Apr 03, 2024 02:12 UTC
  • Jumatano, tarehe 3 Aprili, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 23 Ramadhani 1445 Hijria sawa na Aprili 03 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, ilikamilika kazi ya uandishi wa kitabu cha ‘Jawaahirul-Kalaam’ ambacho kimejumuisha masuala muhimu ya sheria za Mwenyezi Mungu juu ya halali na haramu na kadhalika sheria mbalimbali za dini ya Kiislamu.

Ni vyema kuashiria kuwa, kitabu cha Jawaahirul-Kalaam kimebainisha kwa undani masuala mengi ya sheria kiasi kwamba hadi sasa hakuna msomi aliyeweza kuandika kitabu kama hicho. Kunukuu kauli za wasomi wakubwa wa sheria za Kiislamu na kuzitolea ushahidi kwa umakini wa hali ya juu, ni kati ya nukta zinazopatikana katika kitabu hicho. Ayatullah Muhammad Hassan Najafi, mtunzi wa kitabu hicho, alianza kazi ya uandishi wa kitabu cha Jawaahirul-Kalaam akiwa na umri wa miaka 25 na alitumia karibu muda wa miaka 30 katika uandishi wake na kupewa lakabu ya ‘Sheikhul-Fuqahaa.’ Kipindi cha maisha yake kulitawaliwa na hujuma za fikra potofu za genge la Uwahabi na watu wa kundi la Ikhbariyyun suala ambalo lilimfanya Ayatullah Muhammad Hassan Najafi kuelezea umuhimu wa kuwa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu. Ni baada ya hapo ndipo kukazaliwa fikra ya kuwepo Waliyyul Faqihi ‘walii kiongozi anayesimamia masuala ya sheria za Kiislamu. 

Muhammad Hassan Najafi

Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita Otto Von Bismarck mmoja kati ya shakhsia waliokuwa na nguvu na ushawishi mkubwa katika karne ya 19 barani Ulaya na Kansela wa Ujerumani, alivuliwa madaraka na Kaiser Wilhelm II aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Ujerumani.

Licha ya kuondolewa madarakani, aliendelea kubaki kwenye wadhifa huo kwa muda mchache, lakini baada ya kushadidi hitilafu kati yake na Mfalme Wilhelm II, Bismarck alilazimika kujiuzulu. Bismarck alifariki dunia mwaka 1898.

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Aprili 1941, mji wa Baghdad ulikombolewa na Rashid A'li Gilani kiongozi wa mrengo uliokuwa ukiwapinga Waingereza, baada ya kujiri mapigano kati ya wazalendo wenye uchungu wa nchi yao dhidi ya serikali ya London.

Gilani alikuwa akiungwa mkono na Ujerumani na kutokana na kutopata misaada kwa wakati mwafaka, vikosi vya Uingereza vilifanikiwa kuwakandamiza wafuasi wa wake.

Baada ya tukio hilo serikali ya Iraq ilijiunga na nchi waitifaki katika Vita vya Pili ya Dunia.

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita yaani tarehe 23 Ramadhani mwaka 1392 Hijria Qamaria, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai mwanafalsafa, arifu na faqihi mkubwa wa Kiirani alikamilisha kazi ya uandishi wa tafsiri kubwa na ya aina yake ya Qur’ani ya al Mizan.

Tafsiri hiyo ya Qur’ani ni moja kati ya tafsiri kubwa na makini sana za Qur’ani Tukufu na iliandikwa katika kipindi cha karibu miaka 20. Sifa kubwa zaidi ya tafsiri hiyo ni kwamba imefasiri Aya za Qur’ani kwa msaada wa Aya nyingine za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu.

Tafsiri hiyo kubwa na adhimu iliandikwa na Allamah Tabatabai kwa lugha ya Kiarabu na hadi sasa imetarjumiwa kwa lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiingereza na Kihispania. 

Allamah Muhammad Hussein Tabatabai

Siku kama ya leo miaka 22, iliyopita, yaani sawa na tarehe 3 Aprili 2002, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, katika ardhi za Palestina. Mashambulio hayo yalikuwa mwendelezo wa mashambulizi ya wiki kadhaa ya Wazayuni kwenye eneo hilo, kwa shabaha ya kuzima Intifadha ya wananchi wa Palestina. Kwenye mashambulio hayo ya majeshi ya Wazayuni huko Jenin, asilimia 70 ya mji huo ilibomolewa kabisa, mamia ya Wapalestina kuuawa shahidi na watu wengine wasiopungua 5,000 kukosa makazi.

Jinai za Israel huko Palestina

 

Tags