Sep 05, 2023 11:10 UTC
  • Sura ya Annajm, aya ya 31-42 (Darsa ya 967)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 967 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 53 ya An-Najm. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 31 na 32 ya sura hiyo ambazo zinasema:

‏ وَلِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى

Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, ili awalipe walio tenda ubaya kwa waliyo yatenda, na walio tenda mema awalipe mema.

 الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ وَاسِعُ الْمَغْفِرَةِ ۚ هُوَ أَعْلَمُ بِكُمْ إِذْ أَنشَأَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَإِذْ أَنتُمْ أَجِنَّةٌ فِي بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ ۖ فَلَا تُزَكُّوا أَنفُسَكُمْ ۖ هُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اتَّقَىٰ

Ambao wanajiepusha na madhambi makuu na vitendo vichafu, isipo kuwa makosa khafifu. Hakika Mola wako Mlezi ni Mkunjufu wa maghfira, naye anakujueni sana tangu alipo kuumbeni kutoka kwenye ardhi, na mlipo kuwa mimba matumboni mwa mama zenu. Basi msijitakase nafsi zenu. Yeye anamjua sana mwenye takua.

Aya hizi zinazungumzia kanuni aliyoiweka Allah ya utoaji malipo ya thawabu na adhabu na kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu, ambaye ni Mmiliki wa mbingu na ardhi, hajawaacha watu kama walivyo kwa maana ya kuwa huru kufanya vyovyote vile watakavyo na lolote lile wapendalo, bali ameweka kanuni na mfumo maalumu wa kuhakikisha wafanyao mema wanalipwa thawabu kwa mema waliyofanya na watendao mabaya na maovu, nao pia wanapata malipo ya adhabu kwa maovu waliyotenda. Kwa upande wa matendo mabaya, hayawekwi yote kwenye mizani ya uzito mmoja, bali yapo baadhi yao ambayo ni madhambi na makosa makubwa na baadhi yao ni madogo. Baadhi ya madhambi huwa mtu anayafanya kwa kukusudia na baadhi yao huyafanya bila kudhamiria. Na kwa sababu hiyo, Allah SWT anaamiliana kwa sura tofauti na kila moja kati yao. Kama mtu atakuwa amefanya dhambi kwa kuteleza kisha akaijutia dhambi hiyo na kutia nia ya kutoirudia tena, Mwenyezi Mungu Mtukufu atamsamehe; lakini kinyume na hivyo mtu huyo hatopata maghufira na msamaha wa Mola kwa dhambi aliyofanya. Katika aya hizi tulizosoma, imesisitizwa pia nukta moja ya msingi, nayo ni kwamba, msijitukuze na kujitakasa mbele za watu kwa sababu ya kufanya mambo mema na kujiweka mbali na madhambi ya dhahiri, kwa sababu Yeye Allah SWT ni mjuzi wa batini, yaani hakika ya amali zenu ilivyo ndani ya nafsi zenu, na anawajua ni nani miongoni mwenu wenye taqwa na uchamungu wa kweli. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ulimwengu umeumbwa kwa ajili ya mwanadamu, na yeye mwanadamu ni masuuli na atakwenda kuwajibika mbele ya Mwenyezi Mungu kwa yote ayafanyayo hapa duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, waja wema watendao mazuri na ya kheri, nao pia hukosea, wakateleza kwa kufanya dhambi. Lakini kutokana na kuwa na nyoyo safi, huwa hawaiendei dhambi kwa makusudi; na pale wanapoteleza wakafanya maasi huomba maghufira na kutubia. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, tusije wakati wowote ule tukajihisi hatuna kasoro, wala hatuwezi kufanya baya. Tusijisifu na kuingiwa na ghururi kwa tuyafanyayo, kwa sababu kama watu hawajui undani wa tunayoyatenda, Allah SWT ni mjuzi na mwelewa wa matendo yetu; na muhimu zaidi  anaijua nia na yaliyofichikana ndani ya nafsi zetu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 33 hadi ya 38 ya sura yetu ya An-Najm ambazo zinasema:

أَفَرَأَيْتَ الَّذِي تَوَلَّىٰ

Je! Umemwona yule aliye geuka?

وَأَعْطَىٰ قَلِيلًا وَأَكْدَىٰ

 Na akatoa kidogo, kisha akajizuia?

أَعِندَهُ عِلْمُ الْغَيْبِ فَهُوَ يَرَىٰ

Je! Anayo huyo ilimu ya ghaibu, basi ndio anaona?

 أَمْ لَمْ يُنَبَّأْ بِمَا فِي صُحُفِ مُوسَىٰ

Au hakuambiwa yaliyomo katika Vitabu vya Musa?

 وَإِبْرَاهِيمَ الَّذِي وَفَّىٰ

Na vya Ibrahimu aliye timiza ahadi?

أَلَّا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ

Ya kwamba habebi mbebaji mzigo wa mwengine?

Katika aya zilizopita, yalizungumziwa masuulia na dhima anayobeba mtu kwa amali zake. Aya tulizosoma zinatilia mkazo suala hilo kwa namna nyingine na kueleza kwamba, baadhi ya watu huwa wanadhani Siku ya Kiyama wataweza kumbebesha mtu mwingine mzigo wa madhambi yao na wao wenyewe kujivua na dhima ya madhambi hayo. Kwa upande mmoja, watu hao huwa wanafanya ubakhili katika kutekeleza jukumu lao la utoaji kuwasaidia wanyonge na wahitaji; na kwa upande mwingine huwa hawako tayari kubeba dhima na masuulia ya matendo yao mabaya na maovu wanayofanya. Watu hao wana mtazamo huo ilhali mojawapo ya usuli na misingi ya dini zote za tauhidi, ambao umebainishwa ndani ya vitabu vya mbinguni vilivyotangulia na hata Mitume na Manabii wakautilia mkazo pia, ni msingi mkuu na muhimu usemao, kila mtu anabeba dhima ya matendo yake na wala haiwezekani kutumia njia yoyote ile kama ya ulipaji fedha ili kumbebesha dhambi zako mtu mwingine na wewe ukasalimika na matokeo ya amali zako. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, utoaji endelevu na wa kudumu wa kuwasaidia wahitaji ndio unaomletea mtu kheri na saada. Kutoa msaada kimsimu na kwa nadra ni ishara ya kutokuwa na imani ya dhati na ya moyoni juu ya jukumu hilo la kidini na kiutu. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa, Nabii Ibrahim AS alikuwa ruwaza na mfano wa kuigwa katika utimizaji ahadi na kujitolea mhanga. Utimizaji ahadi kwa Allah na kujitolea mhanga nafsi yake, mke na mtoto wake kwa ajili ya Mola wake. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujihadhari tusije tukahadaiwa na watu watakaotuchochea kufanya dhambi kisha wakatuambia: mimi ninabeba dhima na masuulia ya dhambi hiyo! Ukweli ni kwamba katika mfumo wa haki na uadilifu wa Allah, hakuna mtu yeyote awezaye kubeba dhima ya dhambi za mtu mwingine.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 39 hadi ya 42 ya sura yetu ya An-Najm ambazo zinasema:

وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ

Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyo yahangaikia?

 وَأَنَّ سَعْيَهُ سَوْفَ يُرَىٰ

Na kwamba (matunda) ya mahangaiko yake yataonekana?

ثُمَّ يُجْزَاهُ الْجَزَاءَ الْأَوْفَىٰ

Kisha ndio atalipwa malipo yake kwa ukamilifu.

وَأَنَّ إِلَىٰ رَبِّكَ الْمُنتَهَىٰ

Na kwamba mwisho (wa kila jambo) unarejea kwa Mola wako Mlezi.

Msingi mwingine ambao umekuwepo katika dini zote za tauhidi, ambao unatokana na uadilifu wa Allah TWT ni kwamba, kila mtu atanufaika kulingana na kiwango cha juhudi anazofanya katika kutimiza wajibu wake na ndivyo atakavyolipwa thawabu Siku ya Kiyama. Kama ambavyo haiwezekani mtu kumbebesha mwenzake mzigo wa mabaya yake, vivyo hivyo haiwezekani kutumia kisingizio chochote kile kujivutia mema ya watu wengine na kujihisi mtu kuwa anastahiki kulipwa thawabu yeye kwa mema ya watu hao. Bila shaka, inawezekana pia mtu akafanya jitihada na idili kubwa, lakini jitihada zake hizo zisizae matunda au asipate matilaba na yale hasa aliyokusudia. Kwa sababu hiyo, Qur'ani tukufu imetumia neno "saa'i", yaani jitihada ili mtu asikate tamaa wala kuvunjika moyo kwa sababu ya mambo aliyofanya, ambayo hayakuwa na tija, bali ajue kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anaziona juhudi zake na atampa malipo kamili ya mema aliyojitahidi kufanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wajibu na jukumu letu sisi ni kufanya juhudi katika kutekeleza maamrisho ya Allah, lakini matokeo ya juhudi zetu hayako kwenye mamlaka yetu. Kwa hivyo linalotuwajibikia sisi ni kutekeleza jukumu na amri aliyotupa Mola, lakini hatudhaminiwi kupata matokeo na tija tunayoitaka sisi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hakuna amali yoyote ifanywayo katika ulimwengu wa uumbaji itakayofutika. Kuamini kwamba amali yoyote ile inabaki na kuamini juu ya kuwepo mfumo wa kiuadilifu wa ulipaji thawabu na adhabu, vinamshajiisha na kumtia raghaba mtu ya kufanya mambo mema na vilevile vinamfanya awe na hadhari kwa kutambua kuwa ni yeye mwenyewe ndiye atakayebeba dhima ya matendo yake. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, dunia hii haina uwezo kamili na wa kutosha kwa ajili ya kutekelezea malipo ya amali za watu, na ndio maana inapasa kiwepo Kiyama ili haki ya kila jambo ilipwe kwa namna hasa inayostahiki. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kuwa, Mwenyezi Mungu SWT anayaona tuyafanyayo na atatupa malipo kamili kulingana na nia na malengo yetu pamoja na juhudi tulizofanya. Na kutokana na aya hizi tunajielimisha pia kwamba, kama tunaiamini Siku ya Kiyama na kwamba hatima na mwisho wa amali na matendo yetu uko mikononi mwa Allah, basi tusifanye ajizi hata chembe katika kutekeleza majukumu yetu ya kidini na tujipinde pia kufanya bidii na juhudi ukomo wa uwezo wetu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 967 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa na ikhlasi katika matendo yetu, azitakase na kila aina ya maradhi ya kiroho nyoyo zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/    

 

Tags