Oct 03, 2023 17:36 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (82)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

 

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 82 ya mfululizo huu kitamzungumzia msomi, mwanaharakati na alimu mwingine mashuhhuri wa Kishia ambyo si mwingine bali ni Sayyid Jamaluddin Asadabadi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.

 

Tangu kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu na Wairani kuukkubali Uislamu, idadi kubwa ya watu wa kizazi cha Mtume (SAW) walikuja Iran na wakatawanyika katika miji tofauti. Ilikuwa imepita takriban miaka 1250 tangu kudhihiri Uislamu, wakati huko Hamedan moja ya miji ya Iran alipozaliwa mtoto ambaye aliitwa Jamal al-Din. Baba na mababu zake Jamal al-Din walikuwa maarufu kwa heshima na uchamungu huko Asadabad, mojawapo ya wilaya za Hamedan. Sayyid huyu mdogo, ambaye baadaye alijulikana kwa jina la Sayyid Jamaluddin Asadabadi, alianza kujifunza Qur'an na masomo ya msingi kutoka kwa wazazi wake na tangu enzi za utoto wake, alikuwa akifikiria juu ya suluhisho na tiba ya maumivu, mateso na masaibu ya wengine.

Tabia, maneno na matendo yake yalikuwa tofauti na watoto wengine na hata michezo yake ilikuwa tofauti. Ilitokea mara nyingi kwamba alikuwa akichukua kipande cha mti na kukifanya kama farasi wake ambapo akiwa pamoja na marafiki zake wawili, alijifanya kuwa alikuwa akisafiri kwenda India, Misri, Roma, na Afghanistan, na cha kushangaza ni kuwa, michezo hii baadaye iliondokea na kuunda ukweli na uhalisia wa maisha yake.

Hima na umakini wa Seyyid Jamaluddin katika kujifunza elimu mbalimbali ulikuwa wa kupigiwa mfano. Ilimtosha kusoma kitabu kimoja katika elimu yoyote mbele ya ustadh, basi kwa uwezo wake wa kufikiri na kutoa hoja, angejifunza vitabu vingine vya fani hiyo peke yake bila kuhitaji mwalimu kama ambavyo angeweza pia fundisha wengine. Alisoma fasihi ya Kiarabu, fiq'h, usul na mantiki katika Hawza na chuo cha Qazvin, na wakati huo huo, alipenda sana kujifunza elimu nyingine kama tiba.

 

Baada ya Qazvin, aliingia Tehran akiwa pamoja na baba yake kwa ajili ya kuendelea na masomo, na akiwa bado hajafikisha umri wa baleghe, alivaa kilemba kwa mara ya kwanza. Alitoka Tehran hadi Najaf na akatumia miaka mingine minne akisoma elimu za akili na nakili kwa Sheikh Morteza Ansari, kiongozi wa Mashia duniani wakati huo. Mbali na Tafsir, Hadithi, Fiqh na Usul, Seyyid Jamaluddin Adadabadi alikamilisha pia falsafa, mantiki, tiba, elimu ya nyota na hisabati, na alipokuwa kijana wa miaka 16, alifanikiwa kupata shahada ya Ijtihad kutoka kwa mwalimu wake, Sheikh Murtadha Ansari. Sheikh Ansari, akijua kipaji cha elimu na nguvu ya ushawishi wa maneno sambamba na nguvu ya utendaji wa kijana huyu Sayyid alimpeleka India, na safari hii ndiyo iliyotoa muelekeo tofauti katika maisha yake ya kijamii na kisiasa. Ilikuwa kuanzia wakati huu ambapo safari zake za kwenda India, Roma, Misri na Afghanistan zilianza na hivyo kutimiza ndoto zake za utotoni.

Baada ya miaka miwili ya kushuhudia maisha ya watu na mijadala ya kielimu ya wasomi na wanafikra wa India, Seyyed Jamaluddin Asadabadi alifikia hitimisho kwamba ili kuiokoa India kutoka kwa ukoloni wa Waingereza, ni lazima afikirie mpango na sera mpya. Ni kwa msingio huo ndio maana kabla ya kila kitu alifanya juhudi za kumsoma na kumtambua adui na akafanya hima ya kufahamu nukta za nguvu za adui mkabala na nukta dhaifu za Waislamu. Ili kukamilisha utambuzi na ufahamu huu, alivumilia magumu na taabu nyingi za safarini.

Alitoka India hadi Afghanistan na kisha Makka, Madina, Jordan, Damascus, Aleppo, Mosul na Baghdad, na akachunguza kwa kina hali ya miji yote muhimu ya Kiislamu na hatimaye akarudi Kabul huko Afghanistan. Akafikia natija hii kwamba, machungu ya jamii za Kiislamu ni dhulma ya watawala na ukoloni wa nchi za magharibi, na maumivu makubwa zaidi ni ujinga na kutokuwa na ufahamu watu sambamba na na athari za ushirikina katika fikra za Waislamu, fikra ambazo zimeleta mgawanyiko na utengano baina ya Waislamu na hili limewafanya wasiwe na nguvu dhidi ya ukoloni na dhulma. Kuanzia hapo alitumia juhudi zake zote kuwafahamisha watu na kuwaunganisha Waislamu dhidi ya dhulma na ukoloni.

 

Mnamo mwaka 1278 Hijria wakati Seyyed Jamal alipoingia Kabul kwa mara ya pili, alikuwa na umri wa miaka 24 tu, lakini fikra, mtazamo na mawazo yake yenye upeo mkubwa yalimteka Emir wa Kabul, Dost Muhammad Khan. Uhusiano wake mzuri na Amir ulimfanya aweze kuingilia kati mageuzi ya mambo ya serikali pamoja na kuandika vitabu na kuchapisha magazeti. Kukamilisha baraza la mawaziri, kuandaa jeshi, kuunda shule kwa ajili ya vijana, kukuza lugha ya taifa, kuanzisha hospitali, ofisi ya posta, zahanati ya mifugo na makao ya wazee, nii miongoni mwa mambo aliyofanya akiwa nchini Afghanistan. Katika hali ambayo ilikuwa imepita miaka michache tangu kifo cha Dost Muhammad Khan, shughuli za kitamaduni-kisiasa za Seyyed Jamaluddin nchini Afghanistan zilikuwa bado zinapanuka na zilipokelewa na watu. Katika mazingira kama haya, adui alihisi kukabiliwa na tishio kubwa na hakuweza kuvumilia uwepo jamaluddin nchini Afghanistan. Sayyid Jamaluddin alilazimika kuondoka kwenda India, lakini serikali ya Uingereza huko India ilimruhusu kukaa huko kwa miezi miwili tu. Pamoja na hayo, katika kipindi hiki kufupi, Seyyed Jamaluddin alijaribu kuwafahamisha watu kuhusu hatari ya ukoloni kupitia hotuba zake.

Hotuba na maneno yake yaligusa mioyo ya watu kiasi kwamba, Waingereza walilazimika kumfukuza kutoka India kabla ya kumalizika muda wake wa miezi miwili aliokuwa amepatiwa. Ni katika kipindi hiki ndipo Seyyid Jamal al-Din Asadabadi alipolekea Misri.  Akiwa Misri, alijadiliana na wasomi na wanazuoni na kufanya mihadhara na kuandaa vikao vya elimu kwa vijana. Pia alikutana na mkuu wa serikali ya Misri na kuweza kupata uungaji mkono wake. Wakati wa kukaa kwake kwa miaka 9 nchini Misri, Seyyed Jamal al-Din alifanya mabadiliko makubwa ya kitamaduni, kisiasa na kijamii katika nchi hiyo.

 

Seyyed Jamal alikuwa na wanafunzi wengi nchini Misri, lakini mmoja wao aliyeitwa "Mohammed Abdu baadaye akawa mmoja wa wanafunzi wakubwa wa shule yake na kuendeleza njia na fikra zake huko Misri. Muhammad Abdu ni mwanasheria, fakihi na Mufti wa zamani wa Misri, ambaye mawazo na fikra zake, baadaye zilipelekkea kuundwa kwa Harakati ya Ikhwan al-Musmiin (Muslim Brotherhood). Harakati hii iliibuka kwa ajili ya kuleta mageuzi katika jamii ya Kiislamu. Mnamo mwaka 1296 Hijria wakati Seyyed Jamaluddin alipoingia India kwa mara ya tatu, kutokana na shinikizo la serikali ya kikoloni ya Uingereza, ilimbidi aendelee na shughuli zake kwa siri. Kwa ajili hiyo, alianzisha jumuiya ya siri iitwayo "Urwa", ambayo baadaye ililea shakhsia muhimu kama Muhammad Iqbal Lahori, mwanafikra, mshairi na mwanasiasa kutoka Kashmir na Muhammad Ali Jinnah, ambaye kiongozi wa harakati za uhuru na mwanzilishi wa Pakistan. Safari zake hazikuishia katika nchi za Kiislamu pekee, bali pia alisafiri hadi Uingereza na Russia na kujadiliana na kufanya mdahalo na wanazuoni na wasomi kutoka nchi za Ulaya. Mijadala ambayo iliwafanya watu kama Ernest Renan, mwanafalsafa na mwanahistoria wa Ufaransa, kutambua makosa yao kuhusu Uislamu na kuacha kuuchukia. Katika miaka ya mwisho ya maisha yake, Sayyid Jamaluddin Asadabadi alipokea barua kutoka kwa "Sultan Abd al-Hamid", mfalme wa utawala wa Othmania, ambaye alimuita kufanya mageuzi katika serikali ya Kiislamu. Seyyed, ambaye maisha yake yote alifikiria juu ya kuunda na kuimarisha "Kambi ya Umoja wa Kiislamu" dhidi ya ukoloni wa Magharibi, aliitikia vyema mwaliko huu na akaingia katikati makao ya utawala wa Othmania mnamo 1310 Hijria. Miaka minne baadaye, wakati Sultan Abd al-Hamid alipotambua kwamba alipaswa kutoa mhanga kiti chake cha utawala ili kutimiza azma ya Jamaluddin Asadaabadi, aliacha kumuunga mkono.

Hatimaye, baada ya miaka sitini ya juhudi mtawalia na zenye matunda, Seyyed Jamaluddin Asadabadi aliaga dunia mwaka wa 1314 Hijria. Baadhi wanaamini kwamba aliuawa shahidi kwa amri ya mfalme wa utawala wa Othmania. Mwili wa Seyyed Jamaluddin ulizikwa kwa mara ya kwanza huko Istanbul, lakini baadaye, kwa ombi la mfalme wa Afghanistan, mwili wake ulihamishwa na kupelekwa Afghanistan, na ukazikwa katika Chuo Kikuu cha Kabul. Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili, umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo, siku na wasaa kama wa leo.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Tags