Aug 29, 2023 09:24 UTC
  • Iran ni moja ya nchi tano zinazozalisha maji mazito ya nyuklia duniani

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Maji mazito ni bidhaa ya pili ya kimkakati ya sekta ya nishati ya nyuklia baada ya uranium duniani na Iran ni moja ya nchi tano zinazozalisha bidhaa hii kwa usafi wa hali ya juu kiasi kwamba nchi nyingi zinatazamia kununua maji mazito ya Iran licha ya uwepo wa vikwazo.

Chini ya makubaliano ya nyuklia ya 2015, Iran inaruhusiwa kutumia maji mazito katika kinu chake cha nyuklia cha Arak kilichorekebishwa, lakini ikizalisha maji mazito ya ziada na pia ikirutubisha urani zaidi ya mahitaji yake lazima iuze bidhaa hizo katika soko la kimataifa.

Makubaliano yanasisitiza kwamba maji mazito yasizidi tani 130, lakini kujiondoa kwa Marekani kutoka kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei 2018 kumeiruhusu Iran kuongeza uzalishaji na kuwa na akiba ya bidhaa hizo mbili.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran Mohammad Eslami aliwaambia waandishi wa habari wakati wa ziara yake ya hivi karibuni kwenye Kiwanda cha Uzalishaji Maji Mazito huko Khondab karibu na Arak kwamba maji mazito ya Iran yana wateja wengi. Alisema Iran kwa sasa inawekeza kwenye maji mazito.

Eslami aliongeza kuwa, "wateja wetu wamegundua ubora wa juu na usafi wa maji mazito ya Iran."

Marekani ilikuwa imejitolea kununua tani 32 za maji mazito ya Iran kwa ajili ya matumizi ya vinu vyake vya nyuklia, lakini ilisitisha ununuzi huo baada ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kuachana na makubalianonyuklia ya JCPOA na kutangaza vikwazo dhidi ya Iran.

Baada ya miaka mingi ya jitihada, tasnia ya nyuklia ya Iran sasa imeimarika kwa kiwango cha juu. Iran imestahamili ukaguzi mkubwa zaidi wa kimataifa uliowahi kutokea ulimwenguni ambao uliweka breki kwenye kasi ya maendeleo yake ya nyuklia, lakini pamoja na vizingitii hivyo sekta ya nyuklia ya Iran imeendelea kupiga hatua.

Hivi sasa mafanikio ya kiuchumi ya sekta ya nyuklia yanaanza kudhihirika.

Kulingana na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, tasnia ya nyuklia ni moja ya tasnia zenye thamani ya juu zaidi ulimwenguni.

"Tulikuwa tumepuuza jambo hili muhimu, lakini tunataka kuzingatia uchumi wa nyuklia kwa njia maalum," alisema.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei alitoa wito kwa viongozi wa nchi mwezi Juni kuchukua hatua zinazohitajika ili kufanyia biashara bidhaa na huduma za nyuklia.

"Bidhaa na huduma za nyuklia za Iran lazima ziwe za kibiashara. Kuna mahitaji mazuri ya mafanikio yetu katika masoko ya kimataifa ambayo yanaweza kutumika kusaidia uchumi wetu na mapato. Tunapaswa kuwa na ushirikiano na nchi washirika," alisema.

Tangu mwaka 2021, Iran imesajili mafanikio 159 ya kisayansi katika sekta ya nyuklia ikiwa ni pamoja na nyanja za nishati ya nyuklia, leza, plasma, mionzi, mazingira pamoja na maji na udongo.

Eslami amesema katika mwaka mmoja na nusu uliopita, uwezo wa Iran wa kurutubisha uranium umeongezeka hadi kufikia miaka 11. Anasema alipoingia ofisini zaidi y amwaka mmoja uliopita, ni migodi miwili tu ya urani iliyokuwa ikifanya kazi, lakini idadi hiyo imefikia minane na itapindukia 20 mwaka ujao.

Shirika la Anga za Juu la Iran (ISA) limetangaza kuzindua mchakato wa uzalishaji wa "Pars-3," satelaiti "ya kisasa zaidi na yenye usahihi wa juu"

Hassan Salarieh, mkuu wa shirika hilo,  amenukuliwa na tovuti ya Tasnim akisema," Hapo awali, tulitoa ahadi kadhaa kuhusu utengenezaji wa satelaiti za uchunguzi kutoka mbali zenye usahihi wa hali ya juu."

Ameongeza kuwa: "Leo, ninatangaza kwa fahari kwamba Shirika la Anga za Juu la Iran limechukua hatua muhimu sana katika kubuni na kutengeneza satelaiti za kufanya uchunguzi kwa usahihi mzuri sana."

Alizitaja "Pars-2" na "Pars-3" kama satelaiti mbili kama hizo, ambazo taratibu zake za uzalishaji "zimeanza rasmi."

Salarieh amedokeza kuwa "Pars-2" na "Pars-3" ni satelaiti zenye usahihi wa upigaji picha wa mita nne na mbili.

Iran hivi sasa ni miongoni mwa nchi 10 duniani zenye uwezo mkubwa katika anga za juu, mafanikio ambayo yamepatikana kutokana na juhudi za zaidi ya miongo 4 za wataalamu wa humu nchini, na kwa hivyo Iran ina nafasi muhimu katika sekta hii kati ya nchi chache zilizo na teknolojia hiyo. Hivi sasa, ujenzi wa vituo vya kurushia satelaiti uko mikononi mwa nchi 6 tu, na Iran iko kwenye nafasi inayofuata katika uwanja huo wa kustawisha vituo vya anga za mbali.

Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza kabisa inayojulikana kwa jina la Omid (yaani Tumaini) mwaka 2009.

Iran pia imetangaza kuwa, katika kipindi cha miaka michache ijayo itatuma mwanaadamu katika anga za mbali. Tayari mazoezi yameshafanyika kuhusiana na lengo hilo kwa kutumwa nyani hai katika anga za mbali ambaye alirejea ardhini akiwa salama.

Balozi wa Kenya mjini Tehran ametembelea viwanda vya uzalishaji katika mji wa Arak, makao makuu ya mkoa wa Markazi, unaofahamika kama mji mkuu wa viwanda wa Iran.

Joshua Gatimu, Balozi wa Kenya nchini Iran alizitembelea kampuni hizo za uzalishaji yakiwemo mashirika ya kuzalisha dawa jijini Arak hivi karibuni.

Katika mahojiano na Radio Tehran pambizoni mwa ziara yake hiyo mjini Arak katikati ya Iran, Balozi Gatimu ameashiria safari ya hivi karibuni ya Rais Ebrahim Raisi wa Iran nchini Kenya na kusema kuwa, anatumai ziara hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa nchi mbili.

Amesema, "Kwa bahati nzuri, safari ya Rais wa Iran nchini Kenya ilikuwa na mafanikio, na natumai yatakuwa na matokeo chanya. Nipo tayari kufuatilia makubaliano yaliyofikiwa na nchi mbili hizi katika safari hiyo."

Mwanadiplomasia huyo wa Kenya amebainisha kuwa, wajumbe wa Kenya karibuni hivi wataitembelea Iran kuzungumza na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu, na kufuatilia utekelezaji wa mapatano yaliyosainiwa katika safari ya Rais Raisi mjini Nairobi.