Araqchi: Iran itaendelea kurutubisha urani, kwa makubaliano au bila makubaliano
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema kuwa, Tehran bado haijaamua kama itashiriki katika duru ijayo ya mazungumzo ya nyuklia au la.
Sayyid Abbas Araqqchi amesisitiza kwamba urutubishaji wa madini ya urani utaendelea bila kujali makubaliano yoyote.
Msimamo wa hivi majuzi wa Iran unathibitisha msisitizo wake wa kutekelezwa haki zake kwa mujiibu wa Mkataba wa Kuzuiia Uzalishaji na Usambazajii wa Silaha za Nyuklia (NPT), haswa kurutubisha madini ya urani na kuondolewa vikwazo.
Mazungumzo kati ya Iran na Marekani, ingawa si ya moja kwa moja, yanaonekana kama njia inayoweza kuelekea kufufua mazungumzo yaliyokwama kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
"Tayari tumejibu madai ambayo hayana mashiko," Araghchi aliwaambia waandishi wa habari kando ya kumbukumbu ya kutiimia mwaka mmoja tangu kufa shahidi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian katika ajali ya helikopta mwaka jana akiwa pamoja na shahidi Ibrahim Raisi. "Kauli hizi zisizo za kawaida hazisaidii kuendeleza mazungumzo," amesisitiza Waziri wa Mashauuri ya Kigeni wa Iran.
Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yalianza mapema mwezi Aprili chini ya upatanishi wa Oman. Tangu wakati huo, pande hizo mbili zimefanya duru nne za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na kuondolewa kwa vikwazo.
Pande zote mbili zimeelezea mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja kama yenye mwelekeo chanya kwa ujumla.