Maswali yetu na Majibu ya Thaqalain (129)
Assalaama Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.
Swali la kipindi cha juma hili linasema: Je, tunatumia vipi aya ya Hakika walii wenu hasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini, ambao husimamisha Swala na hutoa Zaka wakiwa wamerukuu…… ambayo ni mashuhuri kwa jina la aya ya wilaya, kuthibitisha Uimamu wa Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) na tunajifunza nini kiitikadi kutokana na aya hii?
Tunatafuta kwa pamoja jibu la swali hili kutoka kwa vizito viwili, yaani Qur’ani Tukufu na Ahlul Bait wa Mtume (saw), karibuni.
***********
Aya ya wilaya ni aya ya 55 ya Surat al-Maida na aya nyingine inayofuata ya 56 ya zinasema: Hakika walii wenu hasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini, ambao husimamisha Swala na hutoa Zaka wakiwa wamerukuu.
Na atakayemtawalisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini, basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndio watakaoshinda.
Kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji Qur’ani Tukufu inatumia njia ya wazi kabisa na ya mabano kwa kutumia neno ‘hakika’ kubainisha kwamba wa kwanza kusimamia masuala ya viumbe ni Mwenyezi Mungu mwenyewe kisha Mtume wake (saw) na baada ya hapo kundi maalumu katika waumini. Mwenyezi Mungu amelitaja na kubainisha kundi hili kwa sifa maalumu kwa kusema kuwa ni lile la watu wanaotoa zaka hali ya kuwa wamerukuu na kufafanua kwa undani zaidi kwa kuendelea kusema kuwa ibada yao kwa Mola wao haiwazuii kuzingatia hali ya viumbe wake na kukidhi mahitaji yao.
Na wafasiri wote wanasema kuwa aya hii iliteremka katika tukio lililotokea katika Msikiti wa Mtume (saw) mjini Madina ambapo Amirul al-Mu’mineen Ali (as) alitoa sadaka pete yake na kumpa masikini hali ya kuwa amerukuu kwenye swala. Katika aya hii kuna ujumbe wa wazi na wa kina kwamba bendera na kiongozi wa kundi hilo la waumini ni Imam Ali al-Murtadha (as), Wasii wa Mtume Mtukufu (saw) ambaye ndiye anayestahiki kuchukua uongozi wa Umma wa Kiislamu- kwa amri ya Mwenyezi Mungu- baada ya kuondoka Mtume humu duniani. Wilaya hii pia inapasa kuwaendea wale watukufu waliokuwa kama yeye katika ukamilifu wa sifa (as), na hiyo ndio maana ya aya hii kuteremka kwa dhamiri ya wingi ambapo Mwenyezi Mungu anasema: …. ambao husimamisha Swala na hutoa Zaka wakiwa wamerukuu.
Katika aya hii kuna ishara ya wazi kwamba waliokusudiwa ni zaidi ya Imam Ali (as) na amabo wana sifa zinazofanana na zake (as). Watukufu hao walikwishaarifishwa na Mtume Mtukufu mwenyewe (saw) mbele ya Umma kwa kuwataja kuwa ni watoharifu na kwamba idadi yao ni kumi na wawili.
Kuhusu suala hili Imam Swadiq (as) anasema katika kufasiri aya hii katika hadithi iliyopokewa katika kitabu cha Usuul al-Kafi: ‘Na Mwenyezi Mungu akateremsha aya hii kumuhusu (yaani Ali (as)) na kuendeleza neema yake kwenye watoto wake ambapo kila mwanawe aliyefikia Uimamu alikuwa na neema hii kama alivyokuwa nayo yeye (Ali), wanatoa Zaka hali ya kuwa wamerukuu.’
************
Ndugu wasikilizaji, jambo muhimu kwenye aya hii ni kuashiria kwake moyo huu wa ikhlasi wa kuunganisha ibada ya Mweyezi Mungu na kutoa huduma kwa waja wake. Moyo huu ndio unaolifanya kundi hili maalumu la waumini waweze kupata fursa ya kupewa wilaya ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake Mtukufu (saw) juu ya wanadamu. Na kusudio si kubana ustahiki huu katika suala la kutoa zaka hali ya kuwa umerukuu. Imepokelewa katika Tafsiri ya Burhan kwamba sahaba mmoja alisema: ‘Wallahi nimetoa zaka pete arubaini hali ya kuwa nimerukuu ili niteremkiwe na aya kama ilivyofanyika kwa Ali bin Abi Talib lakini hakuna aya yoyote iliyoteremka.’
Ama maana ya wilaya aliyoijalia Mwenyezi Mungu kwa Maimamu wotoharifu katika aya tukufu hii iko wazi. Maana ya wilaya hiyo ni sawa na ile ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa watu, nayo ni wilaya ambayo inafungamana na Uimamu na ulazima wa kutii kama ilivyo dhahiri. Kuanza kutoa tafsiri nyingine kama zile zinazomaanisha nusura au mapenzi kwa mfano ni jambo la kujikalifisha ambalo linabatilishwa na aya hiyohiyo kama ambavyo aya inayofuata pia inalibatilisha kwa kusema bayana kwamba wilaya ni ya Mwenyezi Mungu, Mtume wake na kwa kundi hili maalumu la waumini, jambo ambalo linawaingiza waumini kwenye kundi la Mwenyezi Mungu lenye kushinda.
Na Hizbullah, yaani kundi la Mwenyezi Mungu, kwa maana ya Qur’ani ni waumini ambao imani yao imekamilika na kuthibiti wilaya yao kwa Mwenyezi Mungu na kujibari kwao na maadui wake. Na hili ndilo suala ambalo linaashiriwa na Qur’ani Tukufu katika aya ya 22 ya Surat al Mujadala ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Huwakuti watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza katika Mabustani yapitayo mito chini yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio Kundi la Mwenyezi Mungu. Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndio lenye kufaulu.
Na hili ndilo suala linalosisitizwa na hadithi tukufu ambapo tutaashiria baadhi yazo hivi punde, endeleeni kuwa nasi.
Imenukuliwa katika Tafsiri ya Kanz ad-Daqaid ya Abu Ja’far al-Baqir yaani Imam Baqir (as) kwamba kundi moja la Mayahudi lilisilimu akiwemo Abdallah bin Salam. Lilimjia Mtume (saw) na kumwambia: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika Musa (as) alimuusia Yusha’a bin Nun (Joshua), sasa ni nani wasii wako na walii wetu baada yako?
Hapo aya hii ikateremka: Hakika walii wenu hasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini, ambao husimamisha Swala na hutoa Zaka wakiwa wamerukuu.
Mtume (saw) akasema: Simameni……wakafika kwenye msikiti ambapo walimpata mwombaji akitoka nje. Mtume (saw) akamuuliza: Ewe Mwombaji! Hakuna yeyote aliyekupa kitu…? Mwombaji akajibu: Nam, pete hii….. Mtume (saw) akamuuliza: Je, ni nani aliyekupa? Akasema: Amenipa yule mtu anayeswali. Mtu (saw) akamuuliza tena: Alikupa akiwa katika hali gani? Akajibu: Alikuwa amerukuu. Hapo Mtume (saw) akapiga takbiri kisha wale wote waliokuwa msikitini hapo nao pia wakapiga takbiri. Mtume (saw) akasema: Ali bin Abi Talib ni walii wenu baada yangu.’
Wakasema: Tumeridhia Mwenyezi Mungu kuwa Mola wetu, Uislamu kuwa dini yetu, Muhammad kuwa Nabii wetu na Ali bin Abi Talib kuwa Imam na Walii wetu. Hapo Mwenyezi Mungu akateremsha aya inayosema: Na atakayemtawalisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini, basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndio watakaoshinda.’
*********
Na kufikia hapa wapenzi wasikiliza ndio tunafikia mwisho wa kipindi cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kwa juma hili, kipindi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ahsanteni na kwaherini.