Aug 06, 2023 11:34 UTC
  • Mchango wa Maulama wa Kishia Katika Uislamu (74)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kwa pamoja kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.

 

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 74 ya mfululizo huu kitaendelea kumzungumzia Seyyid Hassan Modarres, msomi na mwanaharakati mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu. Nataraji mtakuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.

Duru ya tatu ya Bunge la taifa la Iran ilianza sambamba na kukaribia kuanza Vita vya Kwanza vya Dunia. Licha ya kuwa Iran ilitangaza kutokuwa upande wowote katika vita hivyo, lakini moto wa vita hivyo uliwakumba pia wananchi wa Iran. Maulamaa wa Kiislamu walitangaza jihadi dhidi ya majeshi ya waitifaki sambamba na kutangaza kutetea utawala wa Othmania. Maulamaa wa Iran wakiungana na Maulamaa wa Najaf, waliwatolea mwito watu wa kukabiliana na wavamizi. Mwaka 1918 wakati vita vya kwanza dunia vilipofikia tamati baada ya kudumu kwa miaka minne, utawala wa Othmania nao ulisambaratika na kufikia tamati.

Muda mchache baadaye, Russia nayo ikatumbukia katika vita vya ndani na vikosi vya Russia vilivyokuwa nchini Iran vikakumbwa na hitilafu na mifarakano. Kidogo kidogo majeshi ya Russia yakaondoka nchini Iran, na Uingereza ikaona uwanja na mazingira sasa ni mwafaka kwake kwa ajili ya kupenya na kuwa na ushawishi nchini Iran. Ilikuwa ni katika mazingira haya ambapo Baraza la Taifa (Bunge) la Iran lilitangaza uwepo wake na wawakilishi wake akiwemo Sayyid Hassan Modarres wakaingia Bungeni kwa ajili ya duru ya nne ya Bunge hilo. Mfalme Ahmad Shah Qajar akamtaka Vossug ed Dowleh aunde serikali na Bunge la Nne likaipigia kura ya kuwa na imani nayo serikali yake.

Sayyid Hassan Modarres

 

Hata hivyo badala ya Vossug ed Dowleh kurekebisha na kuboresha hali ya mambo nchini aliingia katika mazungumzo na Uingereza na akatiliana saini na Uingereza mkataba ambao kwa mujibu wake, masuala yote ya kijeshi na kifedha ya Iran yakawa chini ya usimamizi na uangalizi wa Waingereza.

Mkataba huu ambao ulikuwa mashuhuri kama mkataba wa 1919, kivitendo uliifanya Iran kuwa koloni la Uingereza. Hassan Vossug ed Dowleh na mawaziri wake wengine wawili walisaini mkataba huo baada ya kuchukua rushwa ya tomani 400,000.  Viongozi hao waliandaa mazingira ya kutekelezwa mkataba huo hata kabla ya Bunge kuwa na taarifa ya kusainiwa kwake. Baada ya Bunge kupata taarifa ya kusainiwa mkataba huo, lilisimama na kuupinga vikali na Seyyid Hassan Modarres alikuwa kinara wa upinzani huo. Maulamaa wa Najaf nao baada ya kupata taarifa za mkataba huo nao walijitokeza na kuupinga na wananchi kwa upande waop pia, wakifuata msimamo wa Wabunge na Maulamaa waliukataa na kuupinga mkataba huo. Matokeo ya upinzani huo yakawa ni mfalme Ahmad Shah kuchukua hatua ya kumuuzulu Waziri Mkuu Vossug ed Dowleh na kuufutilia mbali mkataba huo.

 

Serikali ya Uingereza ambayo ilikuwa ikimuona Shah kwamba, hana nguvu na mamlaka ya kutosha ya kulishinda Bunge, na ilikuwa ikiliona Bunge na wawakilishi wake kuwa kizuizi chake cha kupanua satwa na ushawishi ilichukua uamuzi wa kuiunga mkono seri

Kamati ya Ulinzi wa Kitaifa

 

kali ambayo itakuwa kibaraka wake na ambayo itapunguza nguvu na mamlaka ya Bunge. Ikiwa na lengo la kufikia hilo,  iliingia katika mazungumzo na wanasiasa kadhaa wa Iran. Hata hivyo serikali ya Uingereza ikamuona Reza Khan Mirpanj aliyekuwa kamanda wa jeshi kuwa mtu anayefaa zaidi hasa kutokana na kuwa mtu anayependa madaraka.

Mpango wa Uingereza ulikuwa ni kubadilisha mfumo unaotawala na kuufanya kuwa wa jamhuri na baada ya muda umtangaze Reza Khan kama Rais wa maisha wa Iran na hivyo kuwatwisha wananchi wa Iran udikteta mwingine. Reza Khan alichukua  na kuupeleka Bungeni mpango wa kubadilisha mfumo wa katiba na kuufanya kuwa jamhuri. Hata hivyo Hassan Modares na marafiki zake walipinga vikali mpango huu. Walijua kuwa matokeo ya jamhuri inayoungwa mkono na ukoloni mkongwe wa Uingereza yasingekuwa chochote isipokuwa dhulma na ukandamizaji. Ni kuanzia hapo ambapo uadui kati ya Reza Khan na Seyyed Hassan Modares ulianza.

 

Waliotia saini mkataba wa 1919

 

Ufuatiliaji wa Modares na washirika wake ulisababisha bunge kutoidhinisha mpango wa Reza Khan, lakini mwaka mmoja baadaye, Uingereza iliunda na kutekeleza mapinduzi kwa msaada wa Reza Khan. Katika mapinduzi haya, Reza Khan aliiteka Tehran, akavunja serikali na bunge, akajiita waziri wa vita na kumpa jukumu Seyyed Ziauddin Tabatabai la kuunda baraza la mawaziri.

Moja ya hatua za kwanza za serikali ya Seyyed Ziauddin ilikuwa kukamatwa na kuhamishwa kwa wapinzani wa Reza Khan. Seyyed Hassan Modares, ambaye alikuwa mmoja wa wapinzani wa kwanza wa Reza Khan, alikamatwa na kupelekwa uhamishoni. Miaka minne baada ya mapinduzi ya Reza Khan, bunge la nne liliundwa upya na mara hii Hassan Modarres alikuwa naibu spika.Alianzisha chama cha mageuzi na kuwafukuza watu waliohusika katika mapinduzi ya 22 Februari 1921. Reza Khan, ambaye bado alikuwa akisimamia Wizara ya Vita, alitaka kuongeza wigo wa madaraka yake, na serikali haikuweza kukabiliana na tamaa na uchu wake, lakini bunge lilisimama kidete mbele yake.

Wakati Bunge la tano lilipofunguliwa, Modares na washirika wake walikuwa waliochache Bungeni kwani akthari ya Wabunge walikuwa wafuasi wa Reza Khan.

Reza Khan Mipanj

 

Wafuasi wa Reza Khan waliweka tena mpango wa kubadilisha mfumo na kuufanya jamhuri, lakini Modares na washirika wake bado walipinga vikali, hata Modares alijaribu kufanyike usaili dhidi ya Reza Khan mara tatu, lakini kwa sababu ya washirika wake kuwa wachache, alishindwa. Hata hivyo, upinzani na hotuba kali na zenye hoja nzuri za msomi huyo zilisababisha mpango wa Reza Khan kutopasishwa. Hatimaye, Reza Khan na marafiki zake hawakuona njia nyingine isipokuwa kumuondoa Modarres. Walimshambulia na kumjeruhi na alipokuwa hayupo bungeni, walipasisha mpango wa Reza Khan.

Miaka miwili baada ya tukio hili, yaani mwaka 1925 , bunge la tano liliuondoa madarakani ukoo Qajar na kumchagua Reza Khan kama Shah wa Iran. Katika Bunge la 6, Seyyed Hassan Modares bado alikuwa mwakilishi wa wananchi wa Tehran, lakini daima alikuwa chini ya uangalizi na ufuatiliaji wa makachero wa siri wa Reza Khan. Wapinzani wa Modarres walipoona sauti yake ya kupigania haki haizimiki walichukua uamuzi wa kumuua. Mnamo 1926, Modarres alinusurika kifo kwa mara ya tatu na mara hii njama hiyo ilifanyika kwa amri ya Reza Khan, ambaye sasa alikuwa mfalme. Mara hii pia njama hiyo ilifeli baada ya kujeruhiwa kwa risasi sehemu za mkononi na mabegani na akawa amenusurika kifo. Baada ya siku 64 alipona na kurejea tena bungeni. Hata baada ya majaribio kadhaa ya kuuawa, Modarres hakubadilika bali aliendelea na misimamo yake.

Sayyid Hassan Modarres akiwa hospitali baada ya jaribio la kutaka kumuua

 

Duru ya saba ya uchaguzi wa Bunge ilikuwa ya kimaonyesho kikamilifu kwani walioshinda viti vya Bunge  takribani wote walikuwa wafuasi wa Reza Khan. Hii ilidhihirisha kwamba, matokeo yalipangwa na kura zilichakachuliwa. Katika uchaguzi huu kulitokea kioja kwani Modarres hakupata hata kura moja. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana alihoji: Hata kama watu laki mbili walionipigia kura uchaguzi uliopita watakuwa wote wamekufa, au wako hai lakini hawajanipigia kura mimi, basi hata kura moja niliyojipigia mimi iko wapi?

Wapenzi wasikilizaji. Kwa leo nakomea hapa kwani muda umenipa mkono tukutane tena wiki ijayo.