Nov 06, 2023 06:58 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Nov 6

Mkunsayiko wa baadhi ya matukio makubwa ya spoti duniani ndani ya siku saba zilizopita.....

Raga: Iran yaweka historia

Timu ya taifa ya raga ya wanawake ya Iran imeingia kwenye madaftari ya historia baada ya kuibuka mshindi wa tatu kwenye mashindano ya kieneo ya mchezo huo. Iran imeibuka ya tatu na kutunukiwa medali ya shaba baada ya kuigaragaza Guam alama 10-0 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kwenye mashindano hayo ya kieneo ya wachezaji saba kila upande yaliyofanyika Doha, mji mkuu wa Qatar. Katika mechi ya kwanza na pili kwenye hatua ya makundi, Iran iliisasambua Uzbekistan 31-12 kabla ya kuwashukia wenyeji Qatar na kuwazaba 22-0. Licha ya kutandikwa 17-0 na Umoja wa Falme za Kiarabu katika mchuano mwingine wa Kundi B, lakini akina dada hao wa Iran walifanikiwa kutinga hatua ya hatua ya nusu fainali.

Hii ni mara ya kwanza katika historia kwa timu ya taifa ya raga ya wanawake ya Jamhuri ya Kiislamu kushinda medali katika mashindano ya kibara kwenye mchezo huo.

Imarati imeibuka kidedea huku nafasi ya pili ikitwaliwa na India. Thailand imeubuka mshindi kwenye safu ya wanaume kwenye mashindano hayo baada ya kuichabanga Bahrain katika fainali. Timu ya wanaume ya raga ya Iran imejikuta katika nafasi ya tisa kwenye mashindano hayo ya kieneo Doha.

Ligi ya Soka Afrika

Klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco wanatazamiwa kutawazwa mabingwa wa mashindano mapya ya kibara ya Ligi ya Kandanda ya Afrika (African Football League) wiki ijayo. Hii ni baada ya kuichabanga Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini mabao 2-1 katika mkondo wa kwanza wa mchezo wa fainali uliopigwa Jumapili. Mabao ya Waarabu kwenye mchuano huo uliopigwa mjini Casablanca yalifungwa na Annas Serhat huku Rivaldo Coetzee akijifunga la kisigino. Waafrika Kusini walipata la kufutia machozi kupitia mkwaju wa penati lililofungwa na Abdelmounaim.

Miamba ya soka ya Afrika Kusini, klabu ya Mamelodi Sundowns ilitinga fainali ya Ligi ya Kandanda ya Afrika (African Football League) baada ya kuigaragaza klabu ya Al Ahly ya Misri kwa jumla ya goli 1-0 baada ya mchezo wa pili baina ya timu hizo kumalizika kwa matokeo ya 0-0 jijini Cairo.

Mamelodi ilitinga fainali dhidi ya Wydad Casablanca baada ya timu hiyo ya Morocco kuiondosha Esperance de Tunis ya Tunisia kwa mabao 5-4 kwenye upigaji matuta, baada ya matokeo ya jumla kuwa 1-1 kwenye nusu fainali.

Debi Kariakoo Jumapili

Siku ya Jumapili, watani wa jadi, klabu za Simba na Yanga zilishuka dimbaani kutoana jasho katika mchuano maarufu wa debi la Kariakoo, ambapo Simba badala ya kunguruma, walisikika wakitoa mlio wa paka eti. Wekundu wa Msimbazi walilishwa kichapo cha mbwa kungia Msikitini, kwa kugaragazwa mabao 5-1 na Wananchi katika mchuano uliopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jiji Dar es Salaam.

Mabao ya Yanga kwenye mchuano huo wa ndovu kumla mwanawe yalifungwa Kennedy Musonda, Max Nzengeli mawili, Aziz Ki, na Pacome Zouzoua, huku la kufutia machozi la Simba likitiwa kimyani na Kibu Dennis.

Ushindi huo wa Yanga umevunja rekodi ya Simba ya kutopoteza mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Bara, tangu vijana wa Msimbazo waanze kutiliwa makali na mkufunzi Robert Oliviera (Robertinho) raia wa Brazil. Huo ulikuwa mchezo wa 111 kwa watani hao kukutana katika Ligi Kuu ya Soka Bara.

Yanga imeshinda mara 39 na kutoa sare 40, huku Simba ikibeba ushindi mara 32. Young Africans wametuama kileleni mwa jedali la Ligi Kuu ya Soka Bara kwa alama 21, mbele ya Azam wenye pointi 19, huku Wana Msimbazi wakifunga orodha ya tatu bora kwa alama 18.

Dondoo za Hapa na Pale

Ulimwengu wa Kiislamu umeendelea kukosoa hatua ya klabu ya sokla ya Mainz 05 ya Ujerumani kuvunja mkataba na nyota wake, Anwar El Ghazi, kutokana na misimamo yake ya kuwatetea wanananchi madhulumu wa Palestina na kulaani jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza. El Ghazi mwenye umri wa miaka 28 amesema kuwa hajutii kwa kuchapish posti za kuwatetea Wapalestina. Kijana huyo wemney asili ya Morocco ameandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii kuwa: Sijutii msimamo wangu. Sijajitenga na yale niliyoyasema na msimamo wangu. Nitaendelea kusimama na ubinadamu na wanaodhulumiwa hadi nitakapovuta pumzi yangu ya mwisho.

Mwanakandanda huyo maarufu ambaye amewahi kuzichezea klabu za Aston Villa, Ajax na PSG amesema: Hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha mauaji ya watoto zaidi ya 3,500 huko Gaza ndani ya wiki tatu zilizopita. Mimi na sisi kama dunia hatuwezi kuendelea kunyamaza kimya. Lazima tutoe mwito wa kusimamisha mauaji Gaza saa hivi.

Maandamano ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina yamefanyika katika kona tofauti za dunia

Mchezaji huyo ambaye alikuwa anakipiga katika Ligi ya Soka ya Bundesliga amesema hajali kupoteza chanzo cha riziki yake, na kwamba kile ambacho hakivumiliki ni ukatili wanaofanyiwa wanananchi wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.

Wachezaji wengi mashuhuri Waislamu na Waarabu wameendelea kutumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kulaani jinai na mashambulizi ya kutisha ya Wapalestina huko Gaza.

Katika hatua nyingine, mwanariadha nyota wa Kenya, Hellen Obiri siku ya Jumapili ilishinda mbio za New York Marathon nchini Marekani kwa kutumia saa 2, dakika 27 na sekunde 23, ikifuatiwa na Muethiopia Letensebet Gidey huku nafasi ya tatu ikitwaliwa na bingwa mtetezi Sharon Lokedi.

Mbali na hayo, mchezaji nyota wa Inter Miami na timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi amefanikiwa kumshinda Erling Halaand wa Manchester City na kushinda tuzo yake ya nane ya Mchezaji bora wa Dunia ya Ballon d’Or. Messi amewahi kutwaa Ballon d’Or katika miaka 2009, 2010, 2011, 2012, 2015, 2019 na 2021.

Naye mshambuliaji wa Manchester City na Norway, Erling Haaland ameshinda tuzo ya 'Gerd Muller Trophy' kama mshambuliaji Bora wa mwaka 2023 kwenye sherehe za tuzo za Ballon d'or huko nchini Ufaransa. Aidha klabu ya Man City imeshinda tuzo ya Klabu Bora ya mwaka katika usiku wa tuzo za Ballon d’Or. Man City walikuwa na msimu bora sana kwa kufanikiwa kutwaa mataji matatu (treble) ambayo ni mataji ya Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza EPL, Champions League na Kombe la FA.

Lionel Messi

Wakati huohuo, mchezaji nyota wa klabu ya soka ya al-Hilal ya Saudi Arabia ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka barani Asia. Shirikisho la Soka Asia AFC, lilimteua Salim Shafi Muhammad al-Dawsari kuwa mchezaji bora zaidi wa soka barani Asia kwa upande wa wanaume, huku Sam Kerr wa Australia akitwaa taji hilo kwa upande wa wanawake.

Na Mashetani wekundu wa Manchester United walishuhudia masaibu yao yakiongezeka Jumatano baada ya kubanduliwa pamoja na wanabunduki wa Arsenal katika raundi ya 16-bora ya Kombe la Carabao. Siku chache baada ya kukung’utwa mabao 3-0 na majirani Manchester City kwenye Ligi Kuu, United, ambayo iliyokuwa ikitetea taji la Carabao, ilidungwa tena dozi sawa na hiyo na Newcastle kupitia mabao ya Miguel Almiron, Lewis Hall na Joe Willock ugani Old Trafford. Kilikuwa kisasi kitamu kwa Newcastle dhidi ya United baada ya kupondwa 2-0 katika fainali ya Carabao ugani Wembley mwezi Februari. Ni mara ya kwanza United kupoteza mechi nane ama zaidi katika 15 za kwanza tangu msimu 1962/63. Jijini London, Arsenal walipata bao la kujifariji dakika ya mwisho kupitia kwa Martin Odegaard wakilimwa 3-1 na wenyeji West Ham.

Mbali na Newcastle na West Ham, Liverpool, Chelsea, Fulham na Everton pia zilijikatia tiketi kushiriki robo-fainali. Droo ya robo-fainali: Chelsea v Newcastle, Port Vale v Middlesbrough, Liverpool v West Ham, na Everton v Fulham.

………………TAMATI………….