Apr 09, 2024 02:17 UTC
  • Jumanne, tarehe 09 Aprili, 2024

Leo ni tarehe 29 Ramadhani 1445 Hijria sawa na Aprili 09, 2024.

Tarehe 29 Ramadhani miaka 797 iliyopita alizaliwa Jamaluddin Hassan bin Yusuf aliyepea laqabu ya Allamah Hilli, alimu, mtaalamu wa Hadithi na mwanafasihi mkubwa wa Kiislamu.

Awali Jamaluddin alisoma elimu mbalimbali kama fiq’hi, usulul fiq’hi na hadithi kwa baba yake na kufikia daraja za juu katika nyanja hizo. Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi vya thamani kama “Tadhkiratul-Fuqahaa”, “Irshaadul-Adh’haan" na "Kashful Murad.”   

Siku kama ya leo miaka 638 iliyopita, alifariki dunia Nasiruddin Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn Furat, faqih, mwanahistoria na mhadhiri wa nchini Misri.

Ibn Furat alizaliwa mjini Cairo mwaka 735 Hijiria na kuanza masomo yake akiwa kijana mdogo. Msomi huyo alijikita sana katika masuala ya historia, kiasi cha kumfanya aandike vitabu mbalimbali katika uwanja huo. Miongoni mwa athari muhimu za Ibn Furat ni pamoja na kitabu kiitwacho ‘Taarikhud-Duwal wal-Muluuk’, kitabu ambacho kina historia na matukio ya karne ya sita Hijria.  

Tarehe 9 Aprili miaka 398 iliyopita aliaga dunia mwanafalsafa maarufu wa Uingereza, Francis Bacon.

Awali, Bacon alijishughulisha na masuala ya kisiasa na baadaye alikamatwa na kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kula rushwa. Kipindi cha kufungwa jela kilikuwa fursa mwafaka kwa Francis Bacon kudhihirisha kipawa chake. Mwanafalsafa huyo alitoa mchango mkubwa katika kueneza sayansi asili nchini Uingereza na kuhuisha sayansi na falsafa barani Ulaya.

Bacon ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha New Atlantis. Msomi huyo wa Uingereza alifariki dunia mwaka 1626. 

Francis Bacon

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, utawala ghasibu wa Israel ulifanya mauaji ya kinyama katika kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas.

Mauaji hayo yalifanyika wakati wa vita vya kwanza vya Waarabu na Israel na yalitekelezwa na Wazayuni wa kundi la Irgun lililokuwa likiongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Israel, Menachem Begin.

Eneo la Dier Yassin lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wazayuni kutokana na kuwa katika njia ya Baitul Muqaddas na karibu na pwani. Baada ya kukivamia kijiji cha Deir Yassin, Wazayuni hao waliwaua kinyama wakazi 270 ambao hawakuwa na hatia yoyote wa kijiji hicho.

Mauaji hayo yaliwalazimisha Wapalestina wengi wa eneo hilo kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukaririwa mauaji kama hayo ya kinyama. 

Mauaji ya Israel huko Deir Yasin

Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na 21 Farvardin 1367 Hijria Shamsia, ndege za kivita za Iraq ziliushambulia mji wa Marivan magharibi mwa Iran na kukilenga kijiji kimoja kwa mabomu ya kemikali.

Raia kadhaa waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika jinai hiyo ya utawala wa Saddam Hussein. Jamii ya kimataifa na hasa nchi za Magharibi zilinyamazia kimya jinai hiyo na badala yake zilitoa misaada zaidi ya silaha za kemikali kwa nchi hiyo.

Marivan

Miaka 32 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Waserbia wa Bosnia waliokuwa wakiungwa mkono na kusaidiwa na dikteta wa zamani wa Yugoslavia Slobodan Milosevic, walianza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo katika mji wa Belgrade.

Mauaji hayo yalianza baada ya kutangazwa matokeo ya kura ya maoni hapo tarehe Mosi Machi 1992 ambayo kwa mujibu wake asilimia 99 ya washiriki walipiga kura ya kujitenga Bosnia Herzegovina na Yugoslavia ya zamani. Hata hivyo Waserbia wachache wa Bosnia walipinga suala hilo la kuanzisha uasi kisha baadaye wakajitangazia mamlaka ya Seribia katika maeneo yao.

Milosevic aliwaunga mkono Waserbia na kuanzisha vita vikubwa zaidi vya mauaji ya kimbari barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Hadi vita hivyo vinamalizika mwaka 1995 zaidi ya Waislamu laki moja wa Bosnia walikuwa wameuawa kwa umati. Zaidi ya Waislamu wengine milioni mbili pia walilazimika kuwa wakimbizi.

Maelfu ya Waislamu waliuawa katika mauaji ya kimbari ya Belgrade.

 

Tags