Feb 15, 2024 08:40 UTC
  • Satalaiti ya Thuraya (Soraya) ya Iran yatuma data kutoka anga za mbali

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Satalaiti ya Thuraya au Soraya ambayo imebuniwa na kutengenezwa kwa juhudi na hima ya wasomi vijana wa Iran na kurushwa katika anga za juu, imefanikiwa kutuma taarifa zake za awali na kuthibitisha kuwa imetua sehemu iliyokusudiwa kwa mafanikio makubwa.

Satalaiti hiyo ya mawasiliano iliyotengenezwa na wataalamu vijana wa masuala ya anga za mbali wa Iran, imetumwa angani kwa kutumia kombora la "Qaim 100" la Kikosi cha Anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC na kutua katika kizingo cha kilomita 750 kutoka usawa wa ardhi.

Shirika la Anga za Juu la Iran limetangaza kuwa, satalaiti hiyo ilifanikiwa kutuma taarifa zake za awali na kupokewa kwenye kituo cha ardhini, tarehe 21 Januari, 2024. 

Mafanikio ya satalaiti ya Thuraya na hasa kuweza kwake kutuma taarifa ardhini mara baada ya kufika kwenye umbali uliokusudiwa angani, ni muendelezo wa mafanikio ya jitihada za kielimu za wasomi na wataalamu vijana wa Iran ambao katika miaka ya hivi karibuni na licha ya kuweko vikwazo vya kila upande na vya kiuharibifu vya Marekani na madola ya Maghairi dhidi ya Iran, lakini vijana hao wameweza kupandisha juu uwezo wao wa kutengeneza satalaiti katika upande wa ubora na nguvu za satalaiti hizo.

Kufanikiwa satalaiti hiyo mpya ya Iran iitawayo Thuraya kutua katika umbali wa kilomita 750 kutoka usawa wa ardhi kumewashangaza wataalamu wa madola ya Magharibi na kukiri kwamba wanashindwa kujua ni vipi vijana wa Iran wameweza kupata mafanikio hayo katika kipindi kifupi tena wakiwa chini ya mashinikizo makubwa ya Marekani na madola mengine ya Magharibi. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, viongozi mbalimbali wa Magharibi hasa wa Marekani wamekuwa wakiponda mara kwa mara uwezo wa kielimu wa Jamhuri ya Kiislamu na lengo lao hasa ni kuwakatisha tamaa wananchi na vijana wa Iran, lakini njama zao hizo zimefeli.

Pamoja na kwamba katika miaka ya hivi karibuni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kutuma anga za mbali aina mbalimbali za satalaiti za kielimu, kiutafiti, kijiografia pamoja na za kijeshi, lakini madola ya Magharibi na vyombo vya habari vinavyofuata mkumbo huo muda wote vinanyamazia kimya mafanikio hayo ya Iran au vinaponda au vinahusisha mafanikio hayo na masuala ya kijeshi ili kuitangaza Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni hatari kwa nchi za eneo hili.

Satalaiti ya Noor 3 ambayo nayo ilitumwa anga za mbali mwaka jana 2023 ilikuwa ni satalaiti iliyoboreshwa na kizazi cha satalaiti za Noor 1 na Noor 2. Satalaiti hiyo ilikuwa ni ya kufanya utafiti wa aina mbalimbali. Satalaiti hiyo ilitumwa umbali wa kilomita 450 kutoka usawa wa ardhi.

Mafanikio ya satalaiti ya Thuraya ni uthibitisho wa mafanikio makubwa ya Iran katika masuala ya anga za mbali. Maendeleo ya masuala ya anga za mbali ya Iran ni makubwa kiasi kwamba, karibuni hivi Jamhuri ya Kiislamu itakuwa na mfumo wake mwenyewe maalumu wa satalaiti mbalimbali kwenye kizingo cha dunia.

Nafasi ya Iran katika sekta ya utaalamu wa anga za mbali imeimarika sana kwenye miaka ya hivi karibuni. Iran imeweza kubuni na kutengeneza satalaiti za kila namna za kielimu, kiutafiti, kijiografia na kijeshi.

@@@

Simu janja za mkononi zinazotegenezwa katika kiwanda cha Safaricom eneo la Athi River nchini Kenya zitauzwa kwa bei nafuu zaidi ya hadi asilimia 30 kuliko zinazoagizwa kutoka nje.

 

Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom Peter Ndegwa alisema punguzo hilo la bei litasaidia kampuni hiyo ya mawasiliano kuongeza matumizi ya simu zinazotumia 4G nchini Kenya na hivyo kusaidia kukuza mapato yake kutokana na biashara ya data.

Amenukuliwa na Jumamosi akisema kuwa: "Lengo letu la kutegeneza simu nchini ni kufikia viwango vya bei vinavyoruhusu wateja kumudu simu hizo.

Kiwanda cha kuunganisha simu, kinachojulikana kama East Africa Device Assembly Kenya Limited, kilianza kufanya kazi Oktoba mwaka jana na kinaendeshwa kama ubia kati ya Safaricom, TeleOne, na Jamii Telkom. Kiwanda hicho kinaweza kutegeneza takriban simu milioni tatu kwa mwaka, na kinwaweza kuongeza idadi kulingana na mahitaji.

Ndegwa alisema kiwanda hicho kinalenga kusafirisha nje katika ukanda wa Afrika Mashariki na kupanua uzalishaji zaidi ya simu.

Aidha alisema mbali na uzalishaji wa simu za mfumo wa 4G, kiwanda hicho pia kina uweza wa kuunda vifaa vingine, kama vile CPU za kompyuta.

Tayari kuna simu kadhaa zinazotegenezwa barani Afrika kama vile Mara Phones, Onyx Connect, na Mi-Fone.

Hadi kufikia 2021, tathmini ya soko la kimataifa la simu jana ilifikia dola bilioni 457.18, na makadirio ya kufikia $ 792.51 bilioni ifikapo 2029. Kwa sasa Afrika si mzalishaji mkubwa wa simu hizo za mkononi kwani utengenezaji mkubwa uko katika maeneo mengine pamoja na kuwa bara hilo lina soko kubwa.

@@

Cameroon Januari 22 imezindua mpango mpya wa chanjo ya malaria ya RTS,S kupatikana katika huduma zake za kawaida za chanjo za kitaifa, na kuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo nje ya mpango wa majaribio wa chanjo ya malaria ambao ulifanywa nchini Ghana, Kenya na Malawi. Hayo ni  kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO.

Uzinduzi huu unakuja huku juhudi zikiongezeka kwa kasi za kuongeza chanjo dhidi ya ugonjwa huo katika maeneo hatarishi barani Afrika, bara ambalo linachukua asilimia 94 ya visa vya malaria duniani kote na asilimia 95 ya vifo vinavyohusishwa na ugonjwa huo.

Dkt. Shalom Ndoula, katibu mkuu wa mpango mpana wa chanjo nchini Cameroon amesema "Chanjo hiyo italenga hasa watoto wote wenye umri wa miezi sita kufikia,"

Chanjo hiyo sasa imesambazwa katika vituo vya afya vya umma na vya kibinafsi, katika wilaya 42 za afya kwenye mikoa 10 ya nchi hiyo.

Uzinduzi huu unafuatia kuwasili kwa dozi 331,200 za chanjo nchini Cameroon mwezi Novemba 2023. Dozi zingine zinatarajiwa kuwasili katika wiki zijazo.

Kulingana na Dkt. Ndoula, chanjo hiyo ni zana ya ziada kwa ajili ya mapambano dhidi ya malaria, ambayo ilichaguliwa na nchi "kwa misingi ya sifa zake za awali, kuhakikisha hakikisho la ubora, ufanisi na usalama wa kuingizwa katika mpango wa chanjo".

Ili kujiandaa na uzinduzi huo, WHO na washirika wengine, ikiwa ni pamoja na Muungano wa chanjo duniani GAVI, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto  UNICEF, na Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, wameisaidia mamlaka ya afya ya kitaifa kuimarisha hatua muhimu za kuanzishwa kwa chanjo.

Kulingana na Dkt. Ndoula, chanjo hiyo ni zana ya ziada kwa ajili ya mapambano dhidi ya malaria, ambayo ilichaguliwa na nchi "kwa misingi ya sifa zake za awali, kuhakikisha hakikisho la ubora, ufanisi na usalama wa kuingizwa katika mpango wa chanjo".

Mbali na Cameroon, Benin, Burkina Faso na Liberia wamepokea chanjo hiyo na wanakamilisha mipango yao ya kuisambaza.

"Kuzinduliwa kwa chanjo ya malaria kunaashiria hatua muhimu katika kuzuia na kupambana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa na vifo," amesema mwakilishi wa WHO nchini Cameroon, Dkt. Phanuel Habimana.

Ameongeza kuwa "Tumejitolea kusaidia mamlaka za afya za kitaifa ili kuhakikisha usambazaji mzuri wa chanjo ya malaria pamoja na uimarishaji wa hatua nyingine za kukabiliana na ugonjwa wa malaria".

Cameroon ni miongoni mwa nchi 11 zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa malaria duniani. Nchi ilirekodi zaidi ya visa milioni 3 na vifo zaidi ya 3,800 mwaka wa 2021.

Vita dhidi ya malaria ni mojawapo ya vipaumbele vya mpango wake wa maendeleo ya afya ya kitaifa.

Juhudi za kudhibiti na kuzuia ugonjwa wa malaria zilizofanywa kwa miaka mingi kwa msaada wa washirika zimepunguza polepole mzigo wa ugonjwa huo nchini Cameroon.

@@@

Naam na hadi hapo tunafika mwisho wa makala yetu