Dec 04, 2023 05:40 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Desemba 4

Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio makubwa ya spoti ndani ya siku saba zilizopita.....

Timu ya taifa ya mieleka ya kujiachia (freestyle) ya Iran imeibuka mshindi wa pili kwenye mashindano ya dunia ya wanajeshi ya mwaka huu 2023. Jamhuri ya Kiislamu ilimaliza ya pili kwenye mashindano hayo ya kimataifa yaliyoandaliwa na Baraza Kimataifa la Michezo ya Wanajeshi CISM siku ya Ijumaa, baada ya kuzoa medali 2 za dhahabu, 4 za fedha na moja ya shaba. Mwenyeji Azerbaijan imeibuka kidedea huku nafasi ya tatu ikitwaliwa na Uturuki. Mejeshi kutoka nchi 20 duniani yameshiriki kwenye mashindano hayo.

Taekwondo; Iran yachota medali 4

Timu ya taekwondo ya walemavu ya Iran imezoa medali nne za dhahabu kwenye mashindano ya kimataifa ya World Taekwondo Grand Prix mjini Manchester, Uingereza. Maryam Abdollahpour alitwaa medali ya dhahabu katika safu ya K44 kwa wanawake wenye kilo chini ya 47, kwa kumzidi ujuzi na maarifa hasimu wake kutoka Peru, Leonor Angelica Espinoza aliyemshinda kwa alama 15-5. Raia wa Mexico, Claudia Romero amezoa shaba. Katika kateogoria ya K44 kwa wanaume wenye kilo 70, Mahdi Pourrahnama alimshnda raia wa Uzbekistan, Javokhir Alikulov kwa pointi 17-10 kutunukiwa dhahabu. Alireza Bakht alimzidi kete Jeonghun Joo kutoka Korea Kusini kwa alama 29-18, kitendo cha K44 kwa wanaume wenye uzani usiozidi kilo 80.

 

Aidha Hamed Haghshenas aliipa Iran dhahbu nyingine katika safu ya K44 Men kwa wanaume wenye Zaidi ya 80, baada ya kumpeleka mchakamchaka Ivan Mikulic wa Croatia kwa kumtoa kwa pointi 17-2. Shirikisho la Taekwondo Duniani liliwalika wanamichezo 128 kutoka pembe tofauti za dunia, kushiriki kwenye mkondo wa mwisho wa GP series kwa mwaka huu 2023 katika Ukumbi wa Manchester Regional Arena. Wawakilishi hao wanne wa Iran mbali na kuzoa medali na kutunukiwa zawadi nyinginezo, lakini wamejikatia tiketi ya kushiriki Michezo ya Paralimpiki ya Paris mwaka ujao 2024.

Kombe la Dunia U17; Ujerumani bingwa

Kwa mara ya kwanza, Ujerumani imetwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa vijana wa kiume wenye chini ya umri wa miaka 17. Hii ni baada ya kuisasambua Ufaransa katika kitimutimu cha fainali iliyopigwa Jumamosi nchini Indonesia. Vijana haho wa Ulaya walipambana kufa kupona na kutoshana nguvu kwa kuzabana mabao 2-2 katika dakika za ada. Walilazimika kuingia kwenye upigaji matuta, na hapa ndipo mbivu na mbichi ikabanika, kwa mabarobaro wa Kijerumani kuibuka na ushindi wa magoli 4-3. Wameibuka kidedea licha ya kujikuta wakicheza wachezaji 10 uwanjani katika dakika 21 za mwisho, baada ya mchezaji wake, Winners Osawe kulishwa kadi ya pili ya njano.

Penati iliyotiwa wavuni na Paris Brunner katika kipindi cha kwanza iliwaweka kifua mbele Wajerumani wakicheza fainali kwka mara ya kwanza tokea mwaka 1985. Walizidi kukoleza ushindi wao kwa bao la nahodha Noah Darvich dakika sita baadaye. Hata hivyo Wafaransa walijikusanya na kusawazisha, na timu mbili hizo zikalazimika kungia kwenye upigaji matumat ili kumpata mshindi wa Kombe la Dunia kwa vijana wasiozidi miaka 17.

Mali ambayo ilimaliza ya pili katika Kombe la Dunia la mwaka 2015, iliichabanga miamba ya soka Argentina mabao 3-0 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu na kutunukiwa medali ya shaba katika duru ya mashindano hayo ya Shirikisho la Soka Dunia FIFA mwaka huu. Mabao ya vijana hao wa Afrika Magharibi kwenye mchezo huo wa Ijumaa yalifungwa na Ibrahim Diarra, Mamadou Doumbia na Hamidou Makalou.

Katika hatua nyingine, klabu ya Yanga ya Tanzania imeondoka na pointi moja baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Huo ulikuwa mchezo wa pili wa hatua ya makundi kwa Yanga iliyo Kundi D baada ya ule wa kwanza kupoteza jijini Algers, Algeria kwa mabao 3-0 kutoka kwa CR Belzoudad. Kwa matokeo hayo, Yanga inasalia nafasi ya nne kwenye msimamo na alama moja na ina kibarua kigumu kwenye kuwania kufuzu hatua ya robo fainali. Yanga yenye historia ya kufuzu hatua ya makundi ya ligi hiyo mara ya mwisho mwaka 1998, ilipata bao la kusawazisha dakika ya 91 lilifungwa na Kiungo Pacome Zouzoua baada ya lile la Al Ahly la dakika ya 87 lilifungwa na Percy Tau. Yanga haijapata ushindi mpaka sasa katika mechi mbili walizocheza na ina kibarua kizito kwani mechi inayofuata, ambapo watakutana na Medeama ambayo iliwafunga CR Belzoudad mabao 2-1. Kwa matokeo hayo, Al Ahly inaendelea kusalia kileleni ikiwa na alama nne, ikifuatiwa na Medeama yenye tatu sawa na Belzoudad na Yanga ya mwisho na pointi moja.

Wakati huohuo, Wekundu wa Msimbazi Simba SC, wamelazimishwa sare kwa mara nyingine ugenini Botswana dhidi ya Jwaneng Galaxy. Simba walifanikiwa kumiliki zaidi mpira na kupoteza nafasi nyingi zaidi za kufunga na hadi filimbi ya mwisho, Simba 0-0 Jwaneng. Hii ni sare ya pili kwa Simba ambapo awali alicheza na ASEC Mimosas katima dimba la Benjamini Mkapa jijini Dar. Simba sasa ana alama mbili katika kundi lao hilo linaloongozwa na Jwaneng Galaxy wenye alama nne. Jwaneng wao mchezo wa awali walikuwa ugenini dhidi ya Wydad Casablanca na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa 1-0.

Matokeo ya CECAFA U18

Timu ya taifa ya soka ya vijana ya Kenya 'Junior Stars' siku ya Jumanne itavaana na Tanzania katika nusu fainali ya Mashindano ya Kandanda ya kanda ya Afrika Mashariki na Kati Cecafa kwa vijana wenye chini ya miaka 18. Aidha nusu fainali nyingine itazikutanisha Rwanda na Uganda katika Uwanja wa Jomo Kenyatta mjini Kisumu, magharibi mwa Kenya. Tanzania imejatia tiketi ya nusu fainali baada ya kutoa sare ya bao 1-1 na Zanzibar katika Uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega, magharibi mwa Kenya wikendi.

Nembo za mashirikisho ya soka kanda ya Cecafa

Uganda ilisogea mbele baada ya kuikung'uta Sudan Kusini mabao 2-0 siku ya Jumamosi mjini Kisumu. Kipindi cha kwanza timu hizi zilishindwa kuona nyavu za mwenzake. Rwanda imemaliza ya pili kwenye Kundi A kwa alama 6, baada ya kusajili ushindi dhidi ya Somalia na Sudan na kisha kupoteza kwa mwenyeji Kenya ambayo inaongoza kundi hilo lwa alama 9. Wenyeji hao waliichapa Sudan, Rwanda na Somalia mabao 5-0, 1-0 na 4-1 kwa usanjari huo.

Dondoo za Hapa na Pale

Timu ya taifa ya kuogelea ya Tanzania imeshika nafasi ya pili katika mashindano ya 8 Kanda ya Tatu ya kuogolea yaliyofanyika Kigali, Rwanda katika viwanja vya michezo Gahanga na kushirikisha nchi 10. Uganda imeibuka kidedea kwenye mashindano hayo, huku Kenya ikifunga orodha ya 3 bora. Mwenyeji Rwanda imeibuka ya 4, Burundi (5), Afrika Kusini (6) Eswatini (7) Eritrea (8) Djibouti (9) huku Ethiopia ikivuta mkia.

Mbali na hayo, Shiriksho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limeondoa adhabu ya kutosajili kwa klabu ya Simba SC baada ya kukamilisha madai ya fedha ya usajili ya klabu ya Teungueth kuhusu usajili wa Pape Sakho. Awali, Simba ilifungiwa kusajili baada ya kushindwa kuilipa klabu hiyo kutokana na mauzo ya Sakho. Baada ya kukamilisha malipo hayo, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) pia limeifungulia Simba kusajili wachezaji wa ndani.

Ligi ya EPL

Na katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, bao la kichwa la dakika ya 90 la Dejan Kulusevski liliisaidia Tottenham kutoa droo ya mabao 3-3 walipovaana na Manchester City Jumapili katika Uwanja wa Etihad. Nahodha wa Spurs, Son Heung-min alijifunga na kisigino katika dakika ya 9 ya mchezo, dakika tatu tu baada ya kuiweka timu yake kifua mbele. Phil Phoden aliipa City la pili kunako dakika ya 31, kabla ya Giovanni Lo Celcso kuisawazishia Spurs katika dakika ya 69. Jack Grealish aliiweka City kifua mbele kunako dakika ya 81, kabla ya Kulesevkis kufanya ngoma kuishia kwa sare ya mabao 3-3. City imetoa sare kwenye mechi zake tatu zilizopita, na hivi sasa ipo katika nafasi ya tatu kwenye jedwali la EPL ikiwa na alama 3-, alama 3 nyumba na Wabeba Bundiki waliotuama kileleni kwa sasa. Arsenal hiyo ilivuna ushindi wa mabao 2-1 ilipovaana na Wolverhampton Wanderers siku ya Jumamosi nyumbani Emirates.

Kinda Bukayo Saka aliwaweka Gunners kifua mbele kwa bao lake la mapema, dakika 6 baada ya kupulizwa kipyenga cha kuonza ngoma, kabla ya nahodha, Martin Odegaard kuongeza jingine dakika saba baadaye. Bao la kufutia machozi la Wolves wanaonolewa na Gary O'Neil lilitiwa kimyani na Matheus Cunha katika dakika za lala salama.

Kwengineko, Burnley wamepata ushindi wa kwanza nyumbani msimu huu baada ya kuinyoa kwa chupa Sheffield United kwa kuichabanga mabao 5-0, Wakati ambapo Brentford iliikuwa ikivuna ushindi mnono wa mabao 3-1 walipotoana udhia na Luton Town.  Liverpool Jumapili walifunga mabao 2 ya dakika za lala salama yalyofungwa na Wataru Endo na Trent Alexander-Arnold walipotoana jasho na Fulham nyumbani Anfield na kupata ushindi mwembamba wa mabao 4-3. Wapo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL wakiwa na alama 31.

…………………MWISHO..………….