Oct 12, 2023 02:30 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 12 Oktoba, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 26 Rabiul Awwal 1445 Hijria inayosadifiia na tarehe 12 Oktoba mwaka 2023.

Leo tarehe 20 mwezi wa Mehr kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, inasadifiana na maadhimisho ya kumuenzi Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, mshairi na malenga mkubwa wa Kiirani.

Hafiz alizaliwa mwaka 727 Hijiria Shamsia huko Shiraz moja kati ya miji ya kusini mwa Iran. Alikuwa mtaalamu wa tafsiri ya Qur'ani, falsafa na fasihi ya Kiarabu na alipata umashuhuri kwa jina la Hafiz kutokana na kuhifadhi kwake Qur'ani Tukufu kwa visomo tofauti.

Mbali na elimu hizo, Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, alikuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan. 

Siku kama ya leo miaka 1101 iliyopita yaani tarehe 26 Rabiul Awwal mwaka 344 Hijiria alifariki dunia Ibn Sammak, mtaalamu mkubwa wa masuala ya itikadi ya Kiislamu huko Baghdad.

Historia haijaweka wazi tarehe na mahala alipozaliwa msomi huyo, lakini ripoti zinasema kwamba aliishi mjini Baghdadi, Iraq na kupata elimu na maarifa kwa wasomi wa mji huo. Vilevile historia inasema Ibn Sammak alilea wasomi wengine mashuhuri akiwemo Haakim Nishaburi.

Miongoni mwa vitabu vya Ibn Sammak ni kile cha "al Aamali" na vitabu vingine kadhaa kuhusu fadhila na matukufu ya Ahlulbait wa Mtume Muhammad (saw). 

Tarehe 12 Oktoba miaka 531 iliyopita mvumbuzi na baharia wa Kitaliani, Christopher Columbus alivumbua bara la America.

Columbus alianza safari yake ya baharini kwa kutumia merikebu tarehe 3 Agosti mwaka 1492 kutoka kwenywe bandari ya Palos nchini Uhispania akielekea kwenye Bahari ya Atlantic.

Baharia huyo hakujua kwamba anaelekea bara America na kwa msingi huo tarehe 12 Oktoba 1492 na baada ya safari ya siku 70 baharini alipoona nchi kavu kwa mbali alidhani kuwa anakaribia Asia, kwa sababu alikua akiamini kwamba ardhi ina umbo la mviringo. Kwa msingi huo Christopher Columbus alivipa visiwa alivyokuwa amegundua jina la India ya Magharibi. 

Christopher Columbus

 

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani, alimu na msomi mkubwa wa Kiislamu.

Abul-Makaarim Zanjani alizaliwa mwaka 1255 Hijiria mjini Zanjani, kaskazini magharibi mwa Iran ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo ya hawza mjini hapo.

Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani alipata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Morteza Ansari. Aidha baada ya kufariki dunia baba yake, Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani alichukua jukumu la umarjaa wa masuala ya kidini na sheria za Kiislamu hususan mjini Zanjani.

Katika kipindi cha mapinduzi ya kikatiba, msomi huyo na kama walivyokuwa wasomi wengine, alisimama kupambana na udikteta wa wakati huo hapa nchini Iran. Vitabu vya 'Makhaarijur-Rahman' na 'Miftaahud-Dhafar' ni miongoni mwa athari za Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani.

Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani

Na tarehe 12 Oktoba miaka 24 iliyopita, Jenerali Parviz Musharraf, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Pakistan alifanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa wakati huo wa nchi hiyo Muhammad Nawaz Sharrif.

Baada ya mapinduzi hayo Musharraf ambaye alichukua madaraka ya rais wa nchi, alivifanyia mabadiliko baadhi ya vipengee vya katiba ya nchi hiyo na kuzidisha nguvu na uwezo wa rais. Hata hivyo kutokana na kuongezeka mashinikizo ya ndani na nje, Musharraf alisalimu amri mwezi Novemba 2007 na kuachia cheo cha Mkuu wa majeshi ya Pakistan.

Musharraf aliondoka kikamilifu madarakani mwezi Julai 2008, baada ya kushika kasi vyama vya upinzani ambavyo vilishinda uchaguzi wa rais.   

Jenerali Parviz Musharraf