejesha tena madarakani. Hata hivyo kuchaguliwa Muhammad Rajai kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu kulimvunja moyo Bani Sadr ambaye aliamua kukimbilia Ufaransa akiwa amevaa nguo za kike. ***
