Feb 15, 2024 08:17 UTC
  • Iran yafanikiwa kuunda bendeji za ugonjwa nadra wa EB

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Kampuni ya kimaarifa ya kimatibabu ya Iran imeweza kuzalisha bendeji maalumu kwa wagonjwa wanaougua ugonjwa wa ngozi wa Epidermolysis Bullosa (EB), ugonjwa adimu wa kurithi ambao husababisha ngozi kuwa tete na kujeruhiwa kwa urahisi.

Mafanikio hayo ni ya wataalamu wa Kampuni ya Teba Zist Polymer yenye msingi wa maarifa au knowledge based, ambayo ni mzalishaji wa kwanza wa bendeji hizo za kipekee za   majeraha nchini Iran. Mafanikio hayo yamepatikana licha ya vikwazo vya muda mrefu vya nchi za Magharibi dhidi ya uagizaji wa vifaa vya matibabu na bidhaa za dawa nchini humo.

Kulingana na Idara ya Sayansi, Teknolojia, na Uchumi unaotegemea Maarifa, kampuni hiyo ya Iran imeweza kupata mbinu sawa na ile inayotumiwa na shirika la Mepilex ya Uswidi. Bendeji hiyo imezingatia  miongozo ya kimataifa inayopendekezwa kwa wagonjwa wa EB na majeraha yao.

Kampuni ya Teba Zist Polymer inakusudia kuzalisha bendeji hiyo kwa wingi na jina lake la kibiashara ni , Tebaflex. Uzalishaji wa bendeji hiyo  utaboresha hali ya afya ya wagonjwa wa EB nchini.

Vidonda vya wagonjwa wa EB huchukuliwa kuwa sugu na wale wanaougua ugonjwa huu adimu wa ngozi wanapaswa kutumia bendeji maalumu ya povu ili isishikane  majeraha na kusababisha uharibifu zaidi kwa malengelenge yao na ngozi nyeti.

Kutokana na vikwazo vya kikatili dhidi ya Iran vilivyoongozwa na Marekani, Sweden ilikataa kuiuzia Iran bendeji maalumu za Mepilex kwa wagonjwa wa EB. Ukosefu wa bendeji mbadala zinazofaa umepelekea kupoteza maisha ya watoto kadhaa wanaosumbuliwa na EB.

Ijapokuwa Washington na washirika wake wa Magharibi wanadai kuwa bidhaa za kibinadamu hazijawekewa vikwazo, makumi ya maelfu ya wagonjwa nchini Iran kwa miaka mingi wamekufa au kupata maradhi sugu kutokana na kutopatikana kwa dawa muhimu.

@@@

Mohammad Eslami Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema, leo hii sekta ya nyuklia ya Iran hususan katika uga wa mzunguko wa mafuta ya nyuklia imejitosheleza na sasa inategemea wataalamu wa ndani ya nchi kikamilifu.

Kwa mujibu wa IRNA; Mohammad Eslami aliyasema hayo katika hafla ya hivi karibuni ya kuzindua kifaa cha  cha spectrometa ya sumaku kilichopewa jina la Iranium katika Jumba la Uturubishaji la Shahid Ahmadi Roshan huko Natanz. Amesema lengo la adui tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilikuwa ni kuweka mipaka na kuzuia ustawi wa nchi katika nyanja mpya ambazo ni udhihirisho wa uwezo na kujiamini.

Ameongeza kuwa: "Msingi na lengo kuu la Mapinduzi ya Kiislamu lilikuwa ni kupata kujiamini na imani ya kimaendeleo kwa kuegemea imani za kitaifa na kidini, jambo ambalo maadui hawakulitafakari."

Islami alisema: Waliweka vikwazo vya pande zote dhidi ya tasnia ya nyuklia ya nchi Iran na pia walitekeleza njama za uharibifu wa viwanda , na ugaidi kwenye ajenda zao na walijaribu kuzuia shughuli zetu kwa kuvuruga michakato ya sasa.

Ameendelea kufafanua kuwa: "Leo hii sekta ya nyuklia ya Iran imepata nafasi nzuri hususan katika uga wa mzunguko wa uzalishaji fueli ya nyiklia. Hii inahesabiwa kuwa teknolojia muhimu zaidi katika uga wa kimataifa na yenye matumizi mengi tofauti, na Iran hivi sasa inajitosheleza katika masuala mbalimbali. 

Eslami amesema chombo kipya cha Iranium kilichoundwa kikamilifu na wataalamu wa Iran  hutumika kupima wigo wa atomi ambazo zipo katika dutu na kuogeza kuwai matumizi yake ni mapana katika tasnia isyo ya nyuklia.

@@@

Februari 10 huadhimishwa kama siku ya mikunde duniani na mwaka huu shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO linasema  siku hii imebeba maudhui ya kutanabaisha jukumu muhimu la jamii ya mikunde katika kuchagiza afya ya udongo na lishe ya binadamu.

Kwa mujibu wa FAO mikunde, kama vile maharagwe, njegere, na mbaazi, ni kikundi kidogo cha mazao ya jamii ya mikunde ambayo huvunwa kwa ajili ya mbegu zao za chakula, na huchukuliwa kuwa vyakula vyenye lishe kwa afya ya binadamu na mazingira.

Katika muktadha wa udongo, mikunde ina jukumu muhimu kwa kutoa virutubisho muhimu, kudumisha bioanuwai ya udongo, na kuimarisha muundo wa udongo.

Aina nyingi za kunde hustahimili ukame na kustahimili hali mbaya ya hewa, kama vile ukame na joto.

Pia shirika hilo linasema ukulima wake hupunguza matumizi ya mbolea, na hivyo kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu katika ujumbe wake wa siku hii amesema "Uwezo wa mikunde ni mwingi na ustahimilivu wake unaweza kuboresha afya ya udongo wetu na ya jamii za wenyeji. Mgogoro wa tabianchi, upotevu wa viumbe hai, mmomonyoko wa udongo na uharibifu ni changamoto kuu, na mapigo yanaweza kuwa sehemu ya suluhisho. Uwezo wa mikunde wa kustawi katika hali ya hewa tofauti pamoja na mali zake za kurekebisha nitrojeni, huifanya kuwa ya thamani sana,”

Mkuu huyo wa FAO amesisitiza haja ya kupanua wigo zaidi wa upatikanaji wa rasilimali za kijenetiki za mikunde, kuwekeza katika utafiti na uvumbuzi, teknolojia ya hali ya juu na mbinu za kilimo, na kuboresha uzalishaji, uvunaji, usindikaji na uuzaji wa mazao ya mikunde.

@@@

Nchini Kenya hivi karibuni wajumbe  Bodi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu Unitaid wamekagua faida za miradi bunifu ya kuimarisha sekta ya afya ambayo imeboresha maisha ya maelfu ya wakenya na wakati huo huo kuokoa fedha.

Herve Verhoosel ambaye ni msemaji wa shirika hilo tanzu la lile la Umoja wa Mataifa la afya, WHO akizungumza kutoka Nairobi, Kenya amesema “Kenya ni nchi iliyopewa kipaumbele na Unitaid kutokana na jinsi nchi hii ilivyo na uvumbuzi muhimu wa teknolojia mbalimbali za kusaidia sekta ya afya na pia ni moja ya nchi iliyo na idadi kubwa ya miradi inayofadhiliwa na Unitaid. Tuna zaidi ya miradi 11 ya kibunifu katika sekta ya afya kuanzia kwenye UKIMWI, Kifua kikuu, Malaria, saratani ya shingo ya kizazi mpaka kwenye huduma za watoto na wajawazito”

Ni kutokana na miradi hiyo ndio maana bodi ya Unitaid imeamua kutembelea nchi hiyo ili kujionea matokeo ya miradi wanayofadhili wakati huu ambapo pia wanajiandaa kupeleka miradi mingine mipya nchini humo.

Kwa ushirikiano na Kenya, Unitaid imeanzisha matumizi ya vipimo vya mapema vya Virusi Vya Ukimwi kwa watoto, dawa bora za kupunguza makali ya Ukimwi kwa watoto, dawa rafiki kwa watoto dhidi ya Kifua Kikuu, uchunguzi wa kisasa na tiba dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, chanjo mpya ya Malaria na ufikiaji rahisi wa uchunguzi na tiba dhidi ya COVID-19.”

Wajumbe wa Bodi walitembelea hospitali ya Kiambu Level 5 ambako walishuhudia tangi la kuhifadhia Oksijeni iliyo kwenye mfumo wa kimiminika ambapo msimamizi wa hospitali hiyo aliwaeleza kuwa uwepo wake  umepunguza kiwango cha vifo kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10.

Msaada wa kiufundi kutoka Unitaid uliwezesha serikali ya Kaunti ya Kiambu kununua tangi hilo kubwa la kujaza hewa ya Oksijeni katika mfumo wa kimiminika. Kila chumba katika hospitali hiyo kina bomba la hewa hiyo kutoka kwenye tangi.

Hewa ya Oksijeni kwa mfumo wa kimiminika husambazwa na kuhifadhiwa kwenye matangi kama kimiminika kwenye kiwango cha chini ya joto. Hubadilishwa kuwa Oksijeni ya matibabu kwenye mfumo wa hewa, katika kiwango cha kawaida cha joto kwa mgonjwa kuivuta pindi inapohitajika. Unitaid inasema katika hospitali, hewa hii ya Oksijeni husambazwa kwa kupitia mfumo wa mabomba ya hewa.

Aina hii ya Oksijeni hutumika kwenye sindano za nusukaputi, na wakati wa mgonjwa anaporejea mwelekeo wa kurejea kwenye hali ya kawaida baada ya upasuaji. 

Halikadhalika  hupatiwa mgonjwa pindi anapokuwa hana Oksijeni ya kutosha mwilini kama wakati wa upasuaji au mgonjwa anapokuwa amepata ajali kubwa ya barabarani. Halikadhalika mgonjwa anapokuwa ametokwa na damu nyingi, sumu ya Kaboni Monokside mwilini, kiwango cha juu cha joto, tatizo la mapafu au moyo na urejeshaji wa uhai kwa watu wazima na watoto.

Katika ziara hiyo iliyokamilika leo jioni kwa saa za Kenya, bodi ya Unitaid imekutana pia maafisa wa Wizara ya Afya ya Kenya, pamoja na wadau mbalimbali katika sekta ya afya walioko nchini humo. 

@@@