Dec 16, 2023 06:21 UTC
  •  Iran imefanikiwa kutuma kapsuli ya kibiolojia katika anga za juu

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Hivi karibuni Iran imefanikiwa kutuma kapsuli ya kibiolojia katika anga za juu kwa kutumia roketi iliyoundwa nchini na iliyopewa jina la Salman.

Kapsuli hiyo yenye uzito wa kilo 500, iliyotengenezwa na Taasisi ya Utafiti wa Anga ya Iran, yenye uhusiano na Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia, ilirushwa katika anga za mbali Jumatano katika eneo lenye umbali wa kilomita 130 kutoka kwenye uso wa sayari ya dunia.

Kurushwa kapsuli hiyo ya kibiolojia katika anga za mbali ni hatua ya kuwapeleka wanadamu katika anga za juu huku serikali ya Iran ikiwa na mpango maalumu wa kufufua sekta mbalimbali za tasnia ya anga za juu.

Tukio hilo ni jaribio kwa teknolojia za anga katika sekta kama vile za kurusha marekoti ya kubeba satalaiti, muundo wa aerodynamic wa kapsuli, na mifumo inayohusiana na udhibiti na ufuatiliaji wa hali ya kibiolojia.

Roketi la Salman limeundwa kikamilkifu katika Kiwanda cha Anga za Mbali cha Iran ambacho ni kampuni tanzu ya Wizara ya Ulinzi ya Iran na ambayo ina uwezo wa kuzindua bio-capsules yenye uzito wa kilo 500. Kapsuli hiyo ya kibiolojia ilirejea katika sayari ya dunia kwa mafanikio baada ya kufika katika anga za juu.

Licha ya vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi katika miaka ya hivi karibuni, Iran imeweza kupiga hatua kubwa katika mpango wake wa anga za juu za kiraia.

Kapsuli yake ya kwanza ya kibiolojia ya Iran iliyokuwa na kiumbe hai ilirushwa katika anga za mbali mwezi Februari 2010, kwa kutumia roketi ijulikanayo kama Kavoshgar.

Akizungumza na shirika la habari la Fars, waziri wa mawasiliano wa Iran Issa Zarepour alisema hivi karibuni Tehran itafanya majaribio ya kizazi kipya cha kapsuli za kibiolojia, ili kukaribia malengo yake ya ustawi wa sekta ya anga za mbali.

Kwa kutilia maanani nafasi na mchango muhimu wa sekta ya anga za mbali na hasa satalaiti katika zama hizi kwenye nyuga zote zikiwemo za mawasiliano, habari, ugunduzi, ujasusi, mazingira na masuala mengi mengine, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia kwa dhati kustawisha miundomsingi na teknolojia yake ya makombora na anga za mbali na imeweza kupiga hatua na kupata maendeleo makubwa katika uga huo. Kubuni na kuunda maroketi ya kubebea satalaiti pamoja na hatua muhimu zilizopigwa katika utengezaji wa satalaiti zinazotokana na utaalamu wa ndani, urushaji wake, upokeaji data na taarifa na hatimaye utumiaji wa data hizo, ni mfumo kamili wa teknolojia hiyo ya anga za mbali na sasa Iran imeweza kumiliki mfumo huo.

Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza kabisa inayojulikana kwa jina la Omid (yaani Tumaini) mwaka 2009.

Iran pia imetangaza kuwa, katika kipindi cha miaka michache ijayo itatuma mwanaadamu katika anga za mbali. Tayari mazoezi yameshafanyika kuhusiana na lengo hilo kwa kutumwa nyani hai katika anga za mbali ambaye alirejea ardhini akiwa salama.

Iran ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza katika tasnia ya anga za juu na kati ya 7 zinazoongoza katika anga za mbali.

Kamati ya Aki Mnemba Iran

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa agizo la kuanzishwa 'Kamati ya Kitaifa ya Uongozi na Kituo cha Kitaifa cha Akili Mnemba, (yaani Artificial Intelligence-AI-)'.

Kuunda mlolongo kamili na thabiti wa mawazo katika sekta ya Akili Mnemna, kufaidika na Akili Mnemba katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi, kupanga kufikia nafasi inayoongoza na endelevu kati ya nchi za ulimwengu na pia kutambua na kukuza talanta katika uwanja huo wa AI ni kati ya kazi muhimu zaidi za Kituo cha Kitaifa cha Akili Mnemba.

Hayo yamebainishwa na Rouhollah Dehqani-Firouzabadi, Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya Sayansi, Teknolojia na Uchumi wa Maarifa.

Amesema ameandaa mipango mitatu ya kina ya kuendeleza Akili Mnemba katika sekta tofauti.

Mnamo Januari 2022, Shahram Moein, mkuu wa kituo cha uvumbuzi na maendeleo cha Akili Mnemba katika Taasisi ya Utafiti wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, alisema, "Iran itawekwa kati ya nchi 10 bora katika Akili Mnemba (AI) ifikapo 2032 kulingana na hati ya kitaifa juu ya mkakati wa upelelezi bandia."

Utafiti wa ramani ya kitaifa ya maendeleo ya akili bandia ulianza miaka miwili iliyopita katika Taasisi ya Utafiti wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na ukakamilishwa rasmi mwishoni mwa Novemba 2021.

Kituo cha Mabadiliko ya Kidijitali cha GIZ cha Kenya

Kituo cha Mabadiliko ya Kidijitali cha GIZ cha Kenya (DTC) kimezindua Kitovu cha Ubunifu cha Kijani na Kidijitali Kenya (gDIH) wakati wa Wiki ya Ubunifu ya Kenya (KIW) ya kila mwaka iliyofanyika Novemba. Mpango huo ambao ulianza kufanya kazi mnamo Desemba, unalenga kuimarisha biashara ndogo ndogo, ndogo na za kati (MSMEs) kote nchini Kenya, kuwapa ufikiaji mpana wa rasilimali za teknolojia na uvumbuzi.

GDIH itazingatia sekta za kimsingi kama vile Kilimo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Nishati, ikijumuisha teknolojia za kisasa kama vile Uendeshaji (Akili Mnemba-AI,  na Intaneti ya Vitui au IoT), Usalama wa Mitandaoni, Kompyuta Winguni, na Miji Erevu. Kwa kuangazia sekta na teknolojia hizi, kitovu hicho kinatarajia kuchukua jukumu muhimu katika kusimamia mpito wa kidijitali na kijani katika kanda.

Ili kukuza utamaduni wa uvumbuzi wa kidijitali na ujasiriamali, Kitovu cha Ubunifu cha Kijani na Kidijitali Kenya kinapanga kuzipa biashara ndogo ndogo, ndogo na za kati safu ya kina ya huduma muhimu kwa kustawi katika uchumi wa kidijitali. Hii ni pamoja na ukuzaji wa ujuzi, ufikiaji wa fedha, vifaa vya majaribio, na uanzishaji wa mfumo ikolojia wa uvumbuzi. Zaidi ya hayo, Kitovu cha Ubunifu cha Kijani na Kidijitali Kenya kinalenga kutumika kama jukwaa shirikishi la kujifunza na ukuaji huku kikikuza mazoea ya biashara endelevu.

Kitovu cha Ubunifu cha Kijani na Kidijitali Kenya kikiwa kinaendeshwa na muungano unaoongozwa na Kituo cha Kiafrika cha Mafunzo ya Teknolojia (ACTS), kina makao yake Nairobi lakini kinaweza kufikiwa na biashara ndogo ndogo, ndogo na za kati (MSMEs) kote nchini Kenya. Vyombo vingine vinavyounda muungano huo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta, Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda ya Kenya, Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo la Kenya, Shirika la Kitaifa la Ubunifu la Kenya, na Jiji la Kiktenolojia la Konza.

Utafiti wa viashiria vya UKIMWI 2022/2023 nchini Tanzania

Na matokeo ya awali ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI 2022/2023 nchini Tanzania yalizinduliwa Disemba Mosi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) ikiwa ni kilelel cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kitaifa yamefanyika Mkoani Morogoro.

Akizindua matokeo ya utafiti huo Mhe. Kassim Majaliwa amesema matokeo ya awali yanaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, lakini harakati za kuutokomeza ugonjwa huo bado zinaendelea.

Aidha, Mhe. Waziri Mkuu amesema utafiti huo unaonesha wanawake wamejitokeza kwa wingi zaidi katika upimaji wa VVU huku wanaume wakiwa nyuma, hivyo ametumia fursa hiyo kuwataka wanaume nchini kuwa mstari wa mbele katika kupima VVU.

Aidha, utafiti huo umeonesha kuwa watu wanaoishi na VVU kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 15 ni asilimia 4.4, kwa kigezo cha jinsia utafiti umeonesha wanawake ni asilimia 5.6 ikilinganishwa na asilimia 3.0 kwa wanaume, kigezo cha makazi mijini asilimia 4 na vijijini asilimia 4.