Nov 20, 2023 07:06 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Nov 20

Natumai hujambo mpenzi msikilizaji, na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika kona mbalimbali za dunia.

Voliboli ya Walemavu; Iran yashinda Kombe la Dunia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiye bingwa wa Kombe la Dunia kwenye fainali za Voliboli ya walemavu (kuketi chini). Iran iliibuka kidedea katika mchuano wa fainali siku ya Jumamosi, kwa kuicharaza Misri seti 3 za (25-21, 25-19, 25-17). Iran ilitinga fainali hiyo baada ya kuzitandika Japan 3-0, Algeria 3-0, Iraq 3-0 na Ukraine 3-0. Ujerumani pia iliibamiza Ukraine seti 3-2 kwa kutunukiwa medali ya shaba. Mechi hizo za Kombe la Dunia zimetumika kama mchujo, ili kuwatafuta watakaoshiriki Mashindano ya Paralimpiki ya Paris, yatakayofanyika nchini Ufaransa mwakani. Tayari Iran, mwenyeji Ufaransa, na Brazil zimejikatia tiketi za kushiriki michezo hiyo ya olimpiki ya walemavu ya Paris. Misri pia imepita kwa kuibuka wa pili.

Futsal ya Vipofu; Iran bingwa

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Futsal Duniani kwa wenye matatizo ya kuona. Iran ilibeba ubingwa huo Jumapili baada ya timu ya taifa ya futsal ya vipofu ya Jamhuri ya Kiislamu kuibamiza Sweden katika fainali ya aina yake iliyopigwa katika mji wa Nova Petrópolis nchini Brazil. Iran imeshinda kwa mabao 3-0 katika upigaji penati, baada ya timu hizo mbli kutoshana nguvu katika muda wa ada katika mchezo ulioshia kwa sare ya bao 1-1.

Image Caption

Japan iliichabanga Thailand mabao 3-2 katika mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu na kutunukiwa medali ya fedha. Mashindano hayo ya kimataifa yaliyofunga pazia Jumapili, yalianza Novemba 11.

Kombe la Dunia; Iran U-17 yatinga hatua ya muondoano

Timu ya taifa ya soka ya vijana ya Iran imemaliza ya tatu katika hatua ya makundi kwenye fainali za Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani FIFA kwa vijana wenye chini ya miaka 17. Iran imetinga hatua ya muondoano sasa kwa kumaliza mechi zake za Kundi C kwa alama 6. Iran imefanikiwa kusogea mbele kutokana na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa. Siku ya Ijumaa, mabarobaro hao wa Kiirani waliwabamiza New Caledonia mabao 5-0 katika mchuano wa mwisho wa makundi.

Iran U17

Kabla ya hapo, Iran iliisasambua Brazil mabao 3-2 katika mchuano wake wa ufunguzi, kabla ya kushindwa kwa mabao 2-1 na Uingereza. Fainali hizo za Kombe la Dunia kwa vijana wenye chini ya miaka 17 zinafanyika nchini Indonesia.

Mbio za Kombe la Dunia 2026; Iran yavuna

Timu ya taifa ya soka ya Iran imevuna ushindi mnono dhidi ya Hong Kong katika mchuano wa kusaka tiketi za kushiriki fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026. Iran ilipata ushindi wa mabao 4-0 ikitandazia gozi nyumbani katika Uwanja wa Azadi hapa jijini Tehran siku ya Alkhamisi.

Mabao ya Iran katika mchuano huo yalifungwa na mshabuliaji wa AS Roma, Sardar Azmoun, aliyefunga mawili, huku mawili mengine yakifungwa na nyota wa Porto, Mehdi Taremi na Ramin Rezaeian. Iran ambayo ipo katika Kundi E kwenye michuano hiyo ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026, inatazamiwa kwenda Tashkent Jumanne kuvaana na Uzbekistan, siku ambayo pia Hong Kong itaikaribisha nyumbani Turkmenistan, ambayo siku ya Alkhamisi ilichabangwa na Uzbekistan mabao 3-1.

 Soka Afrika

Karume Boys U-15 mabingwa wa Cecafa

Timu ya taifa ya soka ya vijana ya Zanzibar 'Karume Boys' imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la kieneo la CECAFA kwa vijana wenye chini ya miaka 15. Hii ni baada ya kuwachapa wenyeji wao Uganda mabao 4-3 kwenye mikwaju ya penalty baada ya dakika za ada kukosa kuamua mbivu na mbichi. Mabarobaro hao wa Kizenji walitoshana nguvu na Waganda katika dakika 90 za ada na nyongeza kwa kutandikana bao 1-1.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipeleka ndege nchini Uganda ili kuwarejesha nyumbani 'Karume Boys' kufuatia ushindi wao wa Kombe la CECAFA. Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mapokezi ya timu hiyo Ofisini kwake Migombani Zanzibar. Waziri Tabia ameeleza kuwa Rais Dk. Mwinyi tayari ametoa shilingi milioni 5 kufuatia ahadi aliyoitoa ya kununua kila goli la Karume Boys kwa shilingi Milioni moja hivyo ametoa kiasi hicho kutokana na magoli matano yaliyofungwa na timu hiyo katika fainali hiyo. Karume Boys walipokewa kwa vifijo, hoi na nderemo katika viwanja vya ndege vya Karume, na kutembezwa sehemu mbali mbali nchini na kuishia katika Mnara wa Kumbukumbu Kisonge.

Mbali na hayo, timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars siku ya Alkhamisi ilichapwa na Gabon mabao 2-1 kwenye mechi ya kwanza ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 katika uwanja wa Stade De Franceville katika jiji la Franceville nchini Gabon. Kiungo wa Red Star Belgrade, Kanga Guelor alifunga bao kutokana na shuti la mbali dakika ya 86 na kuwapa Panther alama zote tatu nyumbani katika mechi hiyo ya Kundi F. Kenya ilikuwa imefunga bao la kwanza kupitia Masud Juma dakika ya 40 lakini Gabon ikasawazisha dakika ya 60 kupitia kiungo Dennis Bounga anayesakata soka ya kulipwa Marekani.

Aidha siku ya Jumapili, Gabon hao walisafiri hadi Burundi na hakukuwa na cha mgeni njoo mwenyeji apone. Gabon iliichabanga Burundi mabao 2-1 katika mchuano mwingine wa Kundi F. Mabao ya wageni yalifungwa na Jim Allevina na Denis Bouanga huku la kufutia machozi la wenyeji likitiwa kimyani na Abedi Bigirimana dakika chache kabla ya kupulizwa kipyenga cha kumaliza mechi.

salah

Mo Salah

Katika hatua nyingine, Mohamed Salah alicheka na nyavu mara nne, walipoanza kampeni ya kufuzu Kombe la Dunia kwa ushindi uliotarajiwa dhidi ya wachovu Djibouti, huku Nigeria wakilazimishwa sare ya kushtukiza na Lesotho Alhamisi. Uchezaji wa Salah uliihakikishia Misri ushindi wa mabao 6-0 katika mechi yao ya ufunguzi ya Kundi A mjini Cairo huku mshambuliaji huyo akinyakua mabao manne ya kwanza na kuongeza jumla ya mabao yake kwa Misri hadi 53 katika mechi 93 huku wakitafuta nafasi ya kutinga fainali za 2026, wakiwa walikosa Kombe la Dunia la Qatar mwaka jana. Aidha wikendi, Misri iliishukia Sierra Leone na kuizaba 2-0.

Wakati huohuo, Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), wikendi katika Uwanja wa Grand Marrakech Annex1 waliitandika Niger bao moja la uchungu bila jibu katika mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu kombe la dunia 2026. Inaelekea kuwa hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa ndege ya kuwapeleka na kuwarejesha nyumbani vijana wa Stars kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa pili dhidi ya Morocco utakaopigwa Novemba 21 katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, ilizaa matunda na kuwafanya wacheze kwa ari. Bao la Tanzania katika mchezo huo dhidi ya vijana wa Afrika Magharibi lilifungwa na Charles M'mombwa kunako dakika ya 56.

Kwengineko Bafana Bafana wa Afrika Kusini waliwakung'uta mahasimu wao wa Benin mabao 2-1 katika mchezo wa Kundi C, wakati ambapo Ivory Coast ilikuwa inaidhalilisha Ushelisheli kwa kuizaba mabao 9-0 mjini Abidjan.

Soka Wanawake Afrika; Cameroon yaibandua Kenya U-20

Ndoto ya timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya 'Rising Starlets' ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 kufuzu kwa Kombe la Dunia imezimwa, baada ya kupoteza katika mchuano wa marudiano. Starlets walishindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani wa Nyayo jijini Nairobi na wakaishia kudhalilishwa kwa kuzabwa mabao 3-2. Akina dada hao wa Kenya walizabwa mabao 3-0 walipovaana na Indomitable Lionesses ya Cameroon ugenini Jumamosi ya wiki iliyopita, na hivyo wameondolea kwa jumla ya mabao 6-2. 

Wakati huohuo, Queen Cranes wa Uganda pia hawakufanya vizuri Jumamosi walipovaana na Senegal mjini Dakar katika mchuano mwingine wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake. Hii ni baada ya kubamizwa bao 1-0 katika mchuano wa ugenini. Kombe la Dunia litaandaliwa nchini Colombia kuanzia Agosti 31, 2024, hadi Septemba 22, 2024, na timu 24 zitapambana kwa tuzo kubwa kwenye jukwaa kubwa. 

Dondoo za Hapa na Pale

Australia imesema itatoa sehemu ya posho na ada zake za mechi kutoka kwenye mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Palestina katika Jiji la Kuwait mnamo Jumanne na kuelekeza kusimamia juhudi za kibinadamu huko Gaza. Mchango wa timu ya taifa ya soka ya Austalia 'Socceroos' utatolewa kupitia Wadhamini wa Wachezaji Soka wa Australia. Mchango huo utatolewa kwa shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam.

Jinai za Israel Gaza; Australia kuwapelekea misaada kupitia Oxfam

Mechi kati ya Palestina na Australia ilikuwa imepangwa kuchezwa katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu, lakini ikahamishia hadi Uwanja wa Kimataifa wa Jaber Al-Ahmad huko Kuwait City nchini Kuwait, kutokana na mashambulio ya kinyama ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Na timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya 'Shujaa' imetwaa ubingwa wa Safari 7s mwaka huu 2023 baada ya kuwafanyia vibaya vijana wa Samurai Baraccudas kwa kuwalima 19-0 jijini Nairobi. Kinara wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga na Waziri wa Michezo Ababu Namwamba walikuwa uwanjani kushuhudia mchuano huo wa kukata na shoka. Hata hivyo timu ya wanawake ya Kenya Lionesses ilishindwa kufurukuta mbele ya Uganda Lady Cranes katika finali kwa upande wa wanawake, na kuishia kuzabwa 15-13.

………………….MWISHO……………