Je, mashirikiano ya Iran na Afrika yataimarika vipi?
(last modified Thu, 12 Jun 2025 02:09:48 GMT )
Jun 12, 2025 02:09 UTC
  • Je, mashirikiano ya Iran na Afrika yataimarika vipi?

Katika kikao chao na Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, mabalozi wa Senegal na Sierra Leone wamesisitiza utayari wa nchi za Kiafrika kwa ajili ya kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na Iran.

Kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Katibu Mtendaji wa Kikao cha Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika kimesisitiza kuendelea kufanyika vikao vya pamoja kati ya pande mbili. Mabalozi wa Senegal na Sierra Leone pia waliwasilisha ripoti kuhusu uwezo wa kiuchumi wa bara hilo na kutoa wito wa kuimarishwa uhusiano kati ya sekta binafsi na za umma za pande mbili.

Wakati wa kufanyika kikao hicho, wawakilishi wa Afrika walisisitiza uwezo mkubwa wa bara hilo katika nyanja za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiteknolojia. Seyyed Mehdi Hosseini, Katibu Mtendaji wa Kikao cha Iran na Afrika pia aliwasilisha ripoti kuhusu maendeleo na mipango ya siku zijazo.

Kupanuliwa uhusiano wa Iran na Afrika ni moja ya sera kuu na za kimsingi ambazo zimekuwa zikifuatiliwa na viongozi wa Iran na nchi mbalimbali za Kiafrika hususan katika miaka ya hivi karibuni. Iran inaichukulia Afrika kuwa bara lenye uwezo usio na kikomo wa kiuchumi na kisiasa, jambo ambalo linaweza kuchangia pakubwa katika ukuaji na maendeleo baina ya pande mbili na pande kadhaa kupitia ushirikiano wa pande husika.

Ikiwa na idadi ya watu zaidi ya bilioni 1.4, Afrika ina moja ya idadi ya watu inayokua kwa kasi kubwa zaidi duniani. Zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa bara hili wako chini ya umri wa miaka 30. Idadi hii ya vijana, pamoja na rasilimali nyingi za asili na nishati, inaifanya Afrika kuwa moja ya masoko makubwa na ya kuaminika zaidi kimataifa.

Rais Pezeshkian wa Iran akizungumza katika kikao cha tatu cha Iran na Afrika mjini Tehran

Kwa upande mwingine, kutokana na uwepo wa kisiasa wa nchi za kikoloni za Magharibi katika bara hilo, nchi nyingi za Kiafrika zinasisitiza juu ya kujitawala, kupinga ukoloni, kutetea haki za wanyonge na kupinga kila aina ya ubaguzi wa rangi. Nchi hizi zimepitia enzi mpya ya mwamko wa kisiasa, hasa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita; hivyo, nyingi hazikubali tena uwepo wa nchi za Magharibi zenye siasa za hadaa na undumakuwili, kwani katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia Ufaransa ikifukuzwa katika nchi kadhaa za bara hilo, kama vile Mali, Niger na Burkina Faso.

Katika mazingira hayo, mshikamano wa kisiasa kati ya Iran na Afrika ni msingi thabiti wa kuundwa uhusiano mpya wa kisiasa kati ya Iran na nchi mbalimbali za bara hili. Kuhusiana na hilo, katika miaka ya hivi karibuni, safari za wajumbe mbalimbali wa kisiasa kati ya Iran na nchi za Kiafrika zimedhihirisha wazi sera na matakwa hayo ya pamoja.

Kwa upande mwingine, Iran na Afrika zina uwezo wa kupanua zaidi uhusiano wao wa kiuchumi na kibiashara kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Kwa kuwa na uwezo kama vile rasilimali watu walioelimika, teknolojia asilia na uzoefu katika maendeleo ya miundombinu, Iran inaweza kubuni na kutekeleza miradi ya kimkakati kwa ushirikiano wa nchi za Kiafrika. Katika miaka ya hivi karibuni, makampuni ya Iran yamekuwa na uzoefu wenye mafanikio katika bara la Asia na Amerika Kusini katika nyanja za ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme, mabwawa, barabara na njia za kusambaza umeme, ambapo uzoefu huu pia unaweza kuhamishiwa Afrika.

Katika sekta ya dawa na vifaa vya matibabu, dawa za kienyeji za Iran zinaweza kukidhi mahitaji ya sehemu kubwa ya masoko ya dawa za Kiafrika kutokana na ubora wake mzuri na bei nafuu. Katika tasnia ya chakula na kilimo, mbolea za kemikali zilizotengenezwa Iran, dawa za kuua wadudu na mashine za kilimo zinaweza kuongeza mazao ya kilimo katika nchi za Kiafrika, na katika sekta ya nishati ya mafuta, gesi na petrokemikali, uhamishaji wa maarifa katika uwanja huu na uuzaji wa bidhaa za petrokemikali, haswa katika nchi ambazo zina rasilimali za mafuta lakini hazina teknolojia ya kuyasafisha, zinaweza kuimarisha uhusiano katika nyanja hizo kwa maslahi ya pande mbili.

Kwa upande mwingine, nchi mbalimbali za Afrika pia zina kiu ya teknolojia, uwekezaji na ushirikiano wa kimaendeleo. Migodi ya dhahabu, urani, bauxite, na akiba kubwa ya mafuta na gesi bado haijatumika katika nchi nyingi za Afrika. Kuhusu suala hili, nchi kama Nigeria, Guinea, Angola, Senegal na Sierra Leone zimefungua milango yao kwa washirika wapya wa kimkakati kwa kutoa suhula na vifaa vya uwekezaji. Katika muktadha huu, Iran inaweza kuwa mshirika wa kuaminika wa maendeleo wa nchi za Kiafrika kwa kutumia fursa zake linganishi katika teknolojia ya gharama ya kati na ya chini, huduma za ushauri na mafunzo ya rasilimali watu.

Wawakilishi wa Afrika katika kikao hicho

Hata hivyo, licha ya fursa hizi zote, uhusiano wa kiuchumi wa Iran na Afrika pia una changamoto zake. Ukosefu wa mifumo thabiti ya kifedha, kutokuwepo mifumo tekelezi ya mikopo na ukosefu wa ofisi rasmi za biashara katika nchi nyingi za Afrika ni vikwazo vikubwa vya kuimarishwa mahusiano. Katika upande wa pili, baadhi ya makampuni ya Iran ambayo yameingia katika soko la Afrika yanalalamikia urasimu mgumu katika baadhi ya nchi na vilevile kutofahamu mazingira yao ya kiutamaduni na kiuchumi.

Hata hivyo kikao cha karibuni cha mabalozi wa Afrika na viongozi wa Iran kinadhihirisha wazi kwamba, pamoja na matatizo yote yaliyopo, lakini kuna nia thabiti ya kisiasa ya kupanua uhusiano.

Ingawa uhusiano kati ya Iran na Afrika bado uko mwanzoni mwa safari yake, mustakabali mzuri unaweza kutabiriwa kwa kutegemea manufaa ya pande mbili, mtazamo wa muda mrefu na kubuniwa mikakati thabiti ya kiuchumi. Mahusiano haya yanaweza kufikia kiwango cha ushirikiano wa kimkakati ambao sio tu unafaidi pande zote mbili, bali pia kutumika kama mfano mzuri wa maingiliano ya Kusini-Kusini katika mfumo wa kimataifa. Kufikiwa lengo hilo bila shaka kunahitajia azma ya kitaifa, ya sekta binafsi na kuendelea kuungwa mkono suala hili na serikali husika.