Sep 23, 2023 17:25 UTC
  •  Iran kwa mara ya kwanza yazalisha mada ya Cesium-137 radionuclid

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Wataalamu wa nyuklia wa Iran kwa mara ya kwanza wameweza kuzalisha mada ya Cesium-137 radionuclide ambayo ilikuwa inaagizwa kutoka nje.

Mada hiyo ambayo hutumika kwa madhumuni mengi ya matibabu na viwanda ilizinduliwa wakati wa maonyesho ya hivi karibuni katika mji mkuu wa Iran, Tehran katika kikao kilichohudhuriwa na Mohammad Eslami, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI).

Radionuclides (au radioisotopi) ni anuai atomiki za mionzi ambazo aghalabu huibuliwa katika mkondo wa nyutroni kwenye kinu cha nyuklia.

Mada hii inatumika katika vifaa vya mionzi, brachytherapy, radiotherapy, chemchemi za calibration, na aina mbalimbali za vipimo vya viwanda.

Mada hii aidha hutumika katika kutengeneza bidhaa za damu, vipodozi, chakula, na bidhaa zingine.

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imepata maendeleo ya ajabu katika sekta ya nyuklia licha ya vitisho na vikwazo vya madola ya Magharibi. Tehran daima imekuwa ikisisitiza kwamba mpango wake wa nyuklia unatekelezwa kwa malengo ya amani.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Eslami amesema kuwa pamoja na mzunguko wa nishati ya nyuklia, Iran ina uwezo wa kubuni, kujenga na kudumisha vinu vya nyuklia, akibainisha kuwa sekta ya nyuklia ya nchi ina jukumu la moja kwa moja katika maisha ya watu.

Hali kadhalika amesema adui zetu walikuwa na wangali wanapinga sekta ya nyuklia ya Iran, lakini wote wanapaswa kujua kwamba sekta ya nyuklia ni sekta ya kimkakati.

Mkuu huyo wa nyuklia wa Iran pia amesifu utengenezaji wa Cesium-137 radionuclide kama mafanikio muhimu ya nyuklia ambayo yanaondoa utegemezi wa nchi kwa nchi zingine kwa uagizaji wa mada hiyo.

Amesema Cesium-137 radionuclide inaweza kutumika katika mifumo ya vifaa vya viwandani, maeneo ya mafuta na gesi na sekta nyinginezo.

Eslami ameongeza kwamba Iran inaendelea kushirikiana na Wakala wa Umoja wa Mataifa wa Nishati ya Atomiki na kwamba maeneo manne ya mvutano na wakala huo yamepunguzwa hadi maudhui mbili tu.

Rwanda kuunda kinu cha nyuklia
Serikali ya Rwanda imetia saini makubaliano na shirika kutoka mataifa ya Canada na Ujerumani, ili kuanzisha ujenzi wa kinu cha nyuklia ambacho kitakuwa tayari kwa majaribio ifikapo mwaka 2026.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ya "Dual Fluid Energy", Goetz Ruprecht amewaambia waandishi wa habari mjini Kigali kuwa " aina mpya ya vinu hivyo, inaweza kutumiwa kuzalisha umeme, haidrojeni na mafuta yaliyosindikwa kwa gharama ndogo kuliko mafuta ya visukuku.

Waziri wa miundombinu wa Rwanda Ernest Nsabimana amesema kuwa, matumizi ya nishati ya nyuklia yatatoa chanzo thabiti na cha kuaminika cha umeme, kupunguza utegemezi wa mafuta na kusaidia kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati.

Nsabimana ameendelea kusema kuwa kujumuisha nyuklia katika jumla ya vyanzo vya nishati kutapelekea kuwa na aina mbalimbali za vyanzo vya nishati, kuimarisha usalama wa nishati na kupunguza hatari ya uhaba wa usambazaji.

Awali mnamo mwaka 2019, Rwanda ilitia saini mkataba wa kuanzisha vinu vya nyuklia kwa ushirikiano na wakala wa nyuklia wa Russia "Rosatom", jambo lililozusha upinzani mkali hasa kuhusu hatari zinazohusiana na masuala ya kiusalama.

Rais wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha "Democratic Green Party of Rwanda", Frank Habineza, ameziambia duru za habari kuwa makubaliano kati ya serikali na Kampuni ya "Dual Fluid Energy" ni hatari na kwamba, hayana tofauti kubwa na makubaliano ya mwaka 2019 kati ya serikali ya Kigali na wakala wa nyuklia kutoka Russia.

Habineza amesisitiza: " Hakuna utafiti unaoweza kunishawishi kuwa kuna mahali katika nchi hii (Rwanda) ambapo kinu cha nyuklia kinaweza kujengwa bila kuyaweka maisha ya watu hatarini."

Bodi ya Nishati ya Atomiki ya Rwanda  ikishirikiana na Kampuni hiyo imebaini kuwa miradi yao ni salama na wala si tishio kwa watu au mazingira. Katika taarifa yao ya pamoja wameeleza: " Kinu chetu cha majaribio ni kifaa kidogo chenye chembechembe ndogo za mionzi. Kwa sababu hii, maradi huu si tishio kwa mazingira."

Siku ya Kimataifa ya uhifadhi wa Tabaka la Ozoni

Dunia imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya uhifadhi wa Tabaka la Ozoni, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akisema kwa pamoja walimwengu wanaweza kuepuka athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha uendelevu wa mazingira na mnepo kwenye sayari.

Mwaka1994, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza Septemba 16 kuwa Siku ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Tabaka la Ozoni, katika kuadhimisha kutiwa saini Itifaki ya Montreal juu ya vitu vinavyopunguza na kuathiri tabaka la Ozoni iliyopitishwa mwaka 1987.

Ozoni ni aina maalum ya oksijeni yenye fomula ya kemikali O3. Ozoni ni sehemu ndogo sana ya anga ya juu, lakini uwepo wake ni muhimu kwa afya na ustawi wa binadamu.

Tabaka la Ozoni hupatikana kati ya kilomita 10 na 40 juu ya uso wa Dunia. Eneo hili linaitwa stratosphere, na lina karibu asilimia 90 ya ozoni yote ya angani.

Kaulimbiu ya siku ya kimataifa ya Ozoni mwaka huu inalenga kuangazia nafasi ya Itifaki ya Montreal katika kulinda tabaka la ozoni na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya Ozoni amesema, "Mikataba ya kimataifa ya kulinda tabaka la ozoni imesaidia kufikia mabadiliko makubwa na yanayoonekana katika kulinda watu na sayari."

Ameongeza kuwa "Inathibitisha ufanisi wa mbinu ya kimataifa." Watu wote wanapaswa kuhamasisha matumaini kwamba kwa pamoja tunaweza kuepuka athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha uendelevu wa mazingira na mnepo kwenye sayari.

Tarehe 16 Septemba 2009 mkataba wa Vienna na itifaki ya Montreal ilikuwa mikataba ya kwanza katika historia ya Umoja wa Mataifa kuidhinishwa duniani kote.

UNESCO yatoa muongozo kuhusu akili mnemba au  Artificial Intelligence yaani AI mashuleni

Wakati muhula mpya wa masomo ukianza Septemba maeneo mengi duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO limetoa muongozo wenye vipengele saba unaotaka nchi kudhibiti matumizi ya akili mnemba au – Artificial Intelligence yaani AI mashuleni.

Katika taarifa yake aliyoitoa wiki ya kwanza ya Septemba, mjini Paris Ufaransa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema matumizi ya AI yanaweza kuwa na fursa kubwa kwa maendeleo ya binadamu, lakini pia inaweza kusababisha madhara na chuki.

AI haiwezi kuunganishwa katika elimu bila ushirikiano wa umma, na ulinzi na kanuni muhimu kutoka kwa serikali.”

Mwongozo huo utazinduliwa rasmi Makao Makuu ya UNESCO wakati wa Wiki ya Mafunzo ya Dijitali ya UNESCO ambayo inakutanisha washiriki zaidi ya 1000 ili kujadili mada kuhusu majukwaa ya umma ya kujifunza kidijitali na matumizi yaAI katika elimu, pamoja na mada nyingine nyingi.

Miongoni mwa mambo yanayopaswa na kushughulikiwa haraka na nchi ni pamoja na kuwa na sera ya matumizi ya AI kimaadili katika elimu na utafiti, kuwe na faragha, umri uanzie miaka 13, pamoja na walimu wapatiwe mafunzo kuhusu AI.

Mwongozo huu pia unajibu hoja zilizoonyeshwa kwenye jedwali la kwanza la mawaziri la kimataifa kuhusu AI lililopitishwa na UNESCO mwezi Mei 2023.

Bi.Azoulay amesema mongozo huo wa UNESCO utasaidia watunga sera na walimu kutumia vyema uwezo wa AI kwa maslahi ya kimsingi ya wanafunzi.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema iwapo jamii ya kimataifa haitachukua hatua za makusudi za kuzuia kuenea kwa matumizi mabaya ya zana za teknolojia ya akili mashine (AI), huenda teknolojia hiyo ikageuka kuwa zimwi lisilodhibitika.

Antonio Guterres alisitiza kuwa, kuna haja kwa dunia kuunda mifumo na sheria za kuzuia matumizi mabaya ya teknolojia hiyo ya Artificial Intelligence.

Onyo la Katibu Mkuu wa UN limekuja wiki chache baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutahadharisha pia kuhusu hatari ya matumizi mabaya ya akili mashine (AI).

Kwa mujibu wa WHO, roboti zinazoundwa na akili bandia zinaweza kutumiwa vibaya kuzalisha na kusambaza taarifa za uongo zenye kushawishi kwa njia ya maandishi, sauti au maudhui ya video ambayo ni vigumu kwa umma kutofautisha na maudhui salama na ya kuaminika.

Naam na hadi hapo ndio tunapofika mwisho wa makala yetu ya sayansi na teknolojia kwa leo. Ni matumaini yangu kuwa umeweza kunufaika