Feb 15, 2024 08:30 UTC
  • Iran yarusha satalaiti tatu kwa mpigo katika anga za mbali

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kutuma angani satalaiti tatu kwa mpigo zilizotengenezwa na wataalamu wa hapa nchini.

Satalaiti hizo za Mahda, Keyhan-2, na Hatef-1 zimetumwa angani mapema 28 Januari  kwa kutumia roketi la  kubeba satalaiti la Simorgh.

Satalaiti hizo za utafiti zilizotengenezwa na Kituo cha Utafiti wa Anga za Juu cha Iran zimewekwa kwa mafanikio katika mzingo uliokusudiwa, umbali wa kilomita baina ya 450 na 1,100 juu ya uso wa dunia.

Haya yalijiri siku chache baada ya satalaiti ya Thuraya ambayo imebuniwa na kutengenezwa kwa juhudi na hima ya wasomi vijana wa Iran na kurushwa katika anga za juu, kufanikiwa kutuma taarifa zake za awali na kuthibitisha kuwa imetua sehemu iliyokusudiwa kwa mafanikio makubwa. Soraya au Thurayya ilifika mzunguko wa kilomita 750 kutoka ardhini kwa kutumia roketi ya "Qaim 100".

Nafasi ya Iran katika sekta ya utaalamu wa anga za mbali imeimarika sana kwenye miaka ya hivi karibuni. Iran imeweza kubuni na kutengeneza satalaiti za kila namna za kielimu, kiutafiti, kijiografia na kijeshi. Mafanikio hayo yote yamepatikana pamoja na kuwa nchi hii imewekewa vikwazo na madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.

adola hayo ya kibeberu ya Ulaya hasa yanapinga hatua ya Iran kujiundia maroketi ya kubeba satalaiti yenye uwezo wa kufika eneo la anga za mbali linalojulikana kama obiti ya geosynchronous na kusema uwezo huo unaiwezesha Iran  kuunda makombora ya kisasa ya balestiki ya kutoka bara moja kwenda jingine (ICBM). Hii ni katika hali ambayo lengo la Iran la kumiliki teknolojia hiyo ni kutengeneza satalaiti zenye uwezo wa kufikia obiti ya geosynchronous.

Mzingo wa geosynchronous ni obiti ndefu inayozunguka  sayari ya dunia ambayo huruhusu satalaiti kuzunguka sayari hii. Hili ni eneo ambalo liko kwenye mwinuko wa takribani kilomita  35,800  juu ya ikweta ya sayari ya dunia. Obiti hii inatumika katika satalaiti za mawasiliano ya simu, na satalaiti zote za mawasiliano na televisheni huwa katika eneo hilo.

Sekta ya anga za mbali inazingatiwa kuwa kati ya tasnia yenye teknolojia ya hali ya juu. Licha ya mapungufu yote  yanayotokana na vikwazo vya madola hasimu ya Magharibi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kumiliki mzunguko kamili wa teknolojia ya anga ya juu. Hii ina maana kuwa, mbali na kuwa na uwezo na kuunda na kurusha satalaiti angani, Iran pia ina kituo cha ardhini cha kupokea data zinazotumwa na satalaiti.

Hivi sasa Iran ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza duniani katika sekta ya anga za mbali na mafanikio hayo ni matokeo ya zaidi ya miongo 4 ya jitihada za wataalamu wa nchi hii ya Kiislamu.

Ijapokuwa maadui wamejaribu kutumia kila mbinu kuzuia maendeleo ya kiuchumi na kisayansi ikiwemo sekta ya anga ya juu ya Iran lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kupata teknolojia mbalimbali za anga na anga za mbali.

Kwa kutilia maanani nafasi muhimu ya satalaiti katika zama za sasa katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu zikiwemo sekta za mawasiliano, utafiti, upelelezi na matumizi mengine mengi ya kimazingira, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina azma kubwa ya kuendeleza miundombinu na teknolojia yake ya makombora na anga za juu, na maendeleo makubwa yamepatikana katika mwelekeo huu.

@@@

RAIS William Ruto wa Kenya hivi karibuni amewambia vijana nchini humo kuchangamkia mpango wake wa kukita vitovu vya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA) ili kujikomboa kutoka kwa lindi la kukosa kazi.

Akizungumza ziarani Kaunti ya Bungoma , Rais wa Kenya ambaye hutumia kila fursa kutangaza mpango wa kubunia vijana mbinu za ajira, alisisitiza kuhusu mpango wa serikali yake wa kujenga vituo vya TEKNOHAMA kuwasaidia kufanya kazi kwenye kopmpyuta.

Rais Ruto alisema serikali yake ina mpango wa kuhakikisha kuwa  kuna vijana kati ya 200 na 300 wanaofanya kazi katika vitovu vya TEKNOHAMA katika kila wadi.

Alisema: "Vijana wana kazi mbili: kujitokeza katika vituo hivyo kwa mafunzo na kubonyeza kompyuta na kuweka pesa mfukoni."

Haya yanajiri majuma mawili tangu Waziri wa TEKNOHAMA na Uchumi Dijitali Eliud Owalo kuzindua vituo dijitali vya Jitume na mtandao wa intaneti (WiFi) katika Chuo cha Kiufundi na mafunzo anuwai cha Bungoma North, Tongaren.

Huu ni mpango mmojawapo wa serikali ya Kenya Kwanza kuinua vijana kiuchumi kupitia njia za kiteknolojia.

Mradi huu wa kutimizwa ndani ya mwongo mmoja (2022 – 2032), umeanza kutekelezwa 2024.

Serikali inalenga kujenga vituo 1,450 kote Kenya kuimarisha stadi za kidijitali kwa vijana, utayarishaji filamu na kuwezesha umma kupata huduma za serikali kutoka pembe zote za taifa.

@@@

Takwimu mpya za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa ugonjwa wa saratani umeendelea kuwa mzigo kubwa wa afya duniani na kusababisha vifo licha ya kuweko kwa mbinu za ugunduzi na matibabu, huku saratani  ya mapafu ikishika nafasi ya kwanza na ile ya titi ikishika nafasi ya pili na wadau wakitaka utashi wa kisiasa ili kutokomeza ugonjwa huo.

Taarifa iliyotolewa Februari Mosi Geneva, Uwisi na Lyon, Ufaransa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO inasema kauli hiyo inafuatia makadirio mapya ya mzigo wa ugonjwa wa saratani duniani.

Taarifa hiyo ilitolewa kwa mnasaba wa siku ya ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu ugonjwa huo ambayo imeadhimishwa  tarehe 4 mwezi huu wa Februari.

Makadirio hayo yaliyotolewa na shirika la kimataifa la utafiti wa saratani, IARC ambalo ni shirika tanzu la WHO yalitokana na utafiti katika nchi 185 yakionesha kuwa idadi kubwa ya nchi zilizoshiriki hazitengi fedha za kutosha na huduma ya uangalizi wa wagonjwa wa saratani si sehemu ya Mpango wa Afya kwa Wote, au UHC.

Mwaka 2022, kulikuweko na wagonjwa wapya milioni 20 wa saratani na kati yao hao milioni 9.7 walifariki dunia. Watu waliosalia hai miaka mitano baada ya kubainika kuwa na saratani ni milioni 53.5.

Takwimu zinaaainisha zaidi kwamba mtu 1 kati ya 5 anapata saratani maishani, sawa na mwanaume 1 kati ya 9, na mwanamke 1 kati ya 12 anakufa kwa saratani.

WHO kupitia takwimu zake za Huduma ya Afya kwa Wote, inasema miongoni mwa nchi 115 zilizohusika na utafiti huu, ni asilimia 39 pekee (39%) ndio zinajumuisha matibabu ya saratani kwenye bima ya afya. Asilimia 28 (28%) zimejumuisha huduma ya ziada ya  usaidizi kwa wagonjwa ikiwemo udhibiti wa maumivu ikiwemo  yale yasiyohusiana na saratani.

Utafiti umebaini kuwa aina 10 za saratani  kati ya aina 36 ndio zilibeba theluthi mbili ya maambukizi mapya ya saratani na vifo duniani kwa mwaka 2022 katika nchi 157 kati ya 185 zilizoshiriki kwenye utafiti.

Saratani ya mapafu ikitajwa kuwa inapata zaidi wanaume,ilishika nafasi ya kwanza ikiwa na wagonjwa wapya milioni 2.5,  ikifuatiwa na saratani ya titi inayopata wanawake na nafasi ya tatu ni saratani ya utumbo mpana. Saratani ya tezi dume ilikuwa ya nne, ile ya tumbo ya tano.

Utafiti huo unasema kuendelea kushika kasi kwa saratani ya mapafu “kunatokana na kuendelea kwa matumizi ya kupindukia ya uvutaji wa tumbaku barani Asia.”

Takwimu hizo zimeonesha kuwa saratani ya shingo  ya kizazi ilishika nafasi ya nane kwa kuwa na wagonjwa wapya, huku ikiwa ni ya tisa katika kusababisha vifo vitokanavyo na saratani ikiwa imekuwa na wagonjwa wapya 661,044 na vifo 348, 186.

WHO inasema Saratani ya Shingo ya Kizazi  ni saratani inayopata sana wanawake kwenye nchi 25, nyingi zao zikiwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. Taarifa hiyo inasema pamoja na kutambua viwango mbali mbali vya ugonjwa huo, saratani ya shingo ya kizazi inaweza kutokomezwa kama tatizo la afya ya umma kupitia Mpango wa WHO wa kutokomeza Saratani ya Shingo ya Kizazi

Shirika hilo linasema makadirio yake, kwa kuzingatia vyanzo bora vya takwimu vilivyopatikana mwaka 2022, yanaangazia ongezeko la mzigo wa ugonjwa wa saratani duniani, na madhara yake kwa jamii zisizopata huduma, na hivyo udharura wa kuondoa ukosefu wa uwiano wa huduma ya saratani duniani.

@@@