Nov 27, 2023 05:56 UTC
  • Ulimwengi wa Spoti, Nov 27

Natumai u mzima wa afya popote pale uliopo mpenzi msikilizaji. Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia.

Unyanyuaji uzani; Iran bingwa

Rais Ebrahim Raisi wa Iran ameipongeza timu ya wanaume ya kunyanyua uzani mzito ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Mabingwa wa Dunia kwenye mchezo huo kwa mwaka huu 2023. Katika ujumbe wake wa tahania Ijumaa hii, Sayyid Raisi amesema anajifakharisha na timu hiyo ya vijana ya Iran kwa kuitoa kimasomaso Jamhuri ya Kiislamu na kuipasha katika ramani ya dunia. Aidha Rais wa Iran amewapongeza wananchi wa Iran kwa ushindi huo wa timu ya wanyanyua uzani mzito wa Iran huko Guadalajara, Mexico.

Rais Raisi wa Iran

 

Timu hiyo ya mabarobaro ya Iran iling'ara kwenye mashindano hayo na kuibuka kidedea kwa kuzoa medali 5 za dhahabu, 9 za fedha na moja ya shaba, na jumla ya alama 660. Hii ni mara ya tano kwa timu hiyo ya taifa ya vijana ya kunyanyua uzani mzito ya Iran kuibuka mshindi kwenye mashindano hayo ya kimataifa. Wanyanyuza uzani 229 kutoka nchi 44 duniani wameshiriki kwenye mashindano hayo ya kimataifa yaliyofanyika nchini Mexico baina ya Novemba 19 na 23.

Soka Iran; Melli yaambulia sare na Uzbekistan

Timu ya taifa ya soka ya Iran Jumanne iliyopita iliambulia sare ya mabao 2-2 ilipochuana na Uzbekistan katika mchuano wa Kundi E wa kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia 2026. Kwenye mchuano huo uliopigwa katika Uwanja wa Bunyodkor mjini Tashkent, Ramin Rezaeian aliwaweka kifua mbele wageni kunadako dakika ya 14 ya mchezo, kabla ya Mehdi Taremi kufanya mambo kuwa mawili kwa nunge kunako dakika ya 38. Hata hivyo wenyeji walijikusanya na kusawazisha katika kipindi cha pili. Matokeo hayo yanaashiria kuwa timu hizo mbili zimesogea mbele kwa hata inayofuata, kwenye kitimutimu cha Machi mwaka ujao 2024. Kabla ya hapo, Iran iliisasambua Hong Kong mabao 4-0 katika mchuano mwingine wa makundi siku ya Alkhamisi.

Katika hatua nyingine, timu ya taifa ya mabarobaro wa Iran imebanduliwa kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wenye chini ya miaka 17, baada ya kushindwa kufurukuta mbele wa Morocco katika mchuano wa raundi ya 16 uliopigwa Jumanne iliyopita. Vijana wa Kiajemi na Kiarabu walitoshana nguvu kwa kuzabana bao 1-1 katika dakika za ada za mchezo na kulazimika kuingia kwenye upigaji matatu. Hapa ndipo mbivu na mbichi ilipobainika, na Iran ikaondolewa kwenye fainali hizo kwa kupigwa mabao 4-1 kwenye penati.

Mbio za Kombe la Dunia 2026; Miamba ya Afrika yatikiswa

Timu za taifa za soka za Ghana, Cameroon, Senegal, Afrika Kusini na Zambia zimeingiwa na kiwewe katika mbio za kusakata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia la mwaka 2026. Hii ni baada ya timu hizo kupoteza alama muhimu katika mechi za raundi ya pili. Ghana, ambao wameshiriki Kombe la Dunia mara nne ikiwemo 2022 nchini Qatar, waliduwazwa na Comoros (Ngazija) kwa bao 1-0 jijini Moroni, Jumanne. Wanavisiwa wa Comoros wanaongoza Kundi I kwa alama sita wakifuatiwa na Mali (4), Madagascar (0), Ghana (3), Jamhuri ya Afrika ya Kati (1) na Chad (0). Afrika Kusini, ambao wameshiriki dimba hilo mara tatu na wanalenga kurejea katika jukwaa hilo baada ya kukosa duru tatu mfululizo, walinyamazishwa na Rwanda kwa kupepetwa mabao 2-0 mjini Butare. Rwanda wamekaa juu ya Kundi C kwa alama nne wakifuatiwa na Afrika Kusini (3), Nigeria, Lesotho na Zimbabwe (2) na Benin (1).

Kombe la Dunia

Mabingwa wa Afrika wa 2012, Zambia, pia walipata pigo walipokung’utwa mabao 2-1 na wenyeji Niger ugani Marrakech. Morocco wanaongoza Kundi E kwa alama tatu. Waliizaba Tanzania mabao 2-0 Jumanne iliyopita. Wako mbele ya Zambia, Niger na Tanzania kwa tofauti ya mabao, ingawa watatu hao wamesakata mechi mbili. Congo Brazzaville wako mkiani bila alama. Cameroon wanaofukuzia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tisa, waliponyoka na alama moja kwa sare ya 1-1 na wenyeji Libya mjini Benin. Indomitable Lions imo kileleni mwa Kundi D kwa alama nne, sawa na Cape Verde na Libya, nayo nambari tatu Angola ina pointi tatu. Mauritius na Eswatini zina pointi moja na sifuri mtawalia. Teranga Lions ya Senegal inaongoza Kundi B kwa alama nne. Mabingwa hao wa Afrika walitoka sare tasa dhidi ya Togo. Sudan pia wana alama nne baada ya kubwaga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bao 1-0 Jumapili. DR Congo wana alama tatu, Togo mbili nao Mauritania na Sudan Kusini moja kila moja. Harambee ya Stars ya Kenya Jumatatu iliyopita iliiadhibu Ushelisheli mabao 5-0 katika mchuano wa Kundi F wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia. Mabao ya vijana wa Kenya yalifungwa na Michael Olunga (2), Masoud Juma, Rooney Onyango na Benson Omala.

Cecafa U-18; Kenya yang'ara

Mashindano ya kimataifa ya soka kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati Cecafa kwa timu za wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18 yalianza wikendi ambapo mechi za Kundi ‘A’ zilichezewa Kisumu wakati zile za Kundi ‘B’ zikichezewa Kakamega. Timu ya taifa ya vijana wasiozidi umri wa mika 18 maarufu kama Kenya Junior Stars ilianza vyema mashindano ya Cecafa U-18 baada ya kupata ushindi mkubwa wa mabao 5-0 dhidi ya Sudan katika mechi iliyochezewa katika Uwanja wa Kenyatta mjini Kisumu, Jumamosi Novemba 25. Vijana hao chini ya ukufunzi wa kocha Salim Babu walikuwa juu kwa mabao 4-0 katika kipindi cha kwanza, kabla ya kuongeza jingine moja kupitia kwa Elly Owande katika kipindi cha pili. Mabao mengine ya Kenya yalifungwa na Louis Ingavi (2), Tyron Kariuki na Aldrine Kibet ambao licha ya kufunga mabao hayo, walicheza kwa kiwango cha juu. Katika mechi ya utangulizi uwanjani humo, Rwanda iliichapa Somalia bao 1-0, lakini Kenya Junior wanaongoza kundi hilo kutokana na ubora wa mabao. Washindi kutoka kila kundi watakutana na timu zitakazomaliza katika nafasi ya pili mjini Kisumu mnamo Disemba 5. Kenya iliyoanza mzoezi yake wiki iliyopita katika uwanja wa kimataifa wa MISC, Kasarani chini ya kocha Salim Babu na naibu wake Anthony Akhulia imepangiwa kuanza kampeni yake Jumamosi Novemba 25, 2023 kwa pambano dhidi ya Sudan Kusini mjini Kisumu kuanzia saa tisa. Kenya imepangiwa katika Kundi A linalojumuisha timu za Somalia, Rwanda, Sudan na Djibouti, wakati Kundi B likijumuisha timu za Tanzania, Zanzibar, Sudan Kusini na Uganda.

Yanga, Simba dhidi CR Belouizdad, Asec Mimosa

Klabu ya Yanga SC ya Tanzania wamekaribishwa kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa kuchezea kichapo cha magoli 3-0 kutoka kwa CR Belouizdad ya Algeria. Wananchi waliruhusu bao la kwanza dakika ya 10 lililofungwa na kiungo Abdelraouf Benguit, kabla ya dakika ya 45 kiungo Abderrahmane Meziane kufunga bao la pili na dakika ya 90 Lamine Jallow kufunga hesabu.

Kundi D linajumuisha timu za Al-Ahly, Yanga, Belouizdad na Medeama. Yanga itarudiana na timu hiyo baada ya kumaliza raundi ya kwanza ya michezo yote mitatu. Yanga wameingia hatua ya Makundi Klabu Bingwa Afrika msimu huu baada ya kupita miaka mingi kadhaa bila kucheza michuano hiyo mikubwa zaidi kwa levo ya klabu. Kwenye kundi lao, CR wanaongoza wakiwa na alama 3 huku ukisubiriwa mchezo kati ya Al Ahly na Medeama utakaopigwa kesho ili kutoa picha ya kundi lao baada ya mechi zao za kwanza.

Wakati huohuo, miamba ya kandanda nchini Tanzania, klabu ya Simba wikendi walitupa karata yao ya kwanza kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CAFCL) walipowaalika, Asec Mimosas ya Ivory Coast katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam na mchezo kuishia kwa sare ya bao 1-1. Simba ilitumia vyema dakika 45 za kwanza kupata bao la kuongoza mfungaji akiwa Said Ntibazonkiza 'Saido' dakika ya 44 kwa mkwaju wa penalti. Penalti hiyo ilitokana na beki wa ASEC kuunawa mpira wakati akitaka kuokoa shuti la mshambuliaji Kibu Denis. Bao hilo lilidumu kwa kipindi hicho na kuifanya Simba kutoka wakiwa na uongozi wa bao 1-0 huku pia wakiwadhibiti vizuri wapinzani wao. Hata hivyo Simba ingeweza kupata mabao ya kutosha lakini wachezaji wake wakashindwa kutulia kumalizia nafasi walizopata. Kipindi cha pili Simba ilirudi na kasi katika dakika 10 za kwanza kujaribu kutafuta bao la kuutanua uongozi wao lakini ASEC Ikawa makini kuwadhibiti ASEC ikaamka na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 77 mfungaji akiwa Serge Pokou akimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji William Sankara.

Dondoo za Hapa na Pale

Mwanariadha nyota na bingwa wa Olimpiki wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius aliachiliwa huru kwa msamaha Ijumaa, miaka 10 baada ya kumpiga risasi mchumba wake katika mauaji ambayo yaliitikisa dunia. Msemaji wa Idara ya Marekebisho, Singabakho Nxumalo alisema Pistorius ataachiliwa kutoka gerezani mnamo Januari 5. Pistorius, ambaye alitimiza umri wa miaka 37 wiki hii, amekuwa gerezani tangu mwishoni mwa 2014 kwa mauaji ya Siku ya Wapendanao 2013 ya mwanamitindo Reeva Steenkamp, ​​ingawa aliachiliwa kwa muda wa kifungo cha nyumbani mnamo 2015, huku moja ya rufaa nyingi katika kesi yake ikisikilizwa. Hatimaye alipatikana na hatia ya mauaji na kuhukumiwa kifungo cha miaka 13 na miezi mitano jela.

Mbali na hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza Mabaraza ya Michezo kuendelea kuratibu na kufuatilia utendaji wa vyama vya michezo na kuhakikisha vinaendeshwa na kujiendesha kwa manufaa ya taifa. Rais Samia amesema serikali inapoweka mazingira mazuri katika sekta ya michezo hutoa hamasa kwa wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo kwa kuwekeza katika timu za vijana.

Rais Samia

Rais Samia ametoa agizo hilo wikendi wakati wa hafla ya chakula cha mchana aliyoiandaa kuwapongeza wachezaji na viongozi wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15 (Karume Boys) iliyofanyika Ikulu ndogo ya Tunguu. Timu ya Karume Boys imetwaa Kombe la Mashindano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yaliyofanyika nchini Uganda ambapo tangu miaka ya 1990 Zanzibar haijawahi kushinda katika mashindano hayo.

Na mwanasiasa wa Ghana aliyemdhihaki Harry Maguire ameomuomba radhi nyota huyo wa Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza baada ya mchezo wake kuimarika ghafla. Mbunge Isaac Adongo alipata umaarufu mkubwa mwaka mmoja uliopita baada ya kutumia usogora wa Maguire kichocheo cha kushambulia wapinzani wake wa kisiasa wakati wa mjadala kuhusu uchumi bungeni.

…………………..TAMATI…………….