Aug 07, 2023 14:21 UTC
  • Sura ya Adh-dhaariyaat, aya ya 54-60 (Darsa ya 959)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 959 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 51 ya Adh-Dhaariyaat. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 54 na 55 ambazo zinasema:

فَتَوَلَّ عَنْهُمْ فَمَا أَنتَ بِمَلُومٍ

Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi.

وَذَكِّرْ فَإِنَّ الذِّكْرَىٰ تَنفَعُ الْمُؤْمِنِينَ

Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini.

Katika darsa iliyopita tulisema, katika zama zote za historia wapinzani wa harakati ya Utume walikuwa wakiwatuhumu Manabii wa Allah kwamba ni watu wachawi na wafanyamazingaombwe au wanawasiliana na majini. Walikuwa wakifanya hivyo ili kuitoa thamani miujiza na makarama ya waja hao wateule pamoja na kukanusha mawasiliano baina yao na Allah SWT. Aya hizi tulizosoma zinamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW kwa kumwambia: wewe umetekeleza vyema na ipasavyo wajibu wako wa kuwafikishia uongofu watu hao, kwa hivyo huna lawama. Kwa mlipofikia, waache kama walivyo, kwani hakuna matumaini ya wao kuongoka; na sababu ni kwamba wao si watu wanaotaka kuujua ukweli na kuukubali. Pamoja na hayo, kutoa maonyo na kuwakumbusha watu wote kwa ujumla ni miongoni mwa majukumu makuu ya Mitume; na watu wenye nia ya kweli ya kuijua haki hunufaika na mawaidha na indhari za kuelimisha zinazotolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kuitambua njia sahihi ya uongofu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, jukumu la Mitume ni kufanya tablighi ya kueneza ujumbe wa Allah kwa watu wote, lakini suala la tija na matunda yatakayopatikana, hilo haliko kwenye mamlaka yao. Wao hawana dhima wala masuulia yoyote kwa watu ambao hawako tayari kuamini na kuifuata haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tusitarajie kwamba watu wote wataiamini haki; kwa hivyo tutumie zaidi uwezo na suhula zetu kwa ajili ya watu ambao tuna matumaini nao ya kuiamini na kuifuata haki. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kuwa tayari kupokea nasaha na mawaidha ni katika sifa za waumini; kwa hivyo mtu asiye na moyo wa kupokea ukumbushaji na kuufanyia kazi basi awe na shaka juu ya ukweli wa imani yake.

Ifuatayo sasa ni aya ya 56 hadi 58 za sura yetu ya Adh-Dhaariyaat ambazo zinasema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

Na sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.

مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ

Sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe.

إِنَّ اللَّهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti.

Aya zilizotangulia zimezungumzia ukumbushaji na kutoa maonyo, ambako kuna faida kwa walioamini. Aya hizi tulizosoma zinasema: moja ya masuala muhimu zaidi ambayo mwanadamu inapasa ayatafakari na kuyazingatia kila wakati ni lengo la kuumbwa kwake; na kughafilika na hilo humfanya aishie kwenye mkanganyo na upotofu. Ni wazi kwamba kuumbwa kwa mwanadamu kulifanywa kwa lengo maalumu, lakini Yeye Allah SWT hakuwa anahitaji chochote kwa ajili ya kumuumba kiumbe huyo. Kwa hakika lengo la kuumbwa mwanadamu ni kiumbe huyo kufikia utukukaji na ukamilifu wa kiutu. Aya hizi tulizosoma zinamuonyesha mwanadamu njia ya ukamilifu wa kiutu na kubainisha kuwa, kuabudu na kudhihirisha uja halisi kwa Allah ndio njia ya kuufikia ukamilifu huo. Ibada tab'an ina pande mbili: Mmoja ni wa maana yake makhsusi inayohusu ufanyaji amali mbalimbali za kiibada kama Sala, Funga, Hija n.k; na nyingine ni maana yake pana na ya ujumla inayojumuisha pande zote za maisha ya mtu. Hii inamaanisha kwamba, katika machaguo na maamuzi yake yote anayochukua maishani, mwanadamu anatakiwa afanye hivyo kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kujiweka mbali na kila linalomghadhibisha Yeye Mola. Ni wazi kwamba, ikiwa mtu atamweka mbele Allah katika hali zote za maisha yake atazidi kujipambanua na ghariza za kinyama na matashi duni na yasiyo na thamani ya kidunia na kuukaribia zaidi na zaidi ukamilifu mutlaki ambao kwa hakika ni Yeye Mola aliyetukuka Muumba wa ulimwengu. Kuwa karibu huko na Mwenyezi Mungu Jalla Fii U'laahu ndiyo daraja ya juu kabisa ya ukamilifu ambao mwanadamu anaweza kuifikia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, majini na wanadamu wana hali sawa katika lengo la kuumbwa kwao na katika kulifikia lengo hilo ambalo ni kudhihirisha uja wao halisi kwa Muumba wao Allah SWT. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hapana shaka kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu si mhitaji wa ibada za waja wake, bali ni kinyume chake, yaani sisi wanadamu tunatukuka kwa kudhihirisha uja wetu kwake Yeye na kufikia ukamilifu wa kimaanawi. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, ni wajibu wa mtu kujituma na kufanya juhudi za kutafuta riziki, lakini wakati huohuo tusighafilike na ukweli kwamba asili na chanzo cha riziki zetu ni Allah TWT.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 59 na 60 ambazo zinasema:

فَإِنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا ذَنُوبًا مِّثْلَ ذَنُوبِ أَصْحَابِهِمْ فَلَا يَسْتَعْجِلُونِ

Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasiniharakishe.

فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِن يَوْمِهِمُ الَّذِي يُوعَدُونَ

Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa.

Aya hizi ambazo ndizo aya za mwisho za Suratu-Dhaariyaat zimefanya majumuisho ya muhtawa na yaliyozungumziwa ndani ya sura hii na kusema: kaumu mbalimbali ambazo habari zao zimesimuliwa kwa muhtasari katika sura hii, kwa masikitiko zilisimama kupinga na kukanusha wito wa Mitume ya Mwenyezi Mungu. Watu hao walishukiwa na adhabu ya Allah hapa duniani na huko akhera pia adhabu ya Moto inawangojea. Wapinzani wa Mitume walikuwa kila mara wakiwauliza Manabii hao wa Allah, hicho Kiyama kitathibiti lini? Na kwa kuzingatia kwamba Mitume wenyewe hawakuwa wakiujua wakati hasa wa kujiri Kiyama na kufufuliwa viumbe, wapinzani hao wakakitumia kisingizio hicho ili kutilia shaka na kukadhibisha asili yenyewe ya kutokea tukio hilo adhimu. Kwa hivyo Qur'ani inasema, msiharakishe; lakini kuweni na uhakika kwamba Mwenyezi Mungu hakhalifu wala haendi kinyume na ahadi yake. Siku hiyo itafika; siku ambayo itakuwa ngumu na nzito kwenu nyinyi na hamtapata njia yoyote ya kurudi mlikotoka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kama mtu ataghafilika na lengo la kuumbwa kwake ambalo ni kudhihirisha uja wake kwa Allah SWT, na badala yake akaacha kufuata njia inayoendana na lengo hilo, atakuwa ametenda dhulma kubwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, huruma na ghadhabu za Mwenyezi Mungu Mtukufu zinaendana na ujuzi na hekima yake; kwa hivyo haraka na papara yetu sisi ya kutaka ufike muda wa kujiri tukio fulani haziwi na athari yoyote katika kujiri kwa jambo hilo. Wa aidha aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba, hatima na majaaliwa ya mtu yanategemea amali na matendo yake. Kwa hivyo ukafiri na dhulma havina hatima na mwisho mwengine isipokuwa kufikwa na adhabu ya Allah hapa duniani na huko akhera. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 959 ya Qur'ani imefikia tamati na ndiyo inayotuhitimishia tarjumi na maelezo kwa ufupi ya sura ya 51 ya Adh-Dhaariyaat. Inshallah tuwe tumeaidhika na kunufaika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba Allah aturuzuku riziki na chumo la halali na lenye baraka na atuwezeshe kuwa waja wake halisi tunaomwabudu na kumtii Yeye peke yake katika kila kitu cha maisha yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags