Akhamisi, 12 Juni, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Mfunguo Tatu Dhulhija 1446 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 12 Juni 2025.
Tarehe 12 Juni miaka 485 iliyopita nchi ya Chile iliyoko magharibi mwa Amerika ya Kusini ilitekwa na wakoloni wa Hispania.
Kabla ya hapo Wahindi Wekundu wa Chile walikuwa wamevunja hujuma na mashambulio kadhaa ya Wahispania waliokusudia kuteka na kukalia kwa mabavu ardhi yao.
Hata hivyo, hata baada ya kutekwa nchi yao, Wahindi Wekundu hao waliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni hadi pale José Francisco de San Martín jenerali wa Argentina alipowasili mwaka 1817 na kuanzisha mashambulio ya kuzikomboa nchi zote zilizokuwa chini ya ukoloni wa Hispania Kusini mwa Amerika, ikiwemo Chile. Kwa msingi huo, Chile akakombolewa na kutangaza uhuru wake mwaka 1818.

Katika siku kama ya leo miaka 111, kwa mara ya kwanza kabisa yalifanyika majaribio ya kutumia nishati ya joto la jua pambizoni mwa Cairo, mji mkuu wa Misri.
Mbunifu na mtekelezaji wa mpango huo alikuwa mwanafizikia wa Kijerumani, ambaye aliweza kukusanya miale ya jua na kufanikiwa kuwasha mashine ya mvuke yenye kutumia 'horse power' 50.

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, Muhammad Hussein Fadhil Toni, msomi na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia katika mji wa Tehran Iran.
Alizaliwa 1257 Hijria Shamsia huko Ferdows kaskazini mashariki mwa Iran. Katika kipindi cha kutafuta elimu, Toni alihudhuria darsa na masomo ya waliimu mahiri wa zama zake.
Fadhil Toni alikuwa mahiri zaidi katika elimu kama za Fiq'h, hisabati, nujumu, fasihi, irfan na kadhalika.
Tarehe Juni 12, 1975, Mahakama Kuu ya Allahabad ilimpata Waziri Mkuu wa India, Indira Gandhi, na hatia ya kufanya udanganyifu katika uchaguzi na kumzuia kushikilia wadhifa wake kwa miaka sita.
Hata hivyo Indira Gandhi alipinga miito iliyomtaka ajiuzulu na akatangaza sheria za kijeshi kote nchini India baada ya maandamano makubwa ya wananchi yaliyotishia kuiondoa madarakani serikali yake. *****
Miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo, Rasul Montazeri mwanadiplomasia wa Iran alikuwa akifanya kazi katika ubalozi wa Iran mjini Zagreb mji mkuu wa Croatia aliuawa shahidi na wanamgambo wa Croatia.
Mwanadiplomasia huyo aliuawa shahidi wakati akitekeleza jukumu la kupeleka misaada ya Iran kwa Waislamu Bosnia Herzegovina waliokuwa wahanga wa vitendo na hatua za kibaguzi za Waserbia.
Na leo, tarehe 12 Juni ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo.
Siku ya Kimataifa dhidi ya Ajira kwa Watoto ilipendekezwa kwa mara ya kwanza mwaka 2002 na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa lengo la kuongeza uelewa na kuimarisha juhudi za kimataifa za kuzuia ajira ya watoto.
Siku hii ni jukwaa la serikali, taasisi na mashirika ya kiraia kujumuika pamoja ili kuchunguza tatizo la utumikishwaji wa watoto na kutafuta suluhisho lake.
Kwa takwimu za ILO, mamia ya mamilioni ya watoto wanafanya kazi duniani kote, wengi wao wakiwa katika mazingira hatarishi, utumwa, usafirishaji haramu wa binadamu na aina nyinginezo za unyonyaji, na wananyimwa haki za msingi kama vile elimu na afya.
