Dec 18, 2023 04:24 UTC
  • Jumatatu, 18 Disemba, 2023

Leo ni Jumatatu tarehe 4 Jamadithani 1445 Hijria sawa na tarehe 18 Disemba 2023.

Miaka 109 iliyopita katika siku kama ya leo, Uingereza iliikoloni rasmi Misri. Inafaa kukumbusha kwamba, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Othmania ulikuwa muitifaki wa madola yaliyokuwa yakiipinga Uingereza yaani Ujerumani na Austria. Uingereza nayo ikiwa na lengo la kukabiliana na kitendo hicho, iliikalia kwa mabavu Misri, ambayo hadi katika kipindi hicho ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Othmania. Harakati za ukombozi za wananchi wa Misri dhidi ya mkoloni Mwingereza zilizaa matunda mwaka 1922, ambapo nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake. *

Bendera ya Misri

Katika siku kama ya leo miaka 85 iliyopita msomi wa Ujerumani, Otto Hahn, alifanikiwa kupasua kiini cha atomu, hatua ambayo ilikuwa mwanzo wa zama za atomu. Mtaalamu huyo wa kemia alizaliwa mwaka 1879 huko Frankfurt na kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya kemia. Tangu wakati huo alijishughulisha na utafiti katika taaluma ya fizikia. Baada ya utafiti mkubwa na katika siku kama hii ya leo Otto Hahn alifanikiwa kupasua kiini cha atomu. Hatua hiyo iliibua nishati kubwa ambayo baadaye ilianza kutumika katika vinu na mabomu ya nyuklia. Mwaka 1944 Otto Hahn alitunikiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya kemia.

Otto Hahn

Tarehe 18 Disemba miaka 44 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake. Makubaliano hayo yana lengo la kuondoa dhulma zinazofanywa dhidi ya wanawake duniani. Hata hivyo makubaliano hayo, kama yalivyo mengine mengi ya kimataifa, yanatawaliwa na mitazamo ya kimaada ya Magharibi inayosisitiza usawa wa jinsia mbili za mwanamke na mwanaume katika kila kitu. Hii ni katika hali ambayo mwanamke na mwanaume wanatofautiana kimwili na kiroho. Kwa sababu hiyo dini za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu unasisitiza kuwa njia ya kuwakomboa wanawake ni kuwatayarishia mazingira ya uadilifu kwa kutilia maanani uwezo wao wa kimwili na kiroho.

Katika siku kama ya leo miaka 70 iliyopita Sayyid Mujtaba Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Sayyid Mujtaba Navvab Safavi