Nov 13, 2023 06:17 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Nov 13

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kuanzia Asia, Afrika hadi bara Ulaya

Iran bingwa wa IFCPF 2023

Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Soka ya Wenye Utindio wa Ubongo (Cerebral Palsy) ya eneo la Asia Oceania. Hii ni baada ya kuigaragaza Australia mabao 2-0 katika mchuano wa fainali ya mashindano hayo ya kieneo uliopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Home of Matildas mjini Melbourne. Mabao ya Moslem Mehrabian na Abbas Torabi yalitosha kuipa ushindi Iran kwenye mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka ya Wenye Utindio wa Ubongo (IFCPF).

Timu ya Soka ya Wenye Utindio wa Ubongo ya Iran uwanjani

Iran ilitinga fainali baada ya kuzisasambua Japan (3-0), Australia (3-1), Thailand (5-0) na India (6-0). Jamhuri ya Kiislamu imetunukuliwa medali ya dhahabu kwa ushindi huo, huku mwenyeji Australia ikitwaa medali ya fedha. Mapema siku hiyo, Japan iliitandika Thailand mabao 3-0 katika mchuano wa kutafuta mshindi wa tatu na kuzawadiwa medali ya shaba.

Soka U-17; Iran yainyuka Brazil

Timu ya taifa ya soka ya vijana ya Iran ilitoka nyuma na kuwashindwa mabingwa watetezi, Brazil mabao 3-2 katika mchuano wa Kundi C kwenye fainali za Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani FIFA kwa vijana wenye chini ya miaka 17. Brazil walitangulia kuona lango la Iran kunako dakika ya 28 kwenye mchuano huo uliopigwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Jakarta, nchini Indonesia, huku Abdolfazl Zamani akijifunga la kisigino katika dakika za majeruhi kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza.

Vijana wa Iran walitoana jasho na Brazil

Mabarobaro wa Iran walirejea kwa kasi isiyo ya kawaida katika kipindi cha pili, ambapo Yaqoub Barajeh aliifungia Jamhuri ya Kiislamu la kwanza katika dakika ya 54 ya mchezo, kabla ya Kasra Taheri kufanya mambo kuwa sawa bin sawa kunako dakika ya 69. Dakika nne baadaye, Esmaeil Gholizadeh aliwapa vijana wa Iran la kiufundi la ushindi.

Kabla ya hapo, mchezo mwingine wa Kundi C ulishuhudia Uingereza ikiinyoa kwa chupa New Caledonia kwa kuicharaza mabao 10-0. Vijana wa Iran wanatazamiwa kuvaana na Waingereza hao Jumanne, kabla ya kushuka dimbani kutoana udhia na New Caledonia siku ya Ijumaa.   

Ligi ya Soka Afrika; Sundowns watwaa ubingwa

Nani zaidi? Klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini imetwaa ubingwa wa Kombe la Ligi ya Kandanda ya Afrika baada ya kuicharaza Wydad Casablanca jumla wa mabao 3-2 kwenye fainali ya mkondo wa pili iliyopigwa Jumapili hii ya Novemba 12. Fainali ya kwanza iliishuhudia Wydad ikishinda mabao 2-1 nyumbani katika Uwanja wa Mohamed V, Morocco, kabla ya Sundowns kushinda mabao 2-0 wakiwa nyumbani pia katika Uwanja wa Loftus Versfeld, mjini Pretoria.

Sundowns mabingwa

Mabao ya Sundowns kwenye fainali hiyo ya kukata na shoka yalifungwa na Peter Shalulile kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza na Aubrey Modibe kunako dakika ya 53.  Waafrika Kusini hao wameandika historia kuwa klabu ya kwanza kutwaa kombe jipya la African Football League.

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Kandanda Afrika CAF, Patrice Motsepe ni miongoni mwa shakhsia watajika waliokuwa uwanjani mjini Pretoria kushuhudia fainali hiyo. Klabu ya Mamelodi imeondoka na kitita cha Dola za Kimarekani Milioni 4 kwa ushindi huo.

Soka la Wanawake Afrika

Klabu ya JKT Queens ya Tanzania siku ya Jumamosi ilishindwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa upande wa wanawake. Hii ni baada ya akina dada hao wa Tanzania kuchezea mkong'oto na kutandikwa mabao 4-1 katika mchezo wake wa mwisho wa hatua ya makundi kwenye michuano ya CAF Women Champions League dhidi ya Sporting Club Casablanca ya Morocco. Mabanati hao wa Kiarabu waling'ara katika mchezo huo wa aina yake uliopigwa katika Uwanja wa Laurent Pokou mjini San Pedro nchini Ivory Coast, na kujikatia tiketi ya kushiriki nusu fainali ya mashindano hayo ya kibara.

JKT ambao ni mabingwa wa ukanda wa CECAFA wamefungasha virago wakiwa na alama tatu katika michezo miwili waliyocheza huko nchini Kodivaa, kwa kuwa walihitaji ushindi au sare ili kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Lakini ndio hivyo tena, haikuwa rizki! Katika Kundi A, Mamelodi Sondowns Ladies wa Afrika Kusini wanaongoza wakiwa na alama sita, huku Athletico Abidjan ikiwa na alama moja. Sporting Casablanca imemaliza hatua ya makundi kwa alama 4.

Katika mechi nyingine, Mamelodi Sundowns walivaana na wenyeji Athletic Club Abidjan na Kodivaa, ambapo Waafrika Kusini wamesogea mbele hadi nusu fainali kwa kupata ushindi japo hafifu wa goli 1-0.

Katika hatua nyingine, ndoto ya timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya 'Rising Starlets' ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa wachezaji wenye chini ya miaka 20 imefifia, baada ya kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Indomitable Lionesses ya Cameroon ugenini siku ya Jumamosi. Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya tatu ilichezwa katika uwanja wa Stade Ahmadou Ahidjo nchini Cameroon.

Kombe la Dunia litaandaliwa nchini Colombia kuanzia Agosti 31, 2024, hadi Septemba 22, 2024, na timu 24 zitapambana kwa tuzo kubwa kwenye jukwaa kubwa. Wakati huohuo, Queen Cranes wa Uganda pia hawakufanya vizuri Jumamosi walipovaana na Senegal mjini Dakar katika mchuano mwingine wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake. Hii ni baada ya kubamizwa bao 1-0 katika mchuano wa ugenini.

Dondoo za Hapa na Pale

Timu ya taifa ya raga ya wanawake ya Kenya maarufu kama 'Lionesses' imewararua na kuwatafuna mahasimu wao wa Uganda 'Lady Cranes' kwa pointi 87-3 katika fainali ya Kombe la Elgon uwanjani Jomo Kenyatta jijini Kisumu na kuhifadhi ubingwa. Lionesses wanaonolewa na kocha Dennis Mwanja anayesaidiwa na Paul Murunga, wamenyakua taji hilo lao la saba la kipute hicho kwa ushindi huo. Wenzao wa kiume pia hawakuachwa nyuma, waliigaragaza Uganda alama 20-13 na kutwaa ubingwa katika uwanja huo huo wa Jomo Kenyatta jijini Kisumu wikendi.

Katika hatua nyingine, mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ghana 'Black Stars' Raphael Dwamena amefariki dunia baada ya kuanguka uwanjani wikendi wakati wa mechi kati ya timu yake ya Egnatia Rrogozhine ya nchini Albania dhidi ya Partizani. Mtandao wa soka wa Citi Sport umeripoti kuwa, habari za kifo chake zimekuja baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 kupata mshtuko wa moyo dakika ya 23 ya mchezo na kusababisha kusimamishwa kwa mchezo huo. Dwamena aligundulika kuwa na tatizo la moyo mwaka 2017, ambapo alifanyiwa upasuaji na kuwekewa kifaa cha kurekebisha mapigo ya moyo 'pacemaker' mwaka 2020.

Na katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, klabu ya Arsenal wikendi iliichabanga Burnley mabao 3-1 nyumbani Emirates, ambapo Leandro Trossard alifunga lake la 1,000 katika mechi hiyo ya aina yake. William Saliba na Alex Zinchenko walilizamisha kabisa jahazi la wageni na kuwahakikishia wenyeji alamu tatu muhimu. Aidha Mashetani Wekundu waliambulia ushindi laini wa goli moja bila jibu waliposhuka dimbani kutoana udhia na Luton Town. Bao la pekee na la ushindi wa Manchester United nyumbani Old Trafford lilifungwa na Victor Lindelof.

Wakati huohuo, Everton ilijizoazoa na kuitandika Crystal Palace mabao 3-2, wakati ambapo Bournemouth walikuwa wanaambulia ushindi mnono wa mabao 2-0 walipogaragazana na New Castle. Wolves pia walivuna alama tatu za nguvu kwa kuisasambua Tottenham mabao 2-1. Man City siku ya Jumapili walitoana jasho na Chelsea katika mchuano mwingine wa kufana, ulioshia kwa mibabe hiyo kutoshana nguvu kwa kufungana mabao 4-4.

Kwa matokeo hayo, City wanasalia kileleni mwa jedwali la EPL wakiwa na alama 28, mbele ya Liverpool na Gunners ambao kwa sasa wametosheka na pointi 27, wakifuatiwa na Tottenham wenye alama 26.

………………TAMATI………….