Apr 14, 2024 06:13 UTC
  • Jumapili, Aprili 14, mwaka 2024

Leo ni Jumapili tarehe 5 Shawwal 1445 Hijiria, sawa na tarehe 14 Aprili 2024.

Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita yaani sawa na tarehe 5 Shawwal mwaka 60 Hijria, Muslim bin Aqil, binamu wa Imam Hussein (as) aliwasili katika mji wa Kufa moja ya miji ya Iraq, kwa shabaha ya kuwalingania wenyeji wa mji huo kwenye njia ya haki na kuchukua baia yao kwa ajili ya Imam Hussein (as).

Kabla ya hapo watu wa Kufa walikuwa wamemwandikia barua nyingi Imam Hussein (as) wakimuomba aende kwenye mji huo na awaongoze kwenye harakati dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Bani Umayyah. Baada tu ya Muslim bin Aqil kuwasili katika mji wa Kufa aliwasomea wenyeji wa mji huo barua ya Imam Hussein (as) iliyowakaribisha kujiunga na harakati ya kiongozi huyo.

Mwanzoni watu wa mji wa Kufa walikubali ujumbe wa Imam Hussein lakini baadaye walikengeuka. Mwishowe watu hao walimuacha peke yake Muslim bin Aqil na mjumbe huyo wa Imam Hussein akauawa shahidi na askari wa utawala wa Bani Umayyah.  

Siku kama ya leo tarehe 14 Aprili miaka 898 iliyopita alizaliwa Ibn Rushd, mwanafalsafa na mwanafikra maarufu wa Kiislamu wa Andalusia (sehemu ya Uhispania ya sasa).

Baba na babu wa Ibn Rushd, wote walikuwa makadhi huko Andalusia. Akiwa kijana alipata kusoma elimu mbalimbali za zama zake na kuutabahari zaidi katika elimu za hisabati, sayansi, nyota, mantiki, falsafa na udaktari. Kufuatia hali hiyo alipewa kipaumbele na watawala wa silsila ya Muwahhidun waliokuwa wakitawala Andalusia wakati huo, na kuteuliwa kuwa kadhi wa wa Córdoba, mji mkuu wa Andalusia. Hata hivyo mwishoni mwa umri wake alichukiwa na watawala na hatimaye akapelekwa uhamishoni. Mielekeo ya Ibn Rushd ilielemea sana kwenye fikra za Aristotle.

Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na ‘Tahaafut al-Tahafat’ ‘Kitabul-Kulliyyaat’ katika taaluma ya tiba na ‘Faslul-Maqaal.’ Ibn Rushd alifariki dunia Disemba 1198 sawa na mwezi Swafar 595 Hijiria.   

Siku kama ya leo miaka 178 iliyopita alizaliwa Friedrich Carl Andreas, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na Iran huko nchini Ujerumani.

Baada ya kufahamiana na mtaalamu mmoja wa masuala ya mashariki wa nchini Denmark, alivutiwa sana na utamaduni wa Iran ambapo alianza kufanya utafiti kwa kipindi cha miaka minne katika uwanja huo. Katika kukamilisha masomo yake aliamua kutembelea nchi za Iran na India sambamba na kujifunza lugha ya Kifarsi.

Kwa karibu kipindi cha miaka 30 alikuwa mwalimu wa lugha ya Kifarsi katika Chuo Kikuu cha Göttingen nchini Ujerumani ambapo wanafunzi wake walipata kufahamu tamaduni za thamani za Iran. Mtaalamu huyo wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ujerumani alifariki dunia mwaka 1930.   

Friedrich Carl Andreas

Katika siku kama hii ya leo miaka 134 iliyopita muungano wa Pan American ambao baadaye ulibadili jina na kujulikana kama Jumuiya ya Nchi za Amerika uliasisiwa.

Nchi wanachama wa jumuiya hiyo zilikuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali hadi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baada ya vita hivyo kumalizika Jumuiya ya Nchi za Amerika iliundwa kutokana na kuweko haja ya kupanuliwa zaidi mashirikiano kati ya nchi hizo. Pamoja na hayo yote kitu kinachoitia wasiwasi jumuiya hiyo ni satwa na ushawishi mkubwa wa Marekani katika jumuiya hiyo na hatua yake ya kukitumia vibaya chombo hicho kwa maslahi yake ya kisiasa. Kwa sababu hiyo nchi wanachama zinafanya jitihada kubwa za kupunguza ushawishi wa Marekani katika jumuiya hiyo.   ***

Miaka 22 iliyopita katika siku kama leo, Hugo Chavez rais wa zamani wa Venezuela alirejea nchini kwake na kushika hatamu za uongozi baada ya kufeli jaribio la mapinduzi ya kumuondoa madarakani.

Chavez Aliingia madarakani mwaka 1999 na kufanya mabadiliko makubwa kwa maslahi ya tabaka la chini. Vilevile alichukua hatua za kusimamia mashirika ya mafuta ya Kimarekani yaliyokuwa yakichimba mafuta ya nchi hiyo. Siasa za kujitegemea za Chavez ziliikasirisha sana Washington. Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana Marekani ilipanga na kuratibu mapinduzi mnamo tarehe 12 Machi mwaka 2002.

Licha ya mapinduzi hayo kupata mafanikio katika hatua za awali, lakini wananchi wa Venezuela waliokuwa wameridhishwa na mabadiliko ya Chavez, walipinga uingiliaji wa nchi za nje katika masuala ya ndani ya nchi yao. Hugo Chavez alifariki dunia Machi 5 mwaka 2013 kutokana na maradhi ya saratani akiwa na umri wa miaka 58. 

Hugo Chavez