Aug 07, 2023 13:36 UTC
  • Sura ya Adh-dhaariyaat, aya ya 24-37 (Darsa ya 956)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 956 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 51 ya Adh-Dhaariyaat. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya ya 24 hadi ya 30 ya sura hiyo ambazo zinasema:

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ

Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao hishimiwa?

إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا ۖ قَالَ سَلَامٌ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ

Walipo ingia kwake wakasema: Amani (juu yako)! Na yeye akasema: Amani (juu yenu)! Nyinyi ni watu nisio kujueni.

 فَرَاغَ إِلَىٰ أَهْلِهِ فَجَاءَ بِعِجْلٍ سَمِينٍ

Akaenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliye nona.

فَقَرَّبَهُ إِلَيْهِمْ قَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ

Akawakaribisha, akasema: Mbona hamuli?

فَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً ۖ قَالُوا لَا تَخَفْ ۖ وَبَشَّرُوهُ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ

Akahisi kuwaogopa (katika nafsi yake). Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu.

فَأَقْبَلَتِ امْرَأَتُهُ فِي صَرَّةٍ فَصَكَّتْ وَجْهَهَا وَقَالَتْ عَجُوزٌ عَقِيمٌ

Ndipo mkewe akawaelekea na ukelele huku akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Kikongwe tasa!

قَالُوا كَذَٰلِكِ قَالَ رَبُّكِ ۖ إِنَّهُ هُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ

Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima, Ajuaye (kila kitu).

Katika majimui ya aya hizi saba tulizosoma kimezungumziwa kisa cha malaika waliomteremkia Nabii Ibrahim AS, ambao walimuendea Mtume huyo mteule wakiwa katika umbo la binadamu pasi na kujulikana na mtu yeyote. Malaika hao walitumwa kwenda kumpa habari mbili muhimu Nabii Ibrahim AS: Ya kwanza ni bishara ya kupata mtoto akiwa katika umri wa uzee; na ya pili ni kuteremshwa adhabu kwa watu waovu na mafasiki wa kaumu ya Nabii Lut’ AS. Aya hizi, kwanza zinasimulia jinsi malaika hao walivyoingia nyumbani kwa Nabii Ibrahim na kueleza kwamba: japokuwa Ibrahim AS hakuwatambua kuwa ni malaika, lakini aliwapokea na kuwakirimu kwa msingi wa kumfanyia takrima mgeni. Kwa mintaarafu hiyo aliwaandalia dhifa wageni wake hao asiowajua kwa kuwachinjia ndama aliyenona na kuwatengezea nyama ya kuoka. Lakini alipoona hawali chochote aliingiwa na wasiwasi kwamba, isije ikawa watu wale asiowajua, wana nia mbaya; kwa sababu ilikuwa desturi hapo kale, kama mtu atakula chakula alichoandaliwa na mtu mwingine, humaanisha kwamba hatamdhuru au kumfanyia ubaya wowote aliyemwandalia chakula hicho. Na ndio maana Nabii Ibrahim AS aliwauliza wageni wale sababu ya kutokula chakula alichowatayarishia. Na hapo ndipo wao walijitambulisha kuwa ni malaika wa Mwenyezi Mungu, ambao kama walivyo malaika wengine hawali kitu. Tunaweza tukajiuliza, kulikuwa na hekima gani ya malaika wale kutojitambulisha kwa Nabii Ibrahim tokea mwanzo, ili Nabii huyo asitaabike na kugharimika kwa ajili ya kuwakirimu wao kwa chakula? Huenda, huo pia ulikuwa mtihani wa kupima kiwango cha ukarimu na urahimu wa Ibrahim AS. Pamoja na hayo, usumbufu aliopata Nabii Ibrahim haukupita bila malipo, kwani malaika wale walimpa bishara Mtume huyo kwamba, Mwenyezi Mungu aliye muweza wa kila kitu, karibuni hivi atamruzuku mwana wa kiume ambaye atakuwa miongoni mwa wajuzi na wenye elimu kubwa wa zama zake. Wakati huo, Nabii Ibrahim na mkewe Sara, wote wawili walikuwa wazee na wagumba. Kwa hivyo wakati Bi Sara aliposikia bishara hiyo alionyesha hisia kubwa za mshangao na akasema, itawezekanaje kupata mtoto, mimi ambaye nimeshazeeka na hakuna uwezekano wowote wa mimi kuzaa? Inavyoonyesha, alikuwa ameghafilika kwamba ulimwengu huu unatawaliwa na irada ya Allah na lile alitakalo Yeye Mola liwe, basi litakuwa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kumuenzi na kumkirimu mgeni ndio sira na mwenendo wa Mitume wa Mwenyezi Mungu, hata kama mgeni huyo atakuwa ni mtu tusiyemjua na asiyeonyesha urafiki na uchangamfu kwa mwenyeji wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, maamkizi ya kumtakia mtu amani ni adabu ya mbinguni, kwani hata malaika pia huanza kuzungumza kwa maamkizi hayo ya Salamun Alaykum. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, tumfanyie ihsani na wema mkubwa mgeni tunayemkirimu, wala tusitosheke na kumfanyia jambo dogo na hafifu tu. Vilevile aya zinatuelimisha kuwa, Mitume walikuwa binadamu; na kwa hivyo wakati mwingine – kama walivyo watu wote – wao pia walikuwa wakipatwa na hali fulani ya hofu na wasiwasi juu ya mambo. Halikadhalika tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba, qudra na uwezo wa Allah hauna mpaka wala kikomo; na uko juu ya sababu zote za kimaumbile. Na ndivyo kama tulivyoona, jinsi mume na mke wazee na wagumba walivyojaaliwa kupata mtoto mjuzi na alimu mkubwa. Kwa hivyo haifai hata kidogo kukata tamaa ya kupata rehma na fadhila za Mwenyezi Mungu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 31 hadi 37 ya Sura yetu ya Adh-Dhaariyaat ambazo zinasema:

قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ

AKASEMA: Basi makusudio yenu ni nini, enyi mlio tumwa?

 قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ

Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu waovu,

لِنُرْسِلَ عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن طِينٍ

Ili tuwatupie mawe ya udongo,

مُّسَوَّمَةً عِندَ رَبِّكَ لِلْمُسْرِفِينَ

Yaliyo tiwa alama kwa Mola wako Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka.

فَأَخْرَجْنَا مَن كَانَ فِيهَا مِنَ الْمُؤْمِنِينَ

Basi tuliwatoa katika hao wale walio amini. 

فَمَا وَجَدْنَا فِيهَا غَيْرَ بَيْتٍ مِّنَ الْمُسْلِمِينَ

Lakini hatukupata humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu! 

وَتَرَكْنَا فِيهَا آيَةً لِّلَّذِينَ يَخَافُونَ الْعَذَابَ الْأَلِيمَ

Na tukaacha humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu iumizayo.

Baada ya malaika kumpa Nabii Ibrahim bishara ya kuruzukiwa mtoto, walimueleza pia kwamba kazi hasa waliyotumwa kuifanya ni kwenda kuiangamiza kaumu ya Nabii Lut’ AS; kaumu ya watu waliokuwa wameghariki kwenye lindi la uchafu wa liwat’i na hawakuwa wakiyaona wanayoyafanya kama ni madhambi na maasi. Watu hao walikuwa hawayajali hata kidogo maonyo na indhari alizokuwa akiwapa Mtume wao Lut’ AS. Nabii Lut’alikuwa ametumwa na Nabii Ibrahim kwenda kuwafikishia wito wa uongofu watu mafasiki na waliopotoka wa kaumu hiyo. Kwa sababu hiyo, malaika walimwendea kwanza Nabii Ibrahim AS ili kumpa taarifa kuhusu adhabu itakayowashukia watu hao na kumhakikishia kwamba Nabii Lut’ na waja wema na waumini ambao wamejiepusha na uchafu huo, wao haitawapata adhabu hiyo. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, adhabu kwa watu waovu haihusiani na Kiyama tu. Baadhi ya kaumu na watu wanaadhibiwa na kuangamizwa papa hapa duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, japokuwa jamii iliyofisidika na kuharibika inachangia kumtumbukiza mtu kwenye maovu, lakini pamoja na hayo inawezekana kuishi kiusafi na kimaadili katika jamii chafu na iliyopotoka. Kwa hiyo mtu asijitetee na kuyapa uhalali madhambi anayofanya kwa kisingizio cha mazingira mabaya na maovu yaliyomzunguka. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, katika mfumo wa haki na uadilifu wa Allah, ikiwa akthari ya watu katika jamii watakuwa waovu na watenda madhambi, adhabu wanayoteremshiwa waovu hao haiwahusishi waja wema wasio na hatia. Allah huwanusuru waja wake hao na adhabu hiyo. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa, athari za kale zilizoachwa na kaumu zilizopita za watu waovu na madhalimu ni somo la kutoa ibra na mazingatio kwa watu wa baada yao kwamba wajihadhari na kumwasi Allah SWT. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 956 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na madhambi yanayostahikisha adhabu ya duniani na atunusuru na maangamizi, pale anapowaonjesha adhabu wanaoasi amri zake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

 

 

Tags